19Mei2013

 

Mtihani darasa la saba usigubikwe na udanganyifu

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa onyo kali kwa watakaojaribu kufanya udanganyifu au waliozoea kufanya vitendo vya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu kutothubutu kufanya hivyo.

Onyo hilo limekuja wakati mwafaka, kwani kesho jumla ya watahiniwa 894,881 wanatarajia kuanza mtihani wao wa kumaliza elimu ya msingi wakiwa na matumaini ya kufanya vizuri na kuvuka salama kipimo hicho ambacho kitatoa tathmini ya kile ambacho wamekuwa wakikifanya kwa kipindi cha miaka saba.

Kimsingi ninaunga mkono onyo hilo, lakini naomba katika suala hilo tusiishie kutoa onyo, bali jambo hilo litekelezwe kwa vitendo ili kuokoa elimu ya Tanzania ambayo inaporomoka kutokana na vitendo vya watu wasio waadilifu na uchungu na Taifa hili ambao hufanya udanganyifu katika mtihani hivyo kuzalisha wasomi feki wasiojua kusoma wala kuandika.

Kutokana na adha hii, inabidi Serikali ilivalie njuga kikamilifu suala hili la udanganyifu katika mitihani hasa ya shule za msingi, kwani hatua hiyo ndio muhimu katika kujenga wasomi wa baadaye kutokana na ukweli kuwa ubora wa elimu unategemea ubora wa elimu ya msingi ulivyo; kinyume chake ni kuwa taifa la ‘vihiyo’ ambao watalidumaza kimaendeleo.

Taifa kama Tanzania ambalo lilipata uhuru mwaka 1961, hivi sasa imepita miaka 50 tangu Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere atangaze vita dhidi ya maadui wakuu watatu; ujinga , umasikini na maradhi , lakini kutokana na hali ilivyo inaonekana vita hii inataka kutushinda.

Ni aibu kwetu baada ya miaka yote hiyo bado tunazalisha wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika , wakati vita dhidi ya ujinga ilianza miaka 50 iliyopita na hili linatokana na mmomonyoko wa maadili na rushwa miongoni mwetu , ambavyo vimesababisha kudorora kwa vita hivyo dhidi ya ujinga na kusababisha tufike hapa tulipo sasa.

Ni jambo la kushangaza lakini ndio ukweli wenyewe tuna wanafunzi ambao hawajui kusoma wala kuandika, lakini ndio hao hao wanaoweza kufanya mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi na kufaulu, huku wakiwa hawajui kuandika wala kusoma.

Na hii ni dhahiri kuwa kuna udanganyifu mkubwa ambao unahusisha si wanafunzi peke yao au walimu na wasimamizi bali hata wazazi na askari ambao hupewa majukumu ya kulinda mitihani na watihaniwa wakati wa mitihani.

Kwa hiyo, Serikali ina wajibu si tu kubana watihaniwa na wasimamizi peke yao, bali hata watu wengi ambao watabainika kuhusika na udanganyifu wa aina yoyote ile, katika mitihani mbalimbali ya kitaifa ili kuhakisha harakati za kuirejesha elimu ya Tanzania katika ubora wake iliyokuwa nao katika miaka iliyopita zinafanikiwa.

Na jambo hili litafanikiwa endapo adhabu ambazo zimebainishwa na Serikali kuwa zitatolewa kwa wahusika wa udanganyifu zitatekelezwa kweli bila kujali nani ni mhusika badala ya kubaki kuwa maneno matupu ili iwe mfano kwa wengi wasijaribu kufanya vitendo kama hivyo katika siku zijazo.