loader
Picha

Kishikwambi kinavyoleta mapinduzi utengaji maeneo ya utafiti

NI mwendo wa karibu saa moja kutoka katikati ya Jiji la Dodoma hadi Kijiji cha Sasajila kilichoko barabara ya Iringa wilayani Chamwino. Huko kuna mradi wa majaribio ya matumizi ya teknolojia mpya ya kutenga maeneo (na kuweka mipaka) kwa ajili ya kazi mbalimbali za kitafiti ikiwemo Sensa ya Watu na Makazi.

Mrasimu Ramani Mwandamizi na Msimamizi wa Sehemu ya Mfumo wa Ukusanyaji na Usambazaji Taarifa za Kijiografia kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Benedict Mugambi akiwa na wataalamu wenzake wanatukaribisha wakiwa wameambatana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Sasajila. Anasema mradi huo unafanywa kwa pamoja kati ya wataalamu kutoka NBS, Ofisi ya Rais- Tamisemi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kusisitiza kuwa, ni mradi utakaoinufaisha serikali kwa kuipunguzia gharama na kueletea ufanisi katika utendaji wake.

Anasema maeneo yatakayonufaika zaidi ni pamoja na ukusanyaji wa takwimu, utambuzi wa mipaka, utambuzi wa maeneo ya kilimo na mifugo, maliasili na mengine mengi yanayohusu taarifa za kijiografia. Kazi hiyo ambayo kwa sasa inafanyika wilayani Chamwino katika vijiji vitano vya Sasajila, Suli, Fufu, Champumba na Chiboli inafanyika kwa kutumia kifaa kiitwacho Kishikwambi (tablet) kinachoonesha eneo husika katika uhalisia wake.

Anafahamisha kuwa, kifaa hicho kimeunganishwa na mawasiliano ya satelaiti katika mfumo mpya wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za kijiografia unaotumia mawasiliano ya satelaiti unaojumuisha mfumo wa taarifa za kijiografia (GIS) na Mfumo wa Utambuzi wa Maeneo (GPS) unaounganishwa na vifaa kama hicho (kishikwambi), simu za mikononi na komputa. “Kama mnavyoona hapa (anatuonesha) katika Kishikwambi tunaona kila kitu kupitia msaada wa mawasiliano ya satelaiti…tunaona tunavyotembea na tunaona kilicho mbele yetu ukiwemo mpaka wa kitongaji cha Ng’umbi na Amani kama alivyoeleza Mwenyekiti,” anaeleza Rahim Mussa ambaye ni Mrasimu Ramani kutoka NBS.

Anasema katika kuweka mipaka na maeneo muhimu ambayo mrasimu ramani anataka yaonekane katika eneo analotenga, anachotakiwa kufanya ni kuweka taarifa hiyo kwa kuandika na kuchora kwenye ramani iliyomo kwenye kishikwambi na akifanya hivyo, atakuwa amekamilisha kazi yake. “Tunapokuwa hapa tunaangalia vitu vyote muhimu vilivyomo katika eneo husika kama hii shule tulipo, hospitali, zahanati na kadhalika na hii itazisaidia wizara kama za elimu, afya, na Tamisemi kufahamu wapi kuna nini na kuweka taarifa zao vizuri,”anasema Rahim tukiwa katika eneo la Shule ya Msingi Sasajila.

Mugambi anasema teknolojia hiyo imerahisisha kazi za utengaji maeneo na zaidi inahamasisha uwajibikaji katika kazi. “Tofauti na zamani kwa kutumia teknolojia hii kazi yote ya kutenga maeneo inamalizika hapa hapa katika eneo husika kinachofanyika ofisi ni kuchapisha ramani,”anaeleza Mugambi huku akionesha kujiamini. Akitoa mfano wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 walikuwa wakitumia ramani zilizochorwa na Wizara ya Ardhi walizokwenda nazo katika maeneo mbalimbali na kunakili taarifa zilizomo.

Baada ya hapo, walikaa tena makao makuu ya mkoa kuweka sawa taarifa hizo. Mugambi anaeleza kuwa baada ya kukamilisha kazi hiyo mikoani ramani zilipelekwa katika Kitengo cha Taarifa za Kijiografia huko NBS na kuigizwa upya katika mfumo wa kidijiti ilipolazimu kuajiri mamia ya wafanyakazi wa muda kufanya kazi hiyo. “Ilitugharimu nguvu nyingi, muda mwingi na gharama kubwa kipindi kile, lakini sasa kwa kutumia teknolojia hii tunatumia muda mfupi na haraka,” anasema Mugambi.

Anaongeza kuwa teknolojia hii inawezesha kufuatilia kazi za watenga maeneo unapokuwa popote nchini na hata nje ya nchi. “Hatuwezi kudanyanga hapa, viongozi wetu wanaweza kufuatilia mwenendo wa kazi zetu kwa sababu popote tutakapokuwa kukiwa na mtandao na viongozi wetu wakiwa katika maeneo yenye mawasiliano ya kimtandao wanatuona,” anasema Mugambi na kuongeza kuwa ni hatua nzuri kwani inahimiza uwajibikaji. Namna ya kufanya kazi katika maeneo yasiyo na mtandao Mugambi anasema kabla ya kwenda katika eneo husika wanapakua (dowload) ramani ya eneo hilo kutoka kwenye mtandao wa ramani za mtandaoni (google map) na kuiweka katika Kishikwambi tayari kwa kuitumia wakiwa katika eneo husika.

Anasisitiza kuwa, tekinolojia hiyo hairuhusu makosa, hivyo taarifa zinazokusanywa zinakuwa na uhakika zaidi. “Mdadisi au ofisa yeyote atakayekwenda kufanya kazi za kitafiti au nyinginezo, atakabidhiwa kishikwambi kikiwa na ramani halisi ya eneo alilopangiwa ikionesha eneo na mipaka yake na maeneo yote muhimu,” anasisitiza. Mugambi anabainisha kuwa, hata mdadisi anapoingia eneo nje ya lile alilopangiwa, kishikwambo kitatoa alama kuashiria ametoka nje ya mipaka ya eneo lake. Martha Macha ambaye ni Mrasimu Ramani kutoka NBS anasema, timu yao haiweki mipaka mipya, bali wanaitumia ile inayotambuliwa na Wizara ya Ardhi na Tamisemi.

Kwamba, inachofanya timu yao ni kutenga maeneo ya kitafiti kama vile Sensa ya Watu na Makazi. Kinachotafutwa hasa Martha anasema maeneo ya kitafiti yalitengwa mara ya mwisho mwaka 2012 kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi na tangu wakati huo, miaka mingi imepita. “Tunachokitafuta ni kufanya maboresho… miaka kumi ni mingi... watu wamezaliana, wamejenga, huduma zimebadilika yawezekana hakukuwa na shule, hakukuwa na zahanati sasa vitu hivyo vipo,” anasema.

Anasema kutokana na mabadiliko kama hayo, hata maeneo ya kuhesabia watu yanaweza kubadilika. Mradi huu wa majaribio unafuatia mafunzo ya siku tisa yaliyotolewa kwa watumishi wa vitengo vya ukusanyaji na usambazaji wa taarifa za kijiografia na vitengo vya tekinolojia ya habari na Mawasiliano vya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia idadi ya watu (UNFPA).

Mafunzo hayo yaliyofanyika Dodoma Machi 19-27, 2018 na kusimamiwa na Kampuni ya Esri Eastern Africa ya jijini Nairobi nchini Kenya, yalilenga kuwajengea uwezo watumsihi wa vitengo hivyo kwa kuwapatia maarifa na ujuzi wa kutumia mfumo mpya wa kukusanya taarifa za kijiografia- (modern Mobile Geographic Information System–Technology (MGIS-T). Mfumo huu utatumika kutenga maeneo yatakayotumika wakati wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.

KIPINDI cha Watanzania kutafuta uongozi wa nchi kimewadia tena ambapo ...

foto
Mwandishi: Said Ameir

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi