22Mei2013

 

Kataeni soko la bidhaa feki, gomeni kuzinunua

WATANZANIA wakiamua kufanya jambo hulifanya kwa umoja na kuhakikisha limefanikiwa.

Uzoefu unaonesha hivyo, na kila mfuatiliaji wa mambo atakubali kuwa wakitaka kuwa na nia, wanaweza kuhakikisha wanachokitaka kinakuwa na wasichokihitaji hakipati nafasi.

Walifanya hivyo kwenye masuala mengi ya msingi yenye kugusa maslahi ya Taifa kama vile ubadhirifu wa mali na fedha za umma na kufanikisha kupaza sauti zao kuyapigia kelele kwa ushirikiano na vyombo vya habari.

Ni kwa sauti zao hizo za msingi, wahusika wa ubadhirifu walichukuliwa hatua mbalimbali za kisheria na kuufanya utumishi wa umma ueleweke miongoni mwa wengi, kwamba si mwanya wa kujilimbikizia mali na kuudhulumu umma, bali ni eneo la uwajibikaji kwa faida ya kila Mtanzania.

Hilo na mengine mengi yaliwezekana, lakini ni katika ngazi hiyo ya utumishi wa umma, inayomtaka aliyemweka mbadhirifu amwondoe kwa kufuata taratibu za ajira.

Hata hivyo, sauti ninayoizungumzia leo si hiyo ya maneno ya kumshinikiza mwajiri amwondoe mbadhirifu katika nafasi fulani au kumshinikiza ajiuzulu, nazungumzia ya kukataa kutenda.

Ndiyo hiyo inayofanana na kugomea jambo fulani kwa sababu za msingi zenye kukubalika hata kisheria, ambapo wagomaji lazima wawe wamejiridhisha kuwa uamuzi wao wa kukataa kulitenda hauathiri mifumo mingine ya uzalishaji, maendeleo na maisha ya wanajamii kwa jumla.

Nimekuwa nikijiuliza mara nyingi sababu za Watanzania kutotumia sauti hiyo yenye nguvu ya moja kwa moja kukomesha soko la bidhaa feki nchini, hivyo kufanya wanaolitumia kuathiri maisha ya wengine, kwa kuwaletea vyakula na bidhaa nyingine zilizo chini ya kiwango kwa mtindo wa kughushi uhalisia.

Nimekuwa nikijiuliza pia kuhusu mantiki ya watu kuendelea kung’ang’ana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili eti zikomeshe uingizwaji wa bidhaa bandia, wakati inaonekana wazi kuwa ngoma hiyo imekuwa nzito kwa mamlaka hizo, kiasi cha kuamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kuikomesha.

Siilaumu Wizara wala TBS katika waraka huu kwa sababu ninafahamu kuwa hata wananchi wenyewe wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa zisizo na ubora pamoja na zinazoghushiwa haziendelei kuwepo sokoni kwa kugoma kuzinunua.

Sina hakika kama Watanzania ninaoamini kuwa ni wajanja na wenye kujithamini, hawajui kuwa wana namna bora ya kuondoa bidhaa feki na halisi zenye upungufu wa ubora, katika soko lao, au pengine wanaozinunua kwa sababu ya unafuu ni wengi wanaoweza kufanya sauti za wachache zisipae na kuleta mafanikio.

Mimi nasema, kataeni kuzinunua mwone kama zitaendelea kuwa sokoni. Fanyeni hivyo hata kwa miezi michache tu mwone kama wauzaji hawatafunga maduka yao. Lakini mkiendelea kuwaunga mkono na kuwachangia mtaji kwa kununua mafuta bandia na sabuni zinazobabua, mtaishia kuwanufaisha huku mkijilundikia maradhi.

Ikumbukwe, kwamba soko haliwi soko bila mnunuzi, na mfanyabiashara anayejali faida kamwe nafsi yake haimwajibishi kumlinda mteja kwa kumwuzia chenye ubora unaostahili, bali hulenga kukuza mapato na faida kwa njia yoyote ile hata kama anazifahamu athari zake.

Cha msingi, wanunuzi waamke sasa na kutekeleza wajibu wao wa kulinda soko na wala wasisubiri Serikali kwa maana ya Wizara ya Viwanda na Biashara na TBS ndio wawalindie soko hata kama huo ni wajibu wao.

Hiyo ni kwa sababu, mambo mengi yanatendeka kwa pande zote zinazohusika na udhibiti wa bidhaa kabla ya kufikishwa sokoni na hakuna anayeweza kuthibitisha kwamba mamlaka au taasisi zinazohusika na udhibiti wa ubora wa bidhaa zinaweza kufanikisha kazi hiyo kwa asilimia 100 bila ushirikiano wa wanaolitumia soko ikiwa ni pamoja na wauzaji na wanunuzi.

Rushwa ipo nchini na imegusa maeneo mengi likiwamo la wasimamizi wa ubora wa bidhaa sasa kama Watanzania hamtatumia sauti yenu kwa njia ya kufanya uamuzi mzuri wa kutonunua bidhaa zisizofaa, zitaondokaje sokoni?

Mnaoweza kuzitambua zisizofaa tafadhali zisuseni. Aidha, nashauri wizara ya biashara na TBS zitoe elimu kwa wananchi waweze kuzitambua zilizoghushiwa na zisizo na ubora.