Hoja ya walipwa pensheni izingatiwe

KATIKA gazeti letu la leo kuna habari tumeichapisha ya wastaafu wanaohakikiwa, wakiiomba serikali kuwafikiria nyongeza katika pensheni wanayopewa.

Ombi la kutaka nyongeza hiyo linatokana na ukweli kuwa hali ya maisha katika taifa hili kwa sasa imepanda wakati wastaafu hao pensheni yao ipo palepale.

Mathalani, mstaafu wa jeshi alisema kwamba analipwa Sh 124,000 kwa mwezi tangu alipostaafu jeshi mwaka 2009.

Kiukweli, fedha hizo kwa mtu ambaye amelitumikia taifa katika utamu na machungu yote, ni fedha kidogo sana hazimtoshi hata kwenda kufanya manunuzi ya chakula cha wiki mbili.

Mwanajeshi huyo ni mfano mdogo wa watumishi wa umma na serikali kuu ambao wanaishi kwa pensheni baada ya kustaafu kwao.

Ingawa inaweza kuonekana hapa si mahali pake kujadili, lakini ni dhahiri kwamba wastaafu wetu wanatakiwa kuenziwa hasa kutokana na mchango wao mkubwa kwa taifa hili wakati wakiwa katika utumishi.

Wengi wa watumishi hawa waliitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa, kwa hiyo ni vyema taifa nalo kwa wakati wake likawakumbuka na hasa kuongeza kiwango chao cha pensheni.

Ikumbukwe kwamba wazee hawa wana mahitaji mengi na zaidi ya matibabu ya afya ambayo yanakula zaidi ya nusu ya kipato chao.

Kutokana na ukweli huo ni vyema kwa serikali kuangalia hoja iliyowasilishwa kwake na wastaafu hao na kuona uwezekano wa kuongeza pensheni hiyo.

Ili wastaafu hao waionje furaha ya utumishi uliotukuka ni vyema kwa serikali kuona namna bora kabisa ya kuwafanya waishi maisha ya furaha.

Aidha, kwa kuwa na maisha ya furaha watakuwa na cha kusimulia kwa watoto wao kuhusu utumishi usio na kifani uliowawezesha kuishi maisha ya kifahari wakati wa uzee kupitia fedha za serikali waliyoitumikia.

Watumishi hawa ambao ni sehemu ya jamii yetu kwa sasa hawawezi kufanya vitu vikubwa vya kutafuta maisha kama walivyokuwa wakifanya wakiwa vijana na wengi waliofanya kazi kwa uadilifu wamekuwa katika hali ngumu kidogo.

Pamoja na pensheni, kuna kila sababu serikali kuanza kufikiria makazi ya wazee au maeneo ambayo wastaafu wake wanaweza kuishi kwa kuanza kuwasaidia kupata makazi wakati wakiwa kwenye uwezo kwa kuweka mfumo bora na imara wa wao kutumia kupata makazi na pia kuendelea kujituma kwa vitu vidogo vidogo.

Watu hawa wanastahili kuwa watu wa mfano wanapoonekana wamepigika sana, vijana watasita kupeleka nguvu kazi zao katika utumishi wa umma kwa hofu kwamba nao watamaliza siku katika hali mbaya.

Ndio kusema pamoja na majukumu mengine, wataalamu wa serikali wa hifadhi wanastahili kukaa chini na kuona namna ya kuwaenzi wastaafu wetu, kwa mashiko makubwa kwani wao ni mfano si maua ya kupongeza kwa kutusaidia ambao ni muhimu katika uletaji ustawi wa watanzania.