SERIKALI mkoani Rukwa imeamuru wavuvi haramu 28 kutoka Zambia waliokamatwa na kikosi cha doria kinacholinda mwambao wa Ziwa Tanganyika katika Kijiji cha Kasanga wilayani Kalambo, wakivua samaki upande wa Tanzania kinyume cha sheria wasifunguliwe mashitaka, bali warejeshwe nchini mwao.
Wavuvi hao walikamatwa hivi karibuni, saa 11 alfajiri katika kijiji cha uvuvi cha Kilewani kilichopo katika mwambao huo wakiwa na boti mbili, nyavu na kilo 520 za samaki.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema licha watuhumiwa hao wote kusafirishwa hadi mjini hapa na Mwanasheria wa Serikali kuanza kuandaa hati ya mashitaka ili wafikishwe mahakamani, uongozi wa juu mkoani hapa umefikia maamuzi wa kuwarejesha Zambia walikotoka.
Awali, wavuvi hao walishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Kasanga, mwambao mwa Ziwa Tanganyika kisha wakahamishwa Matai wilayani Kalambo, kabla ya kusafirishwa hadi mjini hapa ili kufikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, maamuzi hayo yalifikiwa kwa kuwa wakazi wa Rukwa na wale wa Zambia wanaishi vizuri bila chokochoko zozote zile, hivyo ilionekana ni busara kutowafungulia mashitaka badala yake wameamriwa kurejeshwa makwao na kupewa onyo la kutovuka mipaka na kuvua katika eneo la Tanzania kinyume cha sheria. “Busara imetumika.
Ni suala la ujirani mwema kwani wananchi wetu wanaishi vizuri na wenzao wa nchi jirani ya Zambia. Isitoshe mara baada ya kukamatwa kwa wavuvi hao upande wa Zambia walianza chokochoko wakiwabughudhi Watanzania walioko huko au waliokuwa wakiingia katika nchi hiyo ya jirani,” alisema Kamanda.
Pia aliongeza kuwa zaidi ya kilo 500 walizokutwa nazo wavuvi hao siku hiyo, zimetaifishwa na kuuzwa katika mnada wa wazi. Pia alisema wavuvi hao walisindikizwa hadi kijijini Kasanga na kukabidhiwa kwa wenye maboti waliowasafirisha ambao walioamriwa kuhakikisha wanawarejesha walikotoka kwa gharama zao wenyewe.
Vyanzo vya uhakika vya habari kutoka vijiji vya mwambao huo, vinaeleza kuwepo makundi ya wavuvi kutoka Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi wamekuwa wakiingia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na kuvua bila kibali.
Baadhi ya wakazi wa vijiji kadhaa vya mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi na Kalambo wamekiri kuwa wavuvi hao haramu huhifadhiwa na baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyopo katika mwambao wa ziwa hilo na baadaye hujitokeza hadharani na kujitambulisha kuwa ni raia wa Tanzania.
Baada ya kujitambulisha kama Watanzania, wavuvi hao huanza kujishughulisha na uvuvi na kusafirisha samaki hao ambao huwauza nchini mwao.