19Mei2013

 

Mungu bariki uchaguzi wa Kenya uwe wa amani

KESHO wananchi wa Kenya watapiga kura kuchagua rais na wabunge katika uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano.

Kwa kuwa Afrika ni moja tunapaswa kuombea uchaguzi huo uweze kufanyika katika hali ya amani na utulivu ili kuepuka ghasia za kisiasa kama zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2007.

Katika uchaguzi wa mwaka 2007 Kenya iligubikwa na ghasia ambazo zilisababisha watu zaidi ya 1,500 kupoteza maisha, maelfu kujeruhiwa na wapo waliopoteza makazi yao na wengine kuishi uhamishoni kama wakimbizi.

Hata hivyo baada ya uchaguzi huo, Kenya imejitahidi kuboresha mfumo wa demokrasia kwa kuifanyia marekebisho Katiba ya nchi, kuboresha Mahakama na Tume huru ya Uchaguzi.

Ili uchaguzi huo uweze kuwa huru na wa haki ni kila kundi linapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia haki ili kufanya maamuzi yenye manufaa kwa Taifa.

Wananchi wa Kenya wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura mgombea mwenye sifa na uwezo wa kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijao.

Tume ya uchaguzi inapaswa kusimamia uchaguzi huo ili uweze kufanyika kwa huru na haki ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kura zinahesabiwa bila udanganyifu na matokeo kutangazwa wakati muafaka pasipo kupendelea chama chochote.

Wanasiasa na hasa wagombea wa nafasi ya urais wanapaswa kuweka mbele maslahi ya Taifa na kukubali matokeo kwa kuwa asiyekubali kushindwa sio mshindani.

Uchaguzi uliopita ulidhihirisha wazi kuwa katika migogoro ya kisiasa wanaoumia zaidi ni wanawake na watoto wasiokuwa na hatia.

Tunaimani kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa amani na utulivu kama kielelezo cha ukomavu wa demokrasia nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla. Mungu bariki uchaguzi wa Kenya uwe wa haki, usawa, amani na utulivu.