loader
Picha

Tunajifunza nini kutoka kwa Wafaransa Kombe la Dunia?

WATU wengi tutakuwa tumeona mafanikio ya Ufaransa kwenye Kombe la Dunia yametokana kwa kiasi kikubwa na mchango wa wachezaji vijana wenye kujituma wenye asili ya Afrika.

Kutokana na idadi wachezaji weusi walio kwenye timu hiyo, inaelezwa Kocha wa Ufaransa kama angetaka, angeweza kupanga kikosi kizima chenye vijana wa asili ya Afrika. Nini tafsiri ya jambo hili? Ufaransa, Ubelgiji na kwingineko Ulaya, bado kuna vijana wengi wenye asili ya Afrika na wenye kiu ya kucheza fainali za Kombe la Dunia na hawapewi nafasi nchi wanazoishi.

Hawa akina Samuel Umtiti, Kylian Mbappe, Steven Nzonzi, Blaise Matuidi tunao wengi Ulaya. Wengine wana asili ya Tanzania. Tukiwawahi kabla hatujabanwa na sheria za Fifa, tunaweza kuvuna dhahabu inayotokana na Tanzania na iliyochakatwa Ulaya na ikatusaidia.

Na ilivyo kwa Fifa, mchezaji akishacheza hata mechi moja inayotambuliwa na Fifa akiwa na timu ya taifa, iwe ya wakubwa au vijana chini ya miaka 23, basi mchezaji huyo hawezi tena aslani kuchezea timu ya taifa ya nchi nyingine.

Ni kwa sababu hii, mdogo wake Paul Pogba, ingawa ni hodari katika soka na anatamani kuchezea nchi yao ya asili ya Guinea, hawezi kufanya hivyo kwani Wafaransa walikuwa wajanja kwa kumchezesha mechi moja tu akiwa na timu ya taifa ya vijana Ufaransa anakoishi.

Hivyo, hata kama hatachaguliwa kwenye kikosi cha Ufaransa, hawezi kuchezea Guinea kamwe. Na ukweli Tanzania kushiriki Kombe la Dunia inawezekana kama tukiachana na fikra za ukale.

Tukubaliane michezo ngazi za kimataifa ina nafasi kubwa kuitangaza nchi kuinua uchumi. Kwa Watanzania ili kuvuna dhahabu zetu zilizochakatwa Ulaya, yaani wale wanamichezo walioandaliwa vyema kwenye akademia za Ulaya na kwingineko duniani na wenye asili ya Tanzania, tunachohitaji ni kuwa na ujasiri wa kuzipa mgongo fikra za kizamani na kuweka sheria zenye tija kuhusu uraia/hadhi maalumu kwa wenye asili ya Tanzania ili tuwatumie.

Kwa kuanzia tuwe na sheria zenye kutoa uraia pacha kwa wanamichezo vijana wenye asili ya Tanzania. Ni ukweli, kuwa Waafrika na hususan Watanzania tunaweza pia kutimiza ndoto zetu.

Hebu tuangalie katika Kombe la Dunia jinsi Denmark ilivyotamba na kijana Yussuf Poulsen ambaye baba yake ni Mtanzania mwenye asili ya Tanga. Mara kadhaa, amesharipotiwa kutua nchini kusalimia ndugu na kujaribu kujipenyeza aitwe timu ya taifa, lakini hakufanikiwa, hivyo kuichezea Denmark, nchi asili ya mama yake.

Poulsen kwa sasa ni mchezaji wa klabu ya Ligi Kuu Ujerumani,Bundesliga, RB Leipzig. Ni dhahiri Tanzania ina akina Poulsen wengi sehemu mbalimbali duniani lakini juhudi hazijafanyika kuwashawishi wabebe bendera yetu.

Angalia vijana Akram na Ali Afif wanaoichezea timu ya taifa ya Qatar, wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia. Hawa ni watoto wa mchezaji wa zamani wa Simba, Hassan Afif mzaliwa wa Moshi aliyekulia Kariakoo, Dar es Salaam na kwingineko ndani na nje ya Afrika.

Tuangalie mfano mwingine wa Ghana, fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 Afrika Kusini. Ni pale kijana Assamoah Gyan alipokosa penalti muhimu kwa Afrika.

Ni penalti ambayo kama ingetinga wavuni, ingeandika historia mpya kwa Afrika. Na katika michezo na hususan kandanda, Ghana yaelekea kuwa moja ya ‘taifa kubwa’ katika kandanda, si tu Afrika, bali duniani. Ghana ina hazina kubwa ya wachezaji wa soka hasa vijana. Si wengi waliamini Ghana isiyo na Essien, Muntari, Apiah na majina mengine makubwa ingeweza kufanya maajabu kule Afrika Kusini.

Ghana ilifuzu kuingia hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza. Kuna mataifa makubwa katika soka hayakuweza kufuzu hatua ya makundi. Tunachojifunza kutoka Ufaransa ni umuhimu wa kujenga oganaizesheni na kujiamini.

Kuwekeza pia katika maendeleo ya kandanda ya vijana. Mshambuliaji Mbappe ameacha kumbukumbu ya kudumu. Ana miaka 19, anakuja juu kisoka. Hakika, fainali ya Ufaransa na Croatia, Mbappe ndiye aliyekuwa mchezaji nyota uwanjani. Hivi tunavyoandika, Mbappe ndiye nyota mpya wa Kombe la Dunia.

Tulimwona jinsi kijana huyu peke yake alivyoipangua ngome ya Croatia na kupachika bao la tatu kwa Ufaransa. Ndiye yeye pia aliyetoa pasi murua ya bao la nne la Ufaransa lililofungwa na Pogba. Watanzania tunaweza kutimiza ndoto. Tuwe na ujasiri tu wa kuzipa mgongo fikra za kizamani.

KAMA kawaida ya Watanzania hawawezi kufanya jambo lililotangazwa na serikali ...

foto
Mwandishi: Na Maggid Mjengwa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi