POROJO za anko Sagati: Ahsanteni wasomaji wangu, karibuni mwaka mpya!

LEO ni jumapili ya pili ya mwaka 2017. Nichukue nafasi hii kuwashukuru wasomaji wangu wote ambao tumekuwa wote mwaka uliopita.

Naamini kwamba nilijitahidi kuwapigisha porojo zenye ukweli ambazo zimefanyiwa utafiti wa kina. Huu ni mwaka mwingine, niwaombe tena wasomaji wangu, msichoke kuendelea kuitupia jicho safu hii. Nawaahidi kuendelea kuwaletea visa, vituko na miksa mbalimbali inayoendelea ndani na nje ya nchi yetu.

Lengo langu ni kukuburudisha wewe msomaji wangu ukiwa sehemu yoyote ile ambako gazeti hili linafika. Najua mwaka huu umeanza kwa watu wengi kulia ukata kutokana na mzunguko wa fedha kupungua. hapo ulipo unalalamika fedha imekuwa ngumu, mafundi, wachuuzi, wamachinga na wapiga dili wote ni kulalamika tu kwamba pesa imekuwa ngumu.

Hivyo mifuko ya watu wengi iko tupu, kibaya zaidi mwezi huu wa kwanza ambao wazazi wengi wanatoboka kwa kulipa ada za watoto ndio malalamiko yamezidi. Mwaka 2016 umepita kwa mambo mengi ambayo kuna baadhi hayatasahulika kamwe.

Kubwa ambalo halitasahulika licha ya kulia sana suala la ukata, lakini pia utumbuaji majipu unaofanywa na mzee wa Magogoni nao hautasahulika kamwe. Ndugu zetu wengi, marafiki na jamaa ambao walikuwa kwenye nafasi za juu katika maofisi ya umma tumewapoteza. Tumewapoteza kwa sababu wamekuwa katika janga hilo la kutumbuliwa.

Wengine waliahidiwa kutafutiwa kazi nyingine, lakini hadi mwaka umeisha hawajatafutiwa hiyo kazi nyingine; wako vijiweni wanasubiri kutafutiwa hizo kazi nyingine. Najua hawa waliotumbuliwa ni ndugu na rafiki zetu, tuliumia sana na kuhuzunika kwa sababu wana familia ambazo zinawategemea.

Lakini hatuna jinsi kwa kuwa wameachiwa nguvu na akili zao naamini kwamba maisha yao yataendelea kuwa murua kama ilivyokuwa hapo awali. Rais mwenyewe ameshaahidi kuendelea kutumbua majipu, tujipange yawezekana mimi na wewe ndio tutakaofuata. Wewe angalia mwaka huu tu ameshatumbua majipu pale Tanesco.

Na ameshamuahidi baba askofu pale Bukoba kwamba ataendelea kutumbua majipu kwa kuwa bado yapo ndani ya serikali. Kwa hiyo mwaka huu mpya kwa kuwa tayari milango ya majipu imeshafunguka, yawezekana kufikia mwisho wa mwaka majipu ambayo yatatumbuliwa yanaweza kuwa mengi zaidi kuliko hata ya mwaka 2016.

Lakini ni mwaka ambao pia hautasahulika kwa kuwa nidhamu ndani ya serikali imebadilika. Leo hii katika hospitali zetu ambazo mgonjwa alikuwa hatibiwi hati ndugu watoe kitu kidogo, leo hii hilo jambo halipo tena. Watumishi huko kwenye maofisi wanaogopa kupokea kitu kidogo, hawajui nani ni nani na kwa wakati gani.

Kila mtu hamwamini mwenzake huko maofisini jambo ambalo limerejesha nidhamu kwa watumishi wa umma. Yaani ni kwamba kila mtumishi wa umma kwa sasa anaona cheo alicho ni dhamana na ni mali ya umma, siku na wakati wowote anaweza kunyang’anywa akapewa mtu mwingine. Hakuna tena mtu ambaye anabinua mabega na kujiona yeye ndiye yeye.

Kwa sisi wasaka nyoka mambo pia yamenyooka, kiburi cha mawaziri, makatibu waku kutotoa ushirikiano hakipo tena, leo hii hakuna kigogo ambaye anaficha habari za serikali, wamekuwa karibu na midia na hivyo kurahisha utendaji wetu.

Kwa haya mambo ambayo yalionekana mwaka 2016, ni vizuri yakaendelea mwaka huu, sisemi kwamba ukata uendelee kwenye mifuko yetu, hapana ila nidhamu ambayo watumishi wa umma wameionesha sasa iwe mara dufu.

Katika hali ya namna hii nasema kwamba mheshimiwa Magufuli udumu, endelea kutumbua, endelea kusimamia nidhamu ndani ya serikali na endelea kutetea wanyonge ambao ndio wanaokuunga mkono kwa wingi. Mungu atakusimamia katika shughuli zao za kunyoosha nchi.