Wachimbaji wadogo wampongeza Magufuli

WACHIMBAJI wadogo wa madini ya tanzanite mkoani hapa na Manyara wamempongeza Dk John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumwomba afute vibali vyote vya wafanyabiashara kutoka India wanaoingia nchini kununua madini hayo.

Walisema wengi wa raia hao kutoka nje si waaminifu kwa rasilimali za nchi, kwani wanasafirisha madini hayo kwa njia za panya kwa kushirikiana na matajiri wa madini Watanzania wenye asilia ya Kiasia waishio nchini, hivyo kuikosesha serikali mapato.

Mmoja wa wachimbaji hao, Juma Mnzava alisema, vibali hivyo hutolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Idara ya Uhamiaji kwa raia hao kutoka India na wengine China na kwamba wamejaa katika mji wa Mirerani na Arusha wakinunua madini hayo kwa ajili ya kuyasafirisha nje, huku wakikwepa.

Mnzava alidai raia hao wako nchini wakihifadhiwa na matajiri hao Watanzania na wanafanya biashara hiyo haramu, jambo linalolifanya soko la dunia la madini hayo kumilikiwa nao huku wazawa wakishindwa kufanya biashara hiyo nje.

Alisema, vibali hivyo vya miezi mitatu vinavyotolewa zaidi kwa raia hao wa India vinapaswa kufutwa kwa maslahi ya nchi, kwani kwa asilimia kubwa wameteka soko la madini ya tanzanite katika minada mikubwa nje kwa kuuza madini hayo kwa bei ya chini.

Alisema kwa mzawa kufanya biashara hiyo kwa sasa ni ngumu sana kwa kuwa anapitisha madini yake kwa njia halali, lakini bei anayotaka kuuza nje ni kubwa tofauti na raia wa India waliopitisha kwa njia haramu.

“Sisi wachimbaji wadogo tunampongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kutuongoza Watanzania, ila tunamwomba afute vibali vya miezi mitatu vinavyotolewa kwa raia wa India kwa sababu wanaihujumu nchi kwa kukwepa kodi,” Mnzava alisema.

“Hawa wageni wameteka soko la dunia la madini katika minada mikubwa nje ya nchi kwani wanauza kwa bei poa kwa sababu wamenunua madini yetu na wamepitisha madini hayo kwa njia ya panya, hivyo ni ngumu kwa mzawa kuuza madini nje kwa kuwa amenunua kihalala na kulipa kodi kihalali,’’ alisema Mnzava.

Naye Athumani Matambi mbali ya kumpongeza Rais Magufuli, alimwomba ahakikishe kampuni kubwa za madini nchini zinalipa kodi halali ili kodi hizo zifanye mambo ya maendeleo nchini.

Matambi alisema pia kuwa biashara ya madini hayo kwa sasa imeingiliwa na kuporwa na raia wa India na China kwa sababu ya kuruhusu wageni hao kwenda moja kwa moja migodini kununua madini.

Alisema, wazawa hawawezi kushindana na matajiri hao wa nje kwa sababu ya kuwa na fedha za kutosha kutokana na kukopeshwa fedha nyingi na benki zao na kuja nchini kufanya biashara hiyo.

“Iwapo serikali kupitia Rais Magufuli itafuta vibali hivyo na kutoa mwanya kwa wazawa kukopeshwa mitaji mikubwa na benki uko uhakika nchi kuwa na pato la kutosha,” alieleza.

Mchimbaji mwingine, Elibariki Mbise alisema kuwa Rais Magufuli anapaswa kuangalia uwezekano na kupunguza kodi katika vifaa vya uchimbaji kutoka nje kwani kwa sasa zana hizo bei yake iko juu sana.

Mbise alisema, iwapo serikali itazingatia hilo kuna uwezekano mkubwa wa mchimbaji mdogo kufanya biashara hiyo kwa maslahi ya wachimbaji na hatimaye kulipa kodi baada ya kuzalisha.