Azam kamili kuivaa Simba

WACHEZAJI wa Azam FC wamesema mafunzo wanayopewa katika kambi yao ya Tanga yanatosha kuwamaliza wapinzani wao Simba Jumamosi wiki ijayo.

Kikosi cha Azam chini ya Kocha Stewart Hall, kinaendelea kujifua ambapo tayari kilicheza mchezo mmoja wa kirafiki juzi dhidi ya Mgambo na kulazimishwa sare na jana walitarajia kucheza na African Sports.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachezaji hao walisema wamefurahia kambi hiyo ya Tanga kwani wanapewa mafunzo mbalimbali namna ya kukabiliana na maadui zao. Miongoni mwa wachezaji hao ni Erasto Nyoni ambaye alisema:

“Mazingira ya kambi sisi tunayaona mazuri kabisa, tumefurahia sisi kuja kuweka kambi hapa na hata mafunzo tunayopewa ni mazuri”.

Naye beki wa kati kisiki Said Morad ‘Mweda’ alisema: “Kambi tunamshukuru Mungu mpaka sasa ipo salama hatuna majeruhi na mechi inayokuja dhidi ya Simba ni ngumu na sio nyepesi, inatakiwa kujitahidi na tukipata nafasi tuitumie.”

Kwa upande wake winga machachari, Khamis Mcha ‘Vialli’, alisema kambi yao ipo vizuri pamoja na mafunzo wanayopewa huko akidai kuwa wana uhakika wa kuifunga Simba na kumuomba Mungu awajaalie kwa hilo.

Vinara hao wa ligi wanatarajia kurudi leo Dar es Salaam kuendelea na kambi yao ya Chamazi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea katika mchezo huo utakaoamua hatima ya kuendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi.