Wazazi, walimu shawishini wanafunzi kupenda Hisa

UFAULU kwa somo la Hisabati katika mitihani ya taifa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita umekuwa chini kutokana na asilimia 20 pekee ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kufaulu somo hilo.

Kutokana na tatizo hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema juzi kuwa endapo tunataka ufaulu kwa somo la hisabati uongezeke, itabidi tukubali kubadili fikra za wanafunzi wanaochukia somo hilo, pamoja na ya sayansi kwa imani kuwa ni magumu.

Kwa kuzingatia alichosema Profesa Ndalichako, kuna haja ya kuwajengea uwezo wanafunzi kuanzia ngazi ya awali kuwa wanaweza kufanya vyema katika masomo ya sayansi na hisabati, ili wayapende na kuongeza bidii ya kujifunza kama wafanyavyo kwenye masomo mengine.

Kazi ya kufundisha pamoja na kuongoza watoto katika masomo si ya walimu pekee, bali ni ya wazazi na walezi wenye wajibu wa kushirikiana na walimu kuwaondoa hofu kuhusu ugumu unaodaiwa kuwepo katika masomo hayo.

Kama wazazi au walezi tuna wajibu kama walionao walimu wa kuwashawishi wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na hisabati, hasa kwa kuwapa majaribio na mazoezi ya masomo hayo mara kwa mara, bila kuwakatisha tamaa pindi wanapokosea majibu.

Lakini endapo tutakuwa pamoja na watoto wetu na kuwasahihisha wanapokosea huku tukiwaonesha namna rahisi ya kukokotoa hesabu wanazopewa ili kuzitafutia majawabu, ninaamini hawataliona somo hilo kuwa gumu, bali watakuwa na moyo wa kujibidiisha zaidi na kudadisi njia sahihi za kupata majawabu yaliyo sawa.

Hali kadhalika kwa walimu watafute njia nzuri za kuwafanya watoto wafurahie masomo hayo, hivyo kuwajengea mazingira mazuri yatakayowafanya wayaone kuwa rafiki na si masomo ya kuyakimbia. Ikiwa mwalimu ni mkali sana, mwalimu ambaye anatoa adhabu kali kila mwanafunzi anapokosea hii itamfanya mtoto kuchukia somo pamoja na mwalimu husika.

Tunaambiwa samaki mkunje angali mbichi, tuwajengee mapema uwezo na upendo katika masomo na hasa ya hesabu na sayansi, jambo litakalosaidia kuwaondolea wanafunzi dhana kwamba masomo hayo ni magumu. Somo la hisabati si gumu kama inavyofikiriwa na watu wengi ikiwa wanafunzi watashawishiwa kulipenda kuanzia katika ngazi za chini.

Ni somo linalohitaji kujituma kwa mwanafunzi na kutolewa kwa mazoezi ya mifano ya mara kwa mara na walimu au watu wengine wanaolimudu vilivyo. Ili wanafunzi wapende somo lolote si tu hisabati ni lazima wajengewe mazingira mazuri yatakayosaidia wapende somo husika, ikiwemo kuwa na vitabu vya kutosha pamoja na watu walio tayari kuwaongoza kuhusu somo husika kwa mifano na majaribio ya kila mara.

Nakumbuka kuna wakati tulikuwa na walimu wa kujitolea mitaani ambao walikuwa wakikusanya wanafunzi na kuwafundisha hasa waliokuwa wakijiandaa kuingia kidato cha kwanza. Binafsi niliona kuwa walimu hawa walikuwa wakisaidia ingawa kwa sasa naona kama utaratibu huu haupo.

Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, kwa upande wa Wizara, Serikali imekuwa na mikakati kadhaa kuhakikisha tatizo la kutoongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika masoko ya sayansi na hisabati linapatiwa ufumbuzi, ambapo miongoni mwa mambo iliyoyafanya ni pamoja na kuandaa Sera ya Elimu ya mwaka 2014.

Sambamba na hilo, Serikali imeboresha ufundishaji wa somo la hisabati, pamoja na masomo ya sayansi katika ngazi zote za elimu na kuhakikisha kuwa masomo hayo yanapewa kipaumbele.