Rage awang’ang’ania Simba fedha za Okwi

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Ismail Rage, amezidi kuwabana viongozi wa Simba na kusema hawapaswi kuendelea kunyamaza kuhusiana na fedha za mauzo ya mshambuliaji Emmanuel Okwi badala yake waweke wazi.

Akizungumza na gazeti hili, Rage alisema kuwa fedha hizo pamoja na za mshambuliaji Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji zina uwezo wa kujenga uwanja wa Bunju, kuweka nyasi na majukwaa, lakini ukimya wa viongozi wa Simba kuhusu jambo hilo unamtisha.

“Nimeamua kuzikomalia kwa vile nilishutumiwa sana wakati wa uongozi wangu kuwa nilikula zile fedha. Lakini nashukuru fedha zimeletwa na waliokuwa wananituhumu baadhi yao ndiyo hao wameamua kunyamaza.

“Wawaeleze wanachama matumizi ya hizo fedha, zile za Okwi zishaletwa zaidi ya Sh milioni 600, halafu za mgawo wa mauzo ya Samata kutoka TP Mazembe kwenda Ubelgiji nazo zipo njiani,” alisema Rage.