Dawa za kulevya zilivyotikisa bungeni

“IENDESHWE kwa mbinu yoyote ile, kampeni dhidi ya dawa za kulevya ni ya kuungwa mkono na kila Mtanzania,” hayo ni maneno kuntu aliyoyasema Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka wiki iliyopita nilipokuwa ofisini kwake.

Mtaka aliyasema hayo wakati akizungumzia athari za dawa za kulevya kwa Watanzania, wakiwemo wanamuziki na wasanii, akisema ukichunguza vyema utagundua kwamba familia nyingi nchini zilishakumbana na athari za dawa za kulevya.

Ilikuwa ni wakati kundi la mwanamuziki wa muda mrefu nchini, Ally Choki alipomtembelea ofisini kwake, ambapo mkuu huyo wa mkoa alichukua muda huo pia kuwaasa wanamuziki kujitenga na dawa za kulevya.

Wanamuziki ni moja ya makundi ya kijamii yaliyo katika hatari kubwa ya kutumbukia katika utumiaji au usafirishaji wa dawa hizo zinazoua nguvu kazi ya nchi kila kukicha.

Bila kutaja majina, mkuu huyo wa mkoa alisema kuna wanamuziki kadhaa na hata wasanii wa fani zingine ambao wamepotea kabisa katika fani zao na wengine kufariki dunia kutokana na kubwia ‘unga’.

Maneno ya mkuu huyo wa mkoa yalinikumbusha mjadala mmoja niliowahi kuusoma kwenye kundi moja la whatsApp ambapo kulikuwa na mjadala mkali ukihusu kama hatua zilizokuwa zinafanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kupambana na dawa za kulevya zilikuwa sahihi au la.

Mjadala huo haukuwa tofauti sana na ule uliolipuka bungeni ambapo baadhi ya wabunge walikuwa wanampinga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam wakidai hatua anazochukua katika kampeni hiyo, siyo za kisheria huku wengine wakiziunga mkono.

Kwa mfano, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto pamoja na kukiri kwamba tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na linagusa nchi nzima, alidai kwamba kampeni hiyo inahitaji mikakati ya kupambana na siyo kuwaweka rumande wale aliodai kuwa ni waathirika ambao wanahitaji kupatiwa matibabu.

Naye Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliunga mkono vita iliyoanzishwa dhidi ya wafanyabiashara na watumiaji wa dawa hizo, lakini akasema haridhishwi na utaratibu mzima uliotumika katika vita hiyo.

Hapo ndipo mgogoro wangu na waheshimiwa hao ulipo kwani wote waliishia kusema kwamba kampeni hiyo inahitaji mikakati lakini wao hawakutaja mikakati waliyo nayo! Mimi, kama ambavyo niliguswa na maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, ninasimama kwa wale wanaosema kwamba dawa za kulevya ni janga, ni tatizo hatari katika jamii.

Ni tatizo ambalo limeonekana kuwa mfupa mgumu kwa baadhi ya viongozi wetu.

Hivyo, kampeni yoyote ya kupambana na dudu hili hatari, lazima ichukuliwe kama kampeni zingine kama kunapolipuka gonjwa hatari katika jamii. Kunapotokea mlipuko wa kipindupindu au ebola, mamlaka zinachukua hatua ambazo ukiziangalia kwa undani zinavunja sheria zilizopo lakini zinaookoa jamii.

Kwa mfano, kwenye kampeni dhidi ya mlipuko wa kipindupindu, mamlaka mara nyingi huwa zinapiga marufuku uendeshaji wa biashara za vyakula (ambazo kimsingi ni halali) au kuzuia watu wa eneo fulani kwenda sehemu nyingine.

Ni nadra kusikia watu wakilalamikia kampeni hizo kwa sababu wanajua “hakuna namna nyingine.” Kwa muktadha huo, kampeni aliyoianzisha mkuuu wa mkoa wa Dar es Salaam na kuikabidhi kwa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini ni ya kuungwa mkono bila kujali mbinu zinazotumika.

Na mimi ninauliza kwamba kwa nini watumiaji wa dawa za kulevya tunawaita wagonjwa badala ya wahalifu wanaotenda kosa kinyume cha kifungu namba 17 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Namba Tano ya mwaka 2015? Nani anawaambia watu kwamba huwezi kumpata muuzaji kwa kumkamata mnunuzi, yaani mtumiaji? Sitaki unijibu hayo maswali lakini ninaungana pia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, Dk Benson Bana, ambaye amekaririwa akisema kwamba kutokana na madhara yake, Watanzania wanapaswa kuunga mkono mapambano dhidi ya dawa za kulevya bila kuhoji mbinu zinazotumika.

Msomi huyo alikaririwa na gazeti hili akisema: “Hii vita ni yetu sote na kila anayeitakia mema nchi hii, huu si wakati wa kuhoji nani anatumia mbinu gani bali ni wakati wa kushiriki mapambano, kila mtu kwa nafasi yake na kwa mbinu yake alimradi tuweze kutokomeza wale wanaojiohusisha na biashara hii hatari.”

Na mimi, kama alivyosema Dk Ban a, ninaamini kwamba wale wanaohoji mbinu zinazotumika katika mapambano haya hawajaona waathirika wa dawa za kulevya au pengine ni wananufaika wa dawa hizo kama si kutaka kunufaika kisiasa! Dk Bana alidokeza jambo ambalo mimi nilidhani pia linapaswa kuwa kwenye mawazo ya wabunge wetu kwamba hii ni vita na siku zote “vita haina macho.”

Kisha msomi huyo akakaririwa akisema maneno haya yanayopaswa kuandikwa kwa wino wa dhahabu: “Mbinu yoyote itakayotumika kuwatoa pangoni watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ni mbinu halali tu na lazima ihalalishwe kama wao wanavyotumia mbinu zozote zile hata kama ni kutoa watu roho ili waendelee na biashara hiyo.”

Wabunge wetu, heri wangelishauri mbinu zaidi za kutumia katika kupambana na dawa za kulevya kama alivyofanya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mtaka, wakati anazungumza na kundi la Choki, aliyeshauri wanamuziki nchini watunge vibao kwa wingi vinavyoelezea madhara ya dawa za kulevya.

Hata Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali, Dk Jim Yonazi aliwashauri akina Choki kuunda Baraza la Washauri likihusisha wanamuziki wakongwe kama King Kiki, Zahir Zorro na watu wengine wasioko kwenye tasnia ya muziki ili wawe wanatoa ushauri kwa mwanamuziki anayejiingiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya au matatizo mengine.

Na mimi ninashauri kwamba ni vyema kampeni dhidi ya dawa za kulevya iambatane na mabango mbalimbali, barabarani, kwenye kumbi za starehe na viwanja vya michezo yanayoelezea athari za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuwakumbusha hata watumiaji kwamba ni kosa kisheria kutumia dawa za kulevya.

Kampeni iwe kali hata kwenye televisheni na redio, kiasi cha kuwafanya watumiaji wa dawa za kulevya, siyo tu kuona hatari inayowakabili, bali kujiona ni watu wasiotakiwa katika jamii yetu, hatua itakayowaogopesha watu wengine kutumia au hata kusafirisha.

Kampeni ya kuwanyanyapaa wavuta sigara, kusambaza mabango lukuki hadi kwenye vyoo vya umma na kuwapa adhabu kali wanaovuta sigara kwenye maeneo ya umma imesaidia sana kupunguza idadi ya wavuta sigara nchini Australia. Sisi tunaweza kuleta kampeni kama hiyo kwenye dawa za kulevya.

Ingawa nimesoma daktari mmoja akisema ni vyema watumiaji wa dawa za kulevya wasipelekwe polisi bali hospitali, mimi nashauri, kama ushauri huo utaonekana unafaa basi waende huko wakiwa na pingu mikononi kwa sababu kutumia dawa hizi ni kosa kisheria.

Na Hamisi Kibari TUKUBALIANE KUTOKUBALIANA Dawa za kulevya. Mbinu yoyote dhidi ya dawa za kulevya ni halali