Wanasiasa, Wanakagera msikilizeni Rais kuhusu maafa

MWEZI Septemba mwaka jana, mikoa inayozunguka maeneo ya Kanda ya Ziwa, ukiwemo mkoa wa Kagera yalikabiliwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililokadiriwa kuwa na ukubwa wa kipimo cha Ritcher 5.9 na kusababisha vifo vya watu 17, majeruhi 560 na uharibifu wa miundombinu zikiwemo barabara, shule na hospitali.

Baada ya tukio hilo, serikali, nchi wahisani na wadau mbalimbali waliungana kwa pamoja na kuanza kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo vyakula, dawa na malazi ya muda, nguo, tiba, vifaa vya shule pamoja na huduma ya ushauri wa kisaikolojia kwa waathirika, hatua iliyolenga kuwapa pole waathirika wa tukio hilo.

Kutokana na tukio hilo, Serikali kupitia Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu ilituma wataalamu kufanya tathmini ya athari za tetemeko ambapo makadirio ya awali yaliainisha kuwa takribani kiasi cha jumla ya Sh bilioni 104.9 zilihitajika katika kurejesha eneo hilo katika hali ya kawaida baada ya maafa hayo.

Hata hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa walifanya tathimini ya pamoja ya mahitaji ya haraka ya athari za tetemeko hilo ili kubaini maeneo zaidi yaliyoathirika.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alifanya ziara ya siku mbili mkoani Kagera kuwatembelea wananchi walioathiriwa na tetemeko hilo na kukagua baadhi ya miundombinu iliyoathiriwa pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule za sekondari ya Ihungo na Omumwani zilizobomolewa na tetemeko hilo.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliwaeleza waathirika hali halisi ya jukumu la Serikali katika kusaidia waathirika wa majanga tofauti yanayoweza kutokea nchini.

Licha ya wananchi kuonekana kupokea hotuba ya Rais Magufuli kwa hisia tofauti, ni dhahiri ameendelea kuonesha jinsi alivyo mkweli katika kila jambo ambalo serikali inafanya. Rais Magufuli alisema jukumu la serikali ni kurudisha miundombinu ya taasisi za umma zikiwemo hospitali, shule na barabara.

“Lazima niwaeleze ukweli, kwa kuwa msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, mvua zimenyesha watu tufanye kazi, serikali tusimamie yale mahitaji muhimu kwa watanzania, tutengeneze reli, tujenge hospitali, tulete umeme, kuhakikisha huduma ya maji inapatikana na kuendelea kufanya maboresho katika sekta ya elimu,” alisema Rais Magufuli.

Kwa kauli hiyo, serikali ilipaswa kulaumiwa kama ingeshindwa kurudisha miundombinu ambayo inawahudumia wananchi mfano kuharibika kwa shule ya sekondari Ihungo ambayo inahudumia idadi kubwa ya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wa hospitali na vituo vya afya, vingi viliathiriwa na juhudi za serikali katika kuvirudisha katika hali ya kawaida kuwezesha wananchi kuendelea kupata huduma hiyo muhimu katika maeneo hayo.

Rai yangu kwa wanasiasa na wananchi wa Kagera ni kuchambua hotuba ya Rais kwa mtazamo chanya, kwani jukumu la serikali ni kuboresha miundombinu inayohudumia wananchi kwa pamoja na si kujenga nyumba kwa kila mmoja aliyeathirika na janga hilo.

Katika wakati mgumu kama huu, tunapaswa sote kujifuta machozi ya kuondokewa na wapendwa wetu na kuathirika kwetu kwa kuyatafakari maafa hayo kwa akili zetu na sio kwa hisia zetu.

Kwa makusudi, tunatakiwa tujiepushe kuyakumbushia na kuyashadidia yale yaliyotokea, maana kufanya hivyo hakutasaidia bali kutaushindilia msumari wa moto juu ya kidonda kibichi.

Busara ya kiutu inatuelekeza kuwa huu si wakati wa kuulizana vipi maafa haya yalitokea, swali kama hili si mwafaka kwa wakati kama huu, maana jibu lake linatupeleka kutafuta nani alifanya nini, na kwa staili gani.

Changamoto tuliyonayo hapa ni kuendelea kushikamana katika kukabiliana na janga hili tukiwa wamoja hadi hapo wenzetu walioguswa moja kwa moja nalo warejee katika hali yao ya maisha ya kawaida kama walivyokuwa hapo awali.