KWA takribani siku nzima ya jana, mji wa Mtwara jana uligubikwa na vurugu zilizosababisha jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu ili kurejesha hali ya amani.
Hadi kufikia majira ya saa 12:30 jioni vurugu zilikuwa zinaendelea huku wananchi wakifanya uharibifu wa mali, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto Mahakama ya Mwanzo na pia kuvunja vioo vya nyumba inayodaiwa kuwa ya Hawa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Nyumba nyingine iliyoshambuliwa na kuharibiwa katika Mtaa wa Sinani mjini hapa ni ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Mohammed Sinani, huku gari la polisi likivunjwa vioo na pia mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, John Kasembe akijeruhiwa.
Ingawa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki hakupatikana kuzungumzia sakata hilo licha ya kutafutwa kupitia simu zake mbili za mkononi na pia kufuatwa ofisini kwake, baadhi ya maofisa wake, ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa majina, wamethibitisha kutokea kwa vurugu hizo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia shughuli zikisimama kutwa nzima ya jana huku makundi ya vijana yakifanya vurugu na kujaribu kuwazingira askari, licha ya kupigwa mabomu ya machozi.
Katika mitaa kadhaa ikiwa ya Kata ya Chikongola, polisi walikuwa na kazi ya kuondoa matairi ya magari yaliyokuwa yanachomwa moto, kuondoa magogo makubwa na mawe barabarani.
Chanzo cha vurugu hizo kimeelezwa na harakati za polisi za kuwatawanya wananchi walioizingira nyumba ya Diwani wa Kata hiyo, Mohammed Chehako, wakidai kuwa, ndani ya nyumba hiyo walihifadhiwa watu waliodhaniwa kuwa ni wachawi.
Wananchi walitoa tuhuma hizo baada ya kukuta karibu na nyumba ya diwani ungo ukiwa na ‘matunguli’ ndani yake, hivyo kumlazimisha awatoe nje ili waadhibiwe.
Diwani huyo alipinga kuwa hakuna watu wa aina hiyo huku akiwataka waondoke baada ya kuwa amevichoma moto vitu hivyo.
Baadaye polisi waliingilia kati na ndipo vurugu ziliposhamiri na kusambaa katika kila kona ya mji, wengi wakidandia wakiamini polisi walipambana na wananchi wanaopingana na Serikali juu ya suala la gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.
Akihadithia mkasa huo, Chehako alisema alipoamka alfajiri kwa ajili ya kwenda msikitini alishangaa kusikia sauti za watu nje ya nyumba yake na alipotoka alikuta ungo na `tunguli’ , lakini ghafla walikuja vijana wawili waliokuwa na pikipiki, wakaukwapua ungo na kuondoka nao, baadaye inadaiwa ulirushwa na kuteketezwa.