loader
Picha

Tanzania kushiriki kifua mbele mabadiliko ya vipimo duniani

TANZANIA ni miongoni mwa mataifa yanayoshiriki maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani (World Metrology Day). Maadhimisho haya yanafanyika kila mwaka ifikapo Mei 20. Kutokana na utamaduni huo, mwaka huu, Tanzania imeungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hii.

Chimbuko la siku ya vipimo duniani ni kumbukumbu ya kusainiwa kwa Mkataba wa Mita (Metre Convention) uliotiwa saini na mataifa 17, Mei 20, mwaka 1875. Uliweka mazingira sahihi kuiwezesha dunia kushirikiana katika masuala ya sayansi ya vipimo na matumizi yake katika viwanda, biashara na jamii. Lengo hasa la mkataba huu lilikuwa kuhakikisha duniani kote vipimo vinafanana, hatua iliyolenga kuondoa mkanganyiko wa matumizi ya vipimo visivyofanana.

Kimataifa, Siku ya Vipimo Duniani huandaliwa na kudhaminiwa na taasisi mbili. Taasisi hizo ni International Bureau of Weights and Measures (BIPM) na International Organization for Legal Metrology (OIML). Nchi hizo zilikubaliana kutumia vipimo vya aina moja. Hadi sasa hakuna nchi inayoweza kufanya vipimo bila kufuata mfumo uliokubaliwa. Tanzania ikiwa mdau wa mkataba huo, mwaka huu ilishiriki maadhimisho Siku ya Vipimo Duniani kupitia maabara ya ugezi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kaulimbiu ya maadhimisho haya ilikuwa: “Mageuzi ya Mfumo wa Kimataifa ya Vizio vya Vipimo.” Kaulimbiu hiyo inatokana na mapendekezo ya mageuzi hayo yanatokana na utafiti uliofanyika kuhusu mfumo mpya wa upimaji wa kisayansi kwa kutumia sheria za Fizikia zinazotumia; “Quantum phenomena”. Yote haya yamechochewa na kukua kwa sayansi na teknolojia. Mageuzi haya yanahusu maeneo manne ya vizio vya vipimo kama kilogram, Ampere, Kelvin na Mole.

Huu ni mwanzo wa kampeni kuelekea marekebisho ya kihistoria ya Vizio vya Vipimo Duniani inayotegemewa kupitishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Shirika la Vipimo Duniani (BIPM), Novemba, 2018. Kuelekea mabadiliko haya, Bendera ya Tanzania itapeperushwa na TBS. Ifahamike kuwa, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), ndicho chuo pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki kinachofundisha fani ya Mizani na Vipimo kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada. Mkuu wa Chuo CBE, Profesa Emmanuel Mjema, anasema kutokana na mabadiliko yanayotokea duniani, lazima kuwepo mabadiliko ya vipimo.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Profesa Mjema anasema: “Lazima pawepo na mabadiliko ya vipimo...lazima na sisi (Watanzania) tubadilike kwani tunaenda na mabadiliko ya teknolojia.” Mtaalamu wa masuala ya vipimo ambaye kwa sasa ni mstaafu, Peter Elias (71) anasema; “Mahitaji wa wataalamu hao ni makubwa kuliko idadi ya wataalamu wanaozalishwa kwa mwaka.

Sekta hii ni mtambuka kwani inagusa maeneo mbalimbali ya maisha ya mwanadamu na huchangia maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mazingira, teknoloji, gesi, ubunifu mambo ambayo yote yana vipimo vyake.” Anatoa mwito kwa vijana nchini kuchangamkia fursa za mafunzo katika fani ya vipimo na uendeshaji wa mitambo mbalimbali kwa kuwa wachache waliokuwepo kama yeye wamestaafu. “Kwa hiyo, ili tujenge viwanda, lazima tuwe na wataalamu wazawa kutoka ndani ya nchi yetu,” anasema.

Mmoja wa wanafunzi wa CBE bila kutaka jina litajwe anasema mafunzo anayopata yanalenga kuwajengea uwezo wa kubuni na kuanzisha vifaa vyao wenyewe vinavyoweza kutumika kwenye masuala ya mizani na vipimo. Anasema mabadiliko ya Novemba ya vipimo yatawakuta wameandaliwa kikamilifu kwenda sambamba na matakwa ya dunia.

Kwa Tanzania, mtu anapozungumzia maabara hasa zile zilizopata vyeti vya umahiri, ni lazima atagusia Maabara ya Ugezi TBS ambayo ni mdau mkubwa kwenye mabadiliko hayo ya vipimo yanayotarajiwa. Maabara hii ilianzishwa mwaka 1982 ili kuwasaidia wazalishaji kuongeza ubora wa bidhaa zao, kwa kuzingatia viwango vilivyo nchini au vya kimataifa ili kumlinda mlaji na kumfanya atumie bidhaa zinazokidhi ubora. Vipimo hupimwa kwa kuzingatia matakwa ya wateja na hasahasa, viwango vya kimataifa.

Maabara hii inaongozwa na Kaimu Mkuu wa Maabara ya Ugezi, Joseph Mahilla anayesema, ugezi ni hali ya kulinganisha vipimo kati ya kile kinachopimwa na kipimo kile ambacho ni kiwango (chenye thamani inayojulikana). Anasema maabara ya ugezi imepewa dhamana ya kuwa msimamiaji na mtunzaji mkuu wa vipimo vya kitaifa katika Tanzania na hivyo, kutoa nasaba (traceability of measurements) kwa wote wanaojishughulisha na vipimo nchini.

“Hii ndiyo maabara pekee Tanzania yenye jukumu la kutunza vipimo vyenye uhakika wa juu kabisa na hivyo, kuwa ndiyo pekee yenye kutoa nasaba kwa taasisi, mashirika na wadau wengine wote wa vipimo nchini Tanzania,” anasema Mahilla. Kwa mujibu wa Mahilla, Shirika la Viwango Tanzania kupitia maabara hii hutoa nasaba kupitia utaratibu uitwao ‘ugezi’ (kunasibisha vipimo). Ugezi hufanywa katika maabara ya Shirika hilo inayojulikana kitaalamu kama Metrology Laboratory.

Maabara hii inafanya ugezi katika nyanja za tungamo (Mass), ujazo mdogo, jotoridi, muda na masafa, vipimo urefu, mgandamizo, umeme na vipimo vya kani. Kwa mujibu wa Mahilla, maabara ya huduma za ugezi (Metrology), ilipata cheti cha umahiri kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na mara ya pili mwaka 2010 katika eneo la urefu na maeneo ambayo maabara hiyo imepata cheti cha umahiri baada ya kutathminiwa na mashirika mawili makubwa ya South African National Accreditation System (SANAS) na Shirika la SADCAS ni katika vipimo vya vya jotoridi (temperature) , tungamo (mass), Ujazo mdogo, urefu pamoja na muda na masafa.

Kutokana na maabara hiyo kupewa cheti cha umahiri cha utendaji kazi kwa kuzingatia kiwango cha kimataifa cha ISO\IEC17025 ilitambulika duniani kote na kuifanya Tanzania kuwa ya nne barani ya Afrika, ikitanguliwa na nchi za Kenya, Afrika Kusini na Misri. Mahilla anataja vigezo vinavyotumika ili maabara itambuliwe kimataifa kuwa ni lazima iwe na mfumo rasmi (ulioandikwa) wa utendaji kazi, umahiri wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wenyewe katika ugezi, na mbinu zinazotumika katika ugezi kuwa zinakubalika kimataifa. Vigezo vingine ni mazingira ya upimaji na ugezi kukubalika kimataifa na uwiano wa majibu.

Pia upatikanaji wa vielelezo vinavyoonesha mchakato mzima wa upimaji hadi matokeo kupatikana ni jambo la umuhimu.Kuhusu faida ya kuwa na cheti cha umahiri, Mahilla anasema maabara ikitambulika kimataifa vipimo vyake vinakubalika duniani kote. Anasisitiza kuwa vipimo vinapokuwa sahihi vinapunguza hasara na madhara kwa watumiaji. Faida nyingine za kutumia vipimo sahihi ni kukuza biashara, mtoa huduma kujiamini na vinalinda walaji na kusaidia kufanyika kwa biashara kimataifa.

Kuhusu mwitikio wa wadau mbalimbali ikiwemo wenye viwanda na wengine wa vipimo kwenda kugezi, Mahilla anasema: “Mwitikio ni mkubwa wote wanaoanzisha viwanda wanahitaji kugezi... Kwa hiyo maabara hii ndiyo ufunguo wa ubora kwa kila bidhaa na huduma zitolewazo na mchango wetu ni mkubwa kwenye ujenzi wa Tanzania ya viwanda... bila vipimo sahihi hakuna uthibiti wa ubora na viwanda vitakuwa vinatoa bidhaa hafifu.” Anasema viwanda vinavyofunguliwa na vilivyopo vinahitaji huduma ya ugezi, hivyo na wao wamejipanga kikamilifu kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Mahilla anasema licha ya huduma nzuri wanaendelea kutoa zipo changamoto wanazokabiliana nazo ukiwamo uwezo mdogo wa kifedha wa shirika unaochangia kushindwa kununua kwa wakati stahiki, vifaa vya kisasa vya ugezi vinavyoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayotokea duniani.

Anasema: “Nyingine ni miumdombinu ya maabara kutokuwa na uwezo kuruhusu upanuaji wa nyanja za ugezi inayotokana na kwamba, maabara hii ilijengwa mwaka 1982 ikiwa inakidhi mahitaji ya wakati huo, mahitaji ya sasa ya ugezi ni makubwa, hivyo uhitaji wa upanuzi wa maabara hii ni wa lazima.”

Mahilla anasema kwa Mwaka wa Fedha 2018/19, wanatarajia kupanua wigo wa umahiri wa ugezi katika eneo la Mgandamizo (Pressure) na mwendo wa mzunguko. Anasema: “Tunatarajia kuwa na maabara kubwa na za kisasa zaidi baada ya kukamilika kwa ujenzi unaoendelea katika shirika hil. Kutonana na umahiri wa maabara hii, Tanzania inakuwa ni mwakilishi mahiri kuelekea safari ya mabadiliko ya vipimo.”

KIPINDI cha Watanzania kutafuta uongozi wa nchi kimewadia tena ambapo ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi