Tahariri: Weledi uwaongoze wanahabari Uchaguzi

TANZANIA mwaka huu inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu na vyombo vya habari ni moja ya wadau wakubwa katika kufanikisha hatua hiyo ya kidemokrasia na ya Kikatiba ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka ama kuwakubali kuanzia ngazi ya rais, wabunge na madiwani.
Tukiwa katika maandalizi kuelekea hatua hiyo muhimu katika taifa letu, serikali imevikumbusha na kuviasa vyombo vya habari jukumu lake la kuhakikisha vinaripoti habari za uchaguzi mkuu kwa haki ili wananchi wapate taarifa sahihi.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ jijini Dodoma akifunga Mkutano wa mwaka wa Vyombo vya Utangazaji nchini uliondaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alikumbusha wajibu wa vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu kwa kuvitaka kutoa habari sahihi.
Katika hili tunapenda pia kuungana na serikali kukumbushana umuhimu wa vyombo vya habari kama silaha kuu na kutambua vikitumika vibaya ni rahisi kuizamisha demokrasia na amani iliyopo.
Huu ni wakati wa kukumbushana wanahabari kutumia kalamu zetu na vyombo vyetu vya habari kwa kuwapa wananchi taarifa sahihi za vyama na wagombea ili waweze kufanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa taifa.
Kuna mifano ya nchi na mataifa ambayo yamejikuta yakiingia katika migogoro ya kisiasa na vurugu, huku vyombo vya habari au waandishi wa habari wakidaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine kutokana tu na kuandika habari za uchochezi au kupendelea upande mmoja.
Tunaamini vyombo vya habari vikitumia vizuri nafasi na uhuru wa kuhabarisha Watanzania kuanzia kuwatambulisha wagombea, kampeni na hadi upigaji kura basi uchaguzi huu utafanyika kwa amani na utulivu.
Lengo letu ni kukumbusha wajibu kama vyombo vya habari kuhakikisha uzalendo unawekwa mbele na kamwe wanahabari wasikubali kutumika vibaya na wanasiasa wenye nia ovu kwa kugombanisha wananchi na wagombea au vyama vya siasa.
Matumaini yetu vyombo vya habari vikisimamia weledi, taaluma na maadili yake hakuna kitakachoharibika na uchaguzi wa mwaka huu utafanyika na kukamilika vizuri, huku wananchi wakipata viongozi waliowachagua kwa haki yao ya kupiga kura.
Great blog! Do you have any recommendations for aspiring
writers? I’m hoping to start my own website soon but I’m a little lost on everything.
Would you recommend starting with a free platform like WordPress or go for a paid option? There are so many options
out there that I’m totally overwhelmed ..
Any suggestions? Cheers!