22Mei2013

 

Waliofeli wasibezwe, watiwe moyo

KAMA kuna zumari ambalo limelia kwa sauti kubwa kwa kipindi cha tangu Februari hadi sasa, si lingine, bali hili la matokeo ya kidato cha nne ambayo ni mabovu kuliko yote kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania; matokeo ambayo yamesababisha baadhi ya wanafunzi kujiua kwa kujinyonga baada ya kufeli mtihani wao.

Mhitimu aliyejiua Tabora ni Michael Fidelis (19) wa Mtaa wa Mwinyi, Kata ya Chemchemi aliyemaliza Sekondari ya Kanyenye; wakati Dar es Salaam, aliyejiua baada ya kufeli ni aliyekuwa mwanafunzi wa Sekondari Debrabant, Mbagala, Temeke, Barnabas Venant (18).

Yote ambayo yameshazungumzwa mpaka sasa kuhusu aibu hii, ni mengi na mazito kutoka kila kona ya nchi. Kwenye mitandao ya kijamii nako mjadala ulishika kasi. Hili linauma si kidogo.

Lakini, pamoja na kuwa na uchungu ilinilazimu kukumbuka ile methali isemayo; ‘maji yakishamwagika hayazoleki’. Nitoe pole za dhati kwa familia zilizofiwa na shule walizosoma hao vijana waliotangulia mbele ya haki kwa kushawishiwa na ibilisi aliyetuma pepo la mauti kwa wadogo zetu hao.

Vijana wote waliofeli na hata waliofaulu, wote wanahitaji ushauri nasaha. Wanahitaji ushauri nasaha kwa sababu, wengi wao waliingiwa na kihoro tangu kwenye vyumba vya mitihani. Kadri siku zilivyokuwa zikisogea, ndivyo walikuwa wakiweweseka.

Hata hivyo, wazazi, walezi na majirani wa wanafunzi wote kwa njia moja au nyingine, wana mkono katika aibu hii ya matokeo mabovu. Wapo wanafunzi wengi hata wa Dar es Salaam, wanakwenda shuleni asubuhi bila kifungua kinywa.

Na baada ya hekaheka na makondakta wa daladala, wakiwa shuleni wanakula ‘chipsi dume (muhogo)’ na maji. Wazazi na walezi naomba tuwe waaminifu. Watoto wetu wanakula chakula bora cha kutosha na kwa wakati mara ngapi kwa mwezi?

Nyumba nyingi Dar es Salaam hazina umeme. Kwa muda mrefu nimeshuhudia watoto wakiwa wanafanyia kazi za shuleni huku wamekaa barazani kwa watu wakidowea umeme huku waking’atwa na mbu!

Kalizuka mtindo (unaendelea) kwa wanafunzi kujisomea kwa marafiki (hata kama wote kwao kuna umeme) lakini wanafunzi hao ni wa jinsi mbili tofauti, na wanasoma chumbani hadi saa za usiku! Yawezekana wapo wengi tu waliofeli lakini hawako katika maeneo hayo na wanaishi maisha mazuri, hilo ni sawa.

Swali langu kwa wanafunzi wote, ni kwamba ni nani anaishi wapi, wa umri gani aliyesema eti ukifeli mtihani umefeli maisha? Historia inatuonesha msururu mrefu wa watu mashuhuri; mabilionea wa dunia ambao si tu kwamba walifeli mtihani; ila hata hawakupata kukanyaga shule kabisa! Wapo wengi tu.

Hata hivyo, uwapo wao usitumike kama kisingizio cha sisi kutosoma. Ikumbukwe, kuwa tunajifunza kwa walioshinda si walioshindwa. Kwa ujumla, inawezekana kuna sababu nyingi zilizosababisha matokeo mabovu lakini, tumewafariji, kuwashauri na kuwatia moyo watoto wetu kwa kiasi gani?

Mwisho, kila mwanafunzi popote alipo akumbuke kuwa; hakuna mwingine kama yeye; hivyo, ni mtu maalumu usiwe mtu mwingine. Pambana siku moja utashinda. Aluta continua.