23Mei2013

 

Ugonjwa mpya wa mahindi ni janga

WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika imetoa taarifa kuhusu ugonjwa mpya wa mahindi. Unajulikana kama Maize Lethal Necrotic (MLND).

Ugonjwa huo unaosababishwa na virusi wajulikanao kama Maize Chlorotic Mottle (MCMV) na Sugarcane Mosaic (SCMV), umeanzia Kenya.

Taarifa ya Wizara ya hivi karibuni, inaonesha kwamba katika eneo hilo la Kenya ambako ugonjwa ulianzia, ulisababisha asilimia 100 ya uharibifu kwa mahindi yaliyopo shambani.

Hadi sasa ugonjwa umesambaa katika eneo kubwa ndani ya Bonde la Ufa na umeenea katika wilaya 22 nchini humo. Hasara kutokana na ugonjwa huo inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 na 90. Hili ni janga kubwa.

Panahitajika juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa hauingii nchini. Hili ni zao muhimu sana kwa maisha ya asilimia kubwa ya Watanzania wanaolitegemea kwa mlo na matumizi mengine.

Ugonjwa ukishagusa zao la chakula, lazima pawepo mtikisiko mkubwa kwa ustawi wa jamii. Wakazi wa mkoani Kagera wana ushuhuda wa hali hiyo kutokana na migomba kushambuliwa na ugonjwa mnyauko.

Wakazi wa mkoa huo ambao hutegemea ndizi kama chakula kikuu, hivi sasa wanahaha si tu kwa kula chakula ambacho hawakukizoea, bali pia kiuchumi kutokana na kulazimika kutafuta fedha za kuhemea vyakula vingine kama vile unga na mchele.

Katika maeneo mbalimbali hususan wilaya za Muleba na Bukoba Vijijini, wananchi wamekaririwa wakilia na umasikini bila kufahamu hatma ya maisha yao. Serikali hususan wataalamu wa kilimo, haipaswi kukaa kimya juu ya hali hii.

Laiti kama wataalamu wangebaini ugonjwa huo wa migomba mapema na kutoa hadhari, yawezekana hali isingefikia kama ilivyo sasa.

Sasa inapojitokeza pia kwenye mahindi, Serikali inapaswa kuendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha hauingii nchini, vinginevyo litakuwa janga la kitaifa.

Inawezekana suala hili likachukuliwa kwa wepesi na baadhi ya watu. Lakini kwa wanaotambua nafasi ya mahindi katika maisha ya kila siku hasa kwa kuzingatia kwamba ugali ndicho chakula kinachotegemewa na Watanzania walio wengi, hawatachukulia mzaha. Inasemekana ugonjwa unaenezwa kwa mbegu.

Wizara inakiri, kwamba Tanzania inaagiza kiasi kikubwa cha mbegu kutoka nje ya nchi. Serikali inatambua hilo na imeuhakikishia umma, kwamba itahakikisha vibali vyote vinavyotolewa, mbegu husika zihakikiwe kuwa hazina vimelea.

Imesema sampuli zitachukuliwa na kupelekwa kituo cha karantini kwa ajili ya uhakiki. Lakini pia halmashauri za wilaya kwa kushirikiana na wizara, zitatoa elimu ya jinsi ya kutambua ugonjwa huo na mbinu za kuukabili. Haya yanayosemwa na wizara hayana budi kutekelezwa kwa vitendo.

Mamlaka zenye jukumu la kuidhinisha uingizaji wa mbegu lazima ziwajibike na ziwe na uzalendo kuhakikisha ugonjwa huu hauingii ndani.

Linapokuja suala la uelimishaji, wizara ilisimamie ipasavyo kuhakikisha kila mkulima anapata taarifa juu ya janga hilo. Pamoja na vyombo vya habari kutumika, ni wakati wa maofisa kilimo kwenda kwa wakulima kuwapa taarifa ili wachukue hadhari.

Wizara imefanya vyema kutoa taarifa hiyo; lakini haitoshi kuishia katika taarifa hiyo ya siku moja kwenye vyombo vya habari. Inapaswa iendelee kuelimisha wananchi wa mipakani na wasio juu ya hatari ya ugonjwa huu.

Kampeni ya kitaifa ifanyike kwa upana kuhakikisha kuwa umma unaelimishwa juu ya kujihadhari na matumizi holela ya mbegu; vinginevyo, kuruhusu ugonjwa huu kuingia nchini ni kuruhusu janga la kitaifa.