Mradi wa DMDP kutekelezwa Julai

MKOA wa Dar es Salaam utaanza rasmi utekelezaji wa Mradi ya Uendelezaji wa Jiji (DMDP) katika mwaka wa fedha 2016/2017. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema hayo jana akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema mradi huo umetokana na serikali kuingia mkataba na Benki ya Dunia wa thamani ya dola za Marekani milioni 300 kutekeleza mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano. “Sio fedha hizo tu tulizopata kwa ajili ya mradi huo tumepata pia dola za Marekani milioni tano kutoka Mfuko wa Maendeleo ya nchi za Nordic na serikali yetu inachangia dola za Marekani milioni 25.3 kwa ajili ya mradi huo,” alisema Makonda.

Alisema madhumuni ya mradi wa DMDP ni kukabiliana na changamoto zinazolikabili Jiji la Dar es Salaam kwa kutilia mkazo uboreshaji wa huduma za jamii kama miundombinu ; na kujenga uwezo wa manispaa za jiji katika utoaji huduma, kuchangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kukabili matukio makubwa ya dharura.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, walifanya usanifu mbalimbali na kufuata vigezo muhimu bila kuangalia umaarufu wa eneo na itikadi na miradi hiyo itaunganishwa katika maeneo ya watu wenye kipato kidogo na yaliyojengwa kiholela pamoja na kuunganisha wilaya na mkoa.

Aliongeza kuwa fedha hizo zitagawanywa katika manispaa zote za Jiji ambazo watatumia kujenga barabara za mlisho (feeder road) zenye urefu wa kilometa 65.6, ujenzi wa mitaro mikubwa yenye urefu wa kilometa 31.8 na ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 145.