22Mei2013

 

Usafiri wa treni mkombozi kwa wakazi wa Dar es Salaam

MOJA ya kero kubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni pamoja na usafiri wa kutoka na kuelekea sehemu za kazi, hususan nyakati za asubuhi na jioni wakati wa kurejea majumbani.

Mbali ya shida ya usafiri kumekuwa na foleni ndefu kiasi ambacho hulazimu wafanyakazi kutoka majumbani mwao alfajiri sana ili kukwepa foleni na kupata usafiri kirahisi.

Mbali ya wafanyakazi wengine wanaopata shida kubwa ya usafiri ni wanafunzi ambao hunyanyaswa na makondakta kiasi ambacho hufika shuleni wakiwa wamechoka sana huku wamechelewa na kukosa hamu ya kusoma.

Juzi wakazi wa jiji hili walipatwa na mshangao bila kuamini, wakishuhudia kwa mara ya kwanza treni lenye mabehewa sita likifanya majaribio ya kuanza usafiri jijini, jambo ambalo ni ukombozi wa kweli kwa wananchi.

Wakati wa majaribio hayo ambayo pia Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alihudhuria, baadaye aliwahakikishia wakazi wa mkoa huu kuanza rasmi kwa usafiri huo mwezi ujao.

Alisema majaribio hayo yalifanyika baada ya maandalizi ya awali kukamilika lengo ni kuondoa msongamano wa magari mjini.

Usafiri huo utasaidia wasafiri wanaotoka maeneo ya Stesheni kuelekea Ubungo na maeneo mengine kama Tabata, Buguruni, Ilala na kwingineko kuwa na uhakika wa usafiri na hivyo kupunguza msongamano barabarani.

Alisema usafiri huo utaanza baada ya kutathmini bajeti nzima ya uendeshaji wake na kujua nauli kwa wateja ambao watautumia, huku akisisitiza kuwa yanahitajika marekebisho katika reli hiyo.

Alisema usafiri huo utakuwa ukibeba abiria 900 kwa mabehewa mawili ambapo treni hilo litafanya safari mara tatu asubuhi na jioni.

Napenda kupongeza Wizara ya Uchukuzi kwa juhudi ilizoonesha katika kuhakikisha miundombinu iliyopo inatumika kurahisisha maendeleo kwa wananchi kwa kuwa na usafiri wa uhakika.

Pia ninawapongeza kwa kukamilisha ahadi hii kwa muda mfupi tangu Waziri Dk Harrison Mwakyembe ateuliwe kushika nafasi hiyo na kutoa ahadi ya usafiri wa wakazi wake kutumia usafiri huo jijini na kuanza kuona vitendo na si maneno pekee.

Kama alivyosema Naibu Waziri kwa muda uliobaki ni vema wizara ikahakikisha usafiri huo unapoanza unakuwa wa uhakika na si ‘nguvu ya soda’, kwa kuanza muda mfupi na kuacha.

Lakini pia ihakikishe usafiri huo unakuwa salama kwa kukagua miundombinu yake na kuiweka katika hali nzuri, ikiwa ni pamoja na kupanga nauli ambayo kila mwananchi ataimudu.

Naamini iwapo usafiri huu utasimamiwa vizuri, utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji abiria, lakini pia utasaidia kuwaondolea kero ya usafiri wananchi na wanafunzi wanaotumia huduma hiyo Dar es Salaam.

Mwito wangu kwa wizara husika ni kuhakikisha hatua hii inadumu na kuongezeka, kwani ni ukombozi mkubwa hasa kutokana na adha ya usafiri ambayo imekuwa changamoto kubwa katika harakati za maendeleo na ujenzi wa Taifa.