Mgawo wa Ngao ya Jamii kwa jamii hautoshi
- Imeandikwa tarehe 15 Septemba 2012
- By Joseph Kulangwa
- Imesomwa mara: 375
JUMANNE iliyopita, mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania, Simba na walioshika nafasi ya pili msimu uliopita, Azam, walichuana katika kuwania Ngao ya Jamii ambapo Simba iliibuka mshindi na kutwaa Ngao hiyo baada ya kuibamiza Azam magoli 3-2 katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Lengo la mechi hiyo kama inavyofahamika mbali na kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu kwa msimu wa mwaka 2012/13 inayotarajiwa kuanza leo, ni kutoa msaada kwa jamii; na safari hii jamii ambayo inasaidiwa kutokana na mapato ni hospitali ya wilaya ya Temeke.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, jumla ya fedha zilizopatikana katika mechi hiyo ni Sh milioni 146.6 kutokana na mashabiki 26,001 waliokata tiketi na kwamba kati ya fedha hizo, hospitali ya Temeke imetengewa Sh milioni 7.3 baada ya mgawanyo.
Kiasi hicho ni asilimia tano ya mapato. Wambura alisema fedha hizo zitatumika kununulia vifaa kwa ajili ya hospitali hiyo baada ya kufanyika mawasiliano na uongozi wa hospitali kuorodhesha vifaa vinavyotakiwa.
Ni wazo jema kuisaidia hospitali hiyo ambayo kama zilivyo hospitali zingine nchini inakabiliwa na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na upungufu wa vifaa vya tiba, lakini pia vinavyotumika kwa ajili ya huduma za wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa maelezo ya TFF, hospitali ya Temeke ilichaguliwa kunufaika na mapato hayo kwa kuzingatia kuwa Temeke ni wilaya ambayo imekuwa mwenyeji wa michuano hiyo inayofanyika katika Uwanja wa Taifa na ule wa Azam ulioko Chamazi.
Mgawanyo wa fedha hizo, hata hivyo unasababisha dhana nzima ya kuwa mapato hayo ni kwa ajili ya jamii, kupotea na hata jina la Ngao ya Jamii kupoteza maana, kwa sababu haiwezekani jamii ikatengewa asilimia tano tu wakati jambo hilo hufanyika mara moja kwa mwaka.
Ingekuwa busara kama jamii ingepewa sehemu kubwa ya mapato hayo kuliko hata TFF ambayo katika mgawo huo mathalan, imetengewa Sh milioni 10.
Hakika mlolongo wa mgawanyo wa mapato hayo unaacha maswali mengi na kuondoa kabisa maana ya Ngao ya Jamii.
Mimi nilidhani kwa kuwa Ngao hii hutolewa mara moja kwa mwaka, ingewezekana kabisa wote walio katika mgawanyo huo wakasamehe mapato hayo na kupelekwa kwa jamii, ili angalau uwepo uzito wa Ngao yenyewe badala ya kutolewa kiwango hicho kidogo cha fedha kisichokidhi mahitaji hata kwa asilimia tano.
Kama ilivyozoeleka, tunajua kuwa katika michuano kama hii kila mdau anaangalia atapata nini na hivyo kupoteza ukweli kuwa kinachoangaliwa ni kutoa shukurani kwa jamii ambayo kwa kiasi fulani nayo imekuwa ikichangia katika ustawi wa mchezo huu.
Kwa kuwa mechi za Ligi Kuu ni nyingi, sioni sababu ya watu wote hao kunyang’anyana ‘kisungura’ hicho kidogo badala ya kuacha kisaidie wagonjwa ambao wanateseka vitandani katika hospitali ya Temeke na zingine nchini.
Kuna wahusika kama vile Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ambao nao wamepewa Sh milioni 5, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Sh milioni moja, Wachina Sh milioni mbili, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),Sh milioni nne, na wengineo.
Hawa katika hili sioni kama walikuwa na ulazima wa kupata mgawo. Lakini hata kama tunaona ni muhimu nao kupata mgawo huo, basi siku zingine tuhakikishe ili kweli Ngao hii inakuwa ya jamii, basi kiwango kiongezwe hata kufikia asilimia 50 au 75 ili hata kazi itakayokuwa inafanywa na fedha hizo ionekane, kwani Sh milioni 7 kwa hospitali kama ile ni fedha kidogo sana.
Najua mkono mtupu haulambwi, hivyo uongozi wa hospitali ya Temeke utashukuru kwa hicho kidogo itakachopewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, lakini bado haja ya kuboresha mapato hayo kwa jamii itaendelea kuwapo.
Tunauomba pia uongozi wa Hospitali hiyo ya Temeke uhakikishe mahitaji unayoyatoa yapo kweli na ni ya msingi kwa ajili ya uendeshaji wa hospitali hiyo na TFF ifuatilie kuona kuwa kilichoombewa ni halisi na kinafanyiwa kazi kusudiwa.
Nawaomba pia TFF waichukue hii kama changamoto kwa Ngao hiyo badala ya kufikiria tu kuziba ‘mashimo’ katika Shirikisho na kupoteza umaana na umuhimu wa mchuano huo ambao ni fursa pekee kwa jamii kunufaika na michuano ya Ligi Kuu nchini.


