Mayanja wa Simba aipongeza Yanga

KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja amekuwa wa kwanza kuwapongeza watani zao wa jadi Yanga kwa kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2015/16.

Simba inashika nafasi ya pili baada ya jana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipokonya Azam pointi tatu baada ya kumchezesha Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano walipocheza dhidi ya Mbeya City.

Simba kwenye msimamo ikiwa na pointi 58, katika michezo 26 waliyocheza itashuka dimbani Jumapili kuumana na Mwadui FC, ya Shinyanga.

Akizungumza na gazeti hili, Mayanja alisema hana budi kuwapongeza Yanga kwa sababu mpira siyo vita na siku zote uadui wa soka upo ndani ya dakika 90 baada ya hapo watu wote watu hugeuka marafiki na kusahau yaliyotokea ndani ya mchezo.

“Najisikia vibaya sana kuona malengo niliyotarajia kupata nikiwa na Simba msimu huu yapo ni vigumu kutimia, lakini sina budi kuwapongeza Yanga ambao ndiyo wanaoonekana kuwa katika nafasi nzuri ya ubingwa na hiyo inatokana na kazi nzuri waliyoifanya bila kujali upinzani wetu nao,” alisema Mayanja.

Kocha huyo raia wa Uganda, alisema ingawa wapo katika matumaini madogo ya kubeba ubingwa lakini bado mikakati yao ni kushinda mechi zao nne zilizobaki ili angalau waweze kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili licha ya kwamba haina nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Mayanja alisema kitu kizuri kwao ni kuona wanapambana hadi mechi ya mwisho bila kukata tamaa na mwisho wa msimu watajua wamemaliza wapi na kujitathmini mapungufu waliyokuwa nayo ambayo yalisababisha kushindwa kufikia malengo waliyojipangia.

“Kama timu hatupaswi kukata tamaa, nimewaambia wachezaji wangu lazima tupambane hadi siku ya mwisho kuhakikisha tunashinda mechi zilizobaki ingawa nafasi ya ubingwa kwetu ni ndogo, lakini siyo mbaya hata tukimaliza nafasi ya pili kwani tunajiwekea rekodi nzuri kwa siku zijazo,” alisema.

Mayanja ametua Simba mwishoni mwa mzunguko wa kwanza msimu huu akichukua nafasi ya Dylan Kerr, na aliweza kuibadilisha timu hiyo kwa kushinda mechi saba mfululizo na kufanikiwa kuongoza ligi lakini baadaye mambo yalikuwa tofauti katika mechi za mwishoni.