22Mei2013

 

Mtindo huu wa kudai haki uangaliwe vema

IJUMAA iliyopita wafuasi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, walikwenda makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dar es Salaam kushinikiza Waislamu wenzao waliokamatwa kutokana na tuhuma za kuhujumu sensa waachiwe.

Baada ya mazungumzo na uongozi wa Wizara hiyo, ilikubalika kuwa watuhumiwa hao waachiwe, kitendo ambacho kilipokewa kwa mikono miwili na shangwe na wafuasi hao na kutangaza ushindi na kisha kupanga kuendelea na mtindo huo huo wa kudai haki katika taasisi zingine.

Kutokana na ‘ushindi’ huo, wanajumuiya na taasisi hizo, walipanga kwenda Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kumng’oa Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako na kisha kwenda makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kumng’oa Mufti Shaaban bin Simba.

Sababu zinazotolewa na wafuasi hao, ni kwamba Necta imekuwa ikionea wanafunzi wa Kiislamu na kuwafelisha katika mitihani yao, huku wakiishutumu Bakwata kuwa imekuwa kama chombo cha Serikali badala ya kuhudumia na kutetea Waislamu.

Sisi tunadhani dhana hizi hazipaswi kuendekezwa na kuchukuliwa kama njia halali za kudai haki na kuleta mabadiliko katika taasisi zinazosimamia maslahi ya wananchi, lakini pia zinazosimamia huduma ikiwamo elimu.

Tunaamini kwamba, kilichofanyika Mambo ya Ndani Ijumaa kilizingatia busara zaidi baada ya pande mbili kukutana na kufikia maafikiano hayo ya kuwaachia watuhumiwa wa uhujumu wa sensa na hivyo kuepusha mtafaruku ambao ungeweza kutokea.

Lakini kama hilo liliwezekana, basi isiwe tiketi ya kulazimisha kufanyika kwa jambo fulani na kutarajia kuwa Serikali itakuwa tayari kutii na kukubaliana na mashinikizo ambayo wakati mwingine hayana maslahi mema kwa wananchi.

Kwa kuwa zipo njia za kufuatwa katika kufikia makubaliano yenye maslahi kwa Watanzania walio wengi bila kujali itikadi au imani fulani ya kidini, ni dhahiri kwamba zikifuatwa hakutakuwa na sababu za kuingia katika mitafaruku ambayo tunajua ni hatari kwa mustakabali wa nchi.

Kama kweli Waislamu hawana imani na utendaji kazi wa mtu au watu ndani ya Necta na kama hawana imani na utendaji kazi wa Mufti, ni vema wakafuata njia nzuri isiyo na dalili zozote za kutaka kuvunja amani na bila shaka busara ile ile iliyotumika Ijumaa inaweza kutumiwa kama ikibidi.

Tanzania ni nchi isiyo na dini, bali wananchi wake ndio wenye dini na kila mtu ana haki na uhuru wa kuamini na kuabudu dini anayotaka ilimradi havunji sheria, hivyo kama kuna jambo linaonekana kuudhi baadhi ya watu basi njia mwafaka zifuatwe, kupitia uwakilishi na lizungumzwe na mwafaka upatikane.

Mathalani, Mufti amechaguliwa na Waislamu kuwaongoza kupitia Baraza lao Kuu, ni dhahiri kuna wanaomuunga mkono na kumwamini, lakini pia wapo kama hao ambao hawana imani naye na hawamuungi mkono, lakini hawezi kung’olewa kwa mabavu kama inavyopangwa leo.

Tunaamini kwamba Serikali na vyombo vyake wanaliona vuguvugu hili na hivyo wanapaswa kuwa makini na kusimama kidete kukabiliana nalo ili kuepusha uvunjifu wa amani unaoweza kujitokeza na kuliangamiza Taifa hili lenye sifa ya muda mrefu ya utulivu na amani.

Mataifa mengi yalishaingia katika migogoro iliyosababisha umwagikaji wa damu kutokana na matukio kama haya yanayohusisha imani za kidini, na kama Watanzania hatutakuwa makini na tukayashabikia, basi tusipoangalia tutajikuta katika matatizo makubwa.

Kwa wanaotaka Dk Ndalichako aondolewe Necta na Mufti Simba aondoke Bakwata, ni vema wakaelewa kuwa taratibu zipo na zinapaswa kuheshimiwa ili kulinda mustakabali mwema wa nchi yetu; tusikubali kamwe kuiweka nchi rehani kwa madai ambayo hayana maslahi kwa wengi.