21Mei2013

 

Mjajalo wa Katerero bungeni!

NAKUMBUKA vizuuuri wakati naingia katika kilinge hiki cha upaparazi, nikazoea kutumwa kutafuta habari, nilizoea saana kwenda katika ofisi ya mheshimiwa mmoja ambaye alijizolea umaarufu kutokana na utendajikazi wake wa wazi na ukweli.

Uzuri na ubaya wa mheshimiwa huyo ilikuwa ni kwamba kama hajaona vinasa sauti vya jamaa zetu wa ARATIDII hakuwa tayari kuzungumza na ninyi mliowahi na vijinotibuku vyenu na kalamu, aliwaona kama mnammalizia hewa yake kidogo aliyotengewa.

Baada ya kuwa mmetulia vitini mkisubiri kusikia ya siku hiyo kutoka kwa mheshimiwa sana, yeye alifika na kuhoji: “Wa ARATIDII wamefika?”

Kama hawapo alikuwa tayari kujitolea gari lake na dereva aende PUGURODI kuwafuata ndipo aanze mambo yake! Usumbufu gani huu, hivyo ndiyo sababu hata hao jamaa zetu wa ARATIDII nao walikuwa wakideka, kwamba mkutano wa mheshimiwa hautaanza mpaka aone vinasa sauti.

Hivyo walijikongoja polepole na hata kutegea lije gari la mheshimiwa kuwachukua. Tulivumilia kwa sababu wakati huo magazeti ya kila siku yalikuwa mawili tu, letu na la Kidhungu, hivyo lazima walisubiriwa mpaka wafike ndipo kazi ianze.

Nasi tulilazimika kuwapo ili kuhakikisha habari inapatikana ili gazeti litoke tena iwe FRONTIPEJI. Mzee wa Kiraracha bwana alitukosha! Kumbe hiyo haikuishia hapo, hata leo ukienda katika mikutano ya waheshimiwa hao au kama hao, lazima wataulizia kama wa AITIVII na TIBISII wamefika.

Ninyi hata mbebe kalamu kumi kumi na notibuku ishirini ishirini, mtaula wa chuya mpaka wafike hao! Nia na lengo lilikuwa, kwa mfano yule mheshimiwa wa zamani, kuhakikisha kwamba ifikapo saa tatu usiku katika kipindi cha MAJIRA cha ARATIDII asikike akimwaga sera zake huku akiorodhesha waliokamatwa na sungusungu!

Ilikuwa kazi kwelikweli! Hawa wa sasa, wao wanataka ifikapo taarifa ya habari ya saa mbili usiku waonekane kwenye kioo wakimwaga sera zao na kuonesha hata mabunduki waliyokamata kutoka kwa majambawazi.

Tabia hii ipo tu hata kwangu, kwako, kwake, kwao na kwetu! Hebu angalia, unaingia katika ukumbi wa dansi, mara unashangaa kusikia mtu anatajwa jina, mathalan MATIMOOO, unamwona mtu amevalia nyeupe pee anajongea jukwaani kwa mnato na kumwaga minoti kwa wanamuziki.

Wanaitwa mapededjee hao! Unasikia mtu anarushwa na mwimbaji PAPA MSOFEE, NDAMA MUTOTO YA NG’OMBE, nakadhalika nakadhalika, unawaona haoo wanapanda jukwaani na kumwaga minoti.

Hata kama ni wewe unarushwa angani au hewani hivyo, unafanyaje kama si kujitokeza? Sikieni hata hawa watangazaji wetu wa vipindi hivi vya sasa katika redio zetu hizi, hawana cha kusema au hata kama wanacho, kikipungua utasikia wanaanza kutaja majina ya washikaji zao na jioni wakikutana moja baridi moja moto isikose.

“Vipi ulisikiliza kipindi leo? Nimekurusha ile mbaya.” Ukisikia hivyo ujue kiu tayari! Au nyimbo zetu hizi za bendi zetu hizi, tena zilizorekodiwa, ni majina, majina, majina tu, ndiyo yanasikika nusu wimbo, kurushana hewani kwa saana mpaka basi! Yote haya ni kutafuta sifa, yote haya ni kuganga njaa, yote haya ni kutaka kujulikana tupo!

Ugonjwa huu ndio umefika hata katika Bunge letu leo, watu wanaona kwa kuwa wanamulikwa, basi wafanye fujo, vituko, twimbwili tu ili wajulikane wapo bungeni, pengine ndiyo sababu mmoja wao akasema wengine wanakula ndum!

Nakumbuka zamani zile Bunge lilipokuwa halirushwi, watu walikuwa wastaarabu kabisa, wakizungumza masuala yenye hekima na busara, yakiwahusu wananchi waliowachagua, yakigusa mustakabali na ustawi wa nchi, bila kujali wanarushwa moja kwa moja au nini.

Na kwa kweli tulikujawasikia jioni tu tena kwenye taarifa ya habari au kipindi maalumu cha KUTOKA BUNGENI, hapo ndipo tuliweza kuwasikia akina KIMBAU wakiichachafya sirikali lakini kwa pointi.

Tumekuja kusikia haya ya FUNGA MLANGO na ya MGONJWA WANGU, katika Bunge hili la sasa, lenye mchanganyiko maalumu wa vijana na wazee, wasichana na wanawake, walevi na walokole, wasanii na watawa.

Tunawashuhudia sasa wanaotaka kila siku waonekane wakifanya fujo eti mpaka kieleweke, wamo wanaotaka eti Spika waliyemchagua wenyewe na Naibu wake, eti wang’olewe na wananchi kwa kupitia simu za mkononi! Hamjalewa kweli?

Hivi hizi sifa mnataka zitufikishe wapi? Aingiaye kwa demokrasia hutoka kwa demokrasia na si kwa domokrasia jamani au?

Mimi hata msiporushwa laivu najionea sawa tu, kwa sababu vurugu zenu zinawafundisha watoto kuwa ili uwe mbunge lazima uwe mfanya fujo!

Wanashindwa kutofautisha Bunge na Mjajalo wa Katerero! Tehetehe! Eti wabunge, thubutuuu!

Alamsiki.