Tozo za ovyo kwa wakulima zafutwa

SERIKALI imechukua uamuzi wa kufuta tozo zote za hovyo dhidi ya wakulima ikiwemo tozo ya vifungashio ya asilimia 15 ya zao la korosho ili kuwezesha wakulima wote nchini hasa wa mazao ya biashara kuzalisha kwa faida.

Aidha, Serikali hiyo ya Awamu ya Tano imebainisha kuwa imejipanga kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri kwa wakulima nchini ili sasa waanze kuzalisha kwa tija tofauti na miaka ya nyuma.

Hayo yalisemwa bungeni Dodoma jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la msingi na la nyongeza la Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani (CUF). Katika maswali yake mbunge huyo pamoja na kuishukuru serikali kwa kuondoa tozo kadhaa katika zao la korosho, alitaka kufahamu Serikali imekuwa ikiendelea kumkata mkulima wa zao hilo asilimia 15 ya tozo ya bei ya soko hali ambayo bado ni mzigo kwa mkulima.

Pia alitaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa zao la korosho ambao mazao yao yamepotea kwenye maghala, wakati waliosababisha upotevu huo ni serikali kwa kuweka tozo ndogo katika maghala hayo.

Akijibu maswali hayo, alisema tayari serikali imeamua kufuta tozo zote za hovyo kwa wakulima ikiwemo tozo hiyo inayolalamikiwa inayotumika pia kwa ajili ya vifungashio na itaingizwa rasmi kwenye mfuko wa wakfu unaosimamia mazao ya korosho. Alisema tozo nyingi zilipangwa kwa ajili ya kuvuruga mfumo na kusababisha wananchi wauchukie mfumo uliopo unaosimamia zao la korosho.

Alisema mfuko huo wa wakfu uliundwa na wadau wenyewe wa korosho na unachangiwa na tozo za korosho zinazouzwa nje ya nchi kwa asilimia 65 inayotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Mfuko huu wa wakfu kwa asilimia zile 65 sasa hivi una hela nyingi sana kwa ajili ya kukamilisha malengo yaliyopangwa na wadau ambayo ni kuhakikisha masoko ya zao la korosho yanapatikana, kuhakikisha pembejeo na mbegu zinapatikana na kusimamia kupanua mashamba ya korosho,” alisisitiza.

Kuhusu korosho zinazopotea kwenye maghala, Waziri Mkuu alikiri kuwa uko uendeshaji wa hovyo wa vyama vya msingi na vile vikuu vinavyosimamia korosho. Alisema mifumo inayotumika kwenye maghala mara nyingi haisimamiwi na serikali bali na vyama vya ushirika ambavyo vimeundwa na wakulima wenyewe ili kusimamia namna ya kuuza mazao yao.

“Sasa wakulima wote waliopoteza korosho wajibu wao ni kuwauliza viongozi wao wa vyama vya msingi na vikuu kupitia mikutano yao. Na pale wasiporidhika na majibu yao wanachama wana wajibu wa kuwaburuza mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema.

Alisema hatua zitakazochukuliwa na mahakama ndio zitakazothibitisha uwepo wa viongozi wa hovyo katika mashirika na vyama hivi vya mazao. Alisema serikali imejipanga kudhibiti vitendo vyote vya hovyo dhidi ya wakulima wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika katika mazao yote ya biashara ikiwemo pamba, korosho, kahawa na chai, ili kuhakikisha mazao hayo yanaipatia mapato serikali na tija kwa wakulima wake.