Ajali za bodaboda zaweza kudhibitiwa
- Imeandikwa tarehe 14 Septemba 2012
- By Mhariri
- Imesomwa mara: 447
SERIKALI kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, imesema ajali nyingi za barabarani zinazosababisha vifo nchini, zinatokana na waendesha pikipiki zinazobeba abiria, maarufu kama bodaboda.
Kwa mujibu wa takwimu, kati ya Januari na Juni mwaka huu, zilitokea ajali 11,163 na kusababisha vifo vya watu 1,800 huku zaidi ya 9,000 wakijeruhiwa, ambapo asilimia 28 ya vifo hivyo, sawa na watu 504, ikiwa imetokana na ajali za pikipiki hizo.
Idadi hiyo ni kubwa na inachangia kupora nguvukazi ya nchi ambayo inategemewa kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa na hivyo kuhitajika hatua za makusudi za kuhakikisha ajali kama hizo zinapungua kama si kukoma kabisa.
Baada ya Serikali kuruhusu kwa nia njema biashara ya usafirishaji abiria kwa bodaboda, kwa lengo la vijana kujipatia kipato, ndivyo pia ajali zimeongezeka kwa sababu ya vijana wengi kutozingatia kanuni za usalama barabarani au baadhi yao kutozijua sheria.
Lakini pia yamekuwapo madai yanayothibitika, kwamba askari wa Usalama Barabarani wamekuwa wakilinda vijana hao ambao wanaendesha vyombo hivyo barabarani kana kwamba hawatakiwi kufuata sheria.
Si mara chache kuwakuta waendesha bodaboda wakiwa na vyombo hivyo bila kuvaa kofia za chuma ambazo huwasaidia kujikinga iwapo watapata ajali, lakini pia abiria wao ambao nao wamekuwa wakipanda pikipipiki hizo vichwa wazi.
Hata hivyo, hivi sasa licha ya Jeshi la Polisi kukataza ufungaji wa redio kwenye pikipiki ambazo hufunguliwa kwa sauti kubwa na hivyo kumfanya dereva ashindwe kuwa makini barabarani, hivi sasa watengenezaji pikipiki wamekuwa wakiziunganisha moja kwa moja na redio.
Hiyo inaonesha dhahiri kuwa hakuna ufuatiliaji wa dhati wa Jeshi la Polisi katika matamko yake, na ndiyo sababu waendesha bodaboda wanaendelea kupiga muziki kwa sauti kubwa na pengine kushindwa kuwa makini na hivyo kusababisha ajali.
Habari zingine ambazo zilithibitishwa na askari wa Usalama Barabarani ambaye hakuwa tayari kutaja jina kutokana na kutokuwa Msemaji wa Jeshi hilo, baadhi ya waendesha bodaboda wamekuwa wakipata barua za madaktari kuthibitisha kuwa wana mzio wa kofia hizo kwamba wakizivaa hupata matatizo ya ngozi.
Vyeti hivyo vimekuwa kikwazo kwa askari kuchukua hatua dhidi ya wakosaji, kutokana na kuheshimu taaluma ya tiba ambayo haiwezi kupuuzwa na askari kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo kwa asiyekubaliana nayo.
Jambo la msingi kuendelea kufanywa, ni kutoa elimu kwa waendesha bodaboda na watumiaji wengine wa barabara, juu ya kanuni na sheria zinazosimamia usalama barabarani, lakini pia kuhakiki vyeti hivyo vya madaktari, kwani uwezekano wa kughushiwa nao ni mkubwa.
Tabia ya waendesha bodaboda nayo inatakiwa kufuatiliwa kutokana na kuwapo tuhuma kuwa wengi wao wamekuwa wakipata kilevi kabla ya kuanza kazi zao za kusafirisha abiria na matokeo yake ni kuwa na ujasiri usio na uhalisia na hivyo kutamba barabarani na kusababisha ajali.
Ukaguzi wa leseni za madereva hao nao unapaswa kuzingatiwa kutokana na ukweli kuwa wapo ambao hununua pikipiki na kupanda hata kabla hawajajifunza vizuri na hata kujua sheria za barabarani zinazowaongoza katika uendeshaji.
Kama tutataka kupunguza au kumaliza ajali za barabarani, ni vema ukaguzi ukawa endelevu badala ya kusubiri Wiki ya Nenda kwa Usalama, ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka na kudumu kwa wiki moja na baada ya hapo mambo huendelea kama kawaida- sheria za usalama barabarani kukiukwa.


