Mbeya City yaitangazia ubaya Yanga

KIUNGO wa Mbeya City, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, ameionya Yanga ijiandae vya kutosha katika mchezo wao Mei 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Akihojiwa na tovuti ya Mbeya City jana, Redondo aliweka wazi kuwa ana imani kubwa na kikosi cha sasa cha timu yake, hasa baada ya ujio wa kocha Kinnah Phiri aliyefanikiwa kuyaondosha ‘makandokando’ yote yaliyosababisha timu kufanya vibaya kwenye michezo iliyopita.

Tangu alipojumuishwa kwenye kikosi cha City, Redondo, amecheza mechi 8 na kufunga mabao mawili. “Yanga wanatakiwa wajiandae vizuri kwa kuwa wanakuja kukutana na kikosi cha City ambacho kiko kwenye wakati mzuri hivi sasa, wasitegemee mteremko kwani ujio wa kocha Phiri umeiimarisha zaidi timu yetu,” alisema.

Alisema Phiri amewapa mwongozo mzuri na amefanya kazi kubwa kuweka timu sawa, hivyo Yanga wajue watakutana na upinzani mkali, tofauti na ilivyokuwa inacheza hapo mwanzo.

Redondo, aliyewahi kucheza timu za Ashanti, Simba na Azam FC, alisema anafahamu mchezo huo utakuwa mgumu pande zote kwa sababu kila timu inahitaji matokeo kulingana na hali ilivyo kwenye msimamo, Yanga ikitaka kujihakikishia ubingwa na City ikihitaji kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Kuhusu majaliwa yake kwenye kikosi cha City, Redondo alisema kuwa ana imani kubwa atakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao, na kuweka wazi furaha yake ya kuwa mchezaji wa timu hiyo.