Kili Stars kazi bado Chalenji

TIMU ya Kilimanjaro Stars leo inashuka dimbani kucheza na wenyeji Ethiopia katika mchezo wa kukamilisha ratiba, baada ya timu hiyo kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Kilimanjaro Stars na Ethiopia zinakutana katika mchezo utakaofanyika Awassa, ambapo ushindi ni muhimu licha ya timu hiyo kuwa tayari ilishafuzu kwa robo fainali. Timu hiyo kabla ya kukata tiketi ya kucheza hatua hiyo inayoshirikisha timu nane bora, ilizifunga Rwanda na Somali na sasa inahitaji ushindi dhidi ya Ethiopia ili iweze kumaliza ikiwa kileleni.

Kwa mara ya mwisho Tanzania Bara ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2010 ikiwa chini ya kocha Jan Poulsen baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 Kabla ya kutwaa taji hilo, Kilimanjaro Stars ilitwaa tena mwaka 1994 chini ya kocha Sylersaid Mziray, ambaye kwa sasa ni marehemu akisaidiwa na Sunday Kayuni.

Kabla ya hapo, timu hiyo kwa mara ya kwanza ilitwaa taji hilo mwaka 1974. Mwaka huu timu hiyo inafundishwa na Abdallah Kibadeni na ni miaka minne tangu ilipotwaa taji kwa mara ya mwisho, hivyo, wadau wa soka wana kiu na ubingwa huo.

Ni matarajio ya wadau wa soka na wanamichezo kwa ujumla kuwa, wachezaji na benchi zima la Kilimanjaro Stars limejipanga vizuri, ambali na kumaliza hatua ya makundi kwa ushindi, pia watarudi na taji hilo.

Timu hiyo inatakiwa kupambana kweli kweli kuhakikisha kila anayekuja mbele yake anapokea kichapo na Kilimanjaro Stars ina songa mbele hadi fainali na kutwaa ubigwa huo. Wachezaji wengi wa timu hiyo walikuwa pamoja kwa muda mrefu, hivyo maandalizi yao ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na zile za Mataifa ya Afrika, zitawasaidia kufanya vizuri.

Baada ya kutolewa kwa Zanzibar, Watanzania wote macho na masikio yao wameyaelekeza kwa Kilimanjaro Stars, hivyo wachezaji wake wasiwaangushe wapenzi wa soka. Kila la heri Kilimanjaro Stars na mnachotakiwa kushinda kila mchezo ulio mbele yenu ili kulitwaa taji hilo, lakini mjue kuwa kazi iliyo mbele yenu ni kubwa.