Kila kipande cha ardhi nchini kupimwa kumaliza migogoro

SERIKALI imesema iwapo mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya tatu za Morogoro ukipata mafanikio ya kila kipande cha ardhi kupimwa, itaanzisha mpango wa namna hiyo katika vijiji vyote nchini kumaliza migogoro ya ardhi.

Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa John Lupala, alisema jana kuwa mpango huo utakuwa wa miaka 10 kwa kuwa hadi sasa kati ya vijiji 12,00 vilivyoko Tanzania Bara, vijiji 1,640 pekee vina mpango wa matumizi bora ya ardhi.

“Tuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika mpango huu, ndio maana tunataka tufanye kwa uwazi na migogoro iliyopo hapa isemwe kwa uwazi ili tukifanikiwa, ikiwezekana baadaye tulipeleke katika maeneo mengine hapa nchini,” alisema Profesa Lupala.

Alisema, lengo ni kutaka ardhi iwe rasilimali inayowafaidisha wananchi hasa wakulima na kutekeleza azma hiyo ni kuongeza kasi ya kupanua matumizi ya ardhi katika maeneo yote nchini.

Alikiri kuwa jambo hilo ni gumu na linahitaji kushirikisha sekta binafsi pamoja na tume ya matumizi ya ardhi kupima vijiji na miji ili wananchi wapatiwe hati miliki ambazo zitawasaidia katika kuboresha uchumi wao.

Alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa wadau wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya ya Malinyi mkoani hapa. Mkutano huo uliandaliwa na Mpango wa Kuwezesha Kumiliki Ardhi (LTSP), ambao unatekelezwa katika wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero.