Dunia kushuhudia mazishi ya Malkia leo

RAIS Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi wa mataifa mbalimbali katika mazishi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza.

Samia ambaye aliwasili jijini London, Uingereza Jumamosi, anajumuika na viongozi wa nchi na serikali wapatao 100 walioalikwa  kushiriki maziko ya kiongozi huyo yanayofanyika leo.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, Samia  aliungana na viongozi wengine kutoa heshima za mwisho kwa marehemu katika eneo la Westminster Hall na kusaini kitabu cha maombolezo kabla ya kuhudhuria hafla fupi iliyoandaliwa na Mfalme Charles III.

Samia na viongozi wengine, leo wanahudhuria mazishi ya kitaifa yanayofanyika kwenye Kanisa la Westminster Abbey kabla ya maziko yatakayofanyika katika kasri la Windsor.

Mtanzania aliyewahi kupata mwaliko wa Malkia Elizabeth na kutunukiwa tuzo ndani ya kasri, Aseri Katanga anayeishi Uingereza, alilileza HabariLEO kuwa Rais Samia amefanya vyema kuungana na viongozi wengine kumzika Malkia.

“Ameifungua Tanzania upande wa kimataifa…na sisi tunatakiwa kutambuliwa kwa kuwakilishwa na Mama Samia… Isingeleta sura nzuri kutohudhuria maana ni sehemu ya nchi za Jumuiya ya Madola na wana mwaliko rasmi,” alisema.

Aliongeza, “Malkia alikuwa mkuu Common Wealth (Jumuiya ya Madola), Tanzania ikiwamo na malkia amekaa madarakani kwa miaka 70 kwa hiyo amepata kujua viongozi mbalimbali. Aliwahi kumualika pia Nyerere (Mwalimu Julius Nyerere) kwenye kasri…alikuwa kiongozi mzuri katika ulimwengu wa leo.”

Katanga ambaye ni mwanzilishi wa Kampuni ya Computers 4 Africa nchini humo, alisema pia amepata mwaliko wa kushiriki maziko leo kutokana na ukaribu wake na familia ya Malkia uliotokana na tuzo aliyopewa Oktoba 28 mwaka 2013 kutambua mchango wake wa kusambaza kompyuta kusaidia watoto katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.

Mtanzania huyo aliyeishi Uingereza tangu mwaka 1979 alisema licha ya wanaoishi eneo la Windsor kupewa nafasi ya ushiriki, yeye na wengine ambao walikuwa wakifahamiana na malkia wamo kwenye kanzi data ya kasri hivyo wamepewa fursa ya pekee.

Katanga ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Ishozi, Wilaya ya Missenyi katika Mkoa wa Kagera, alisema haijawahi kutokea msiba nchini humo uliofikia wingi wa watu kama huu wa malkia Elizabeth II.

Alisema leo ni siku ya mapumziko Uingereza na walitangaziwa kuwa ndege hazitaruka hivyo usafiri utakuwa kwa treni na mabasi hasa treni kutoka London hadi Windsor inayopita katika njia iliyopewa jina la Elizabeth Line.

Alisema pia hoteli za karibu zimejaa wageni na kila kitu kimekuwa ghali.”Hakuwa malkia wa Uingereza pekee bali wa dunia,” alisema Katanga.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button