loader
Picha

Magufuli, Museveni kukuza biashara

RAIS John Magufuli ametaka nchi za Tanzania na Uganda, kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na umeme na miradi ya maendeleo ili kuendeleza uhusiano kati ya nchi hizo mbili hasa kwenye biashara.

Alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alikuwa na ziara ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Uganda.

Rais Magufuli alisema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Uganda ni mazuri na kwamba wanaendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara ili kunufaisha nchi zote mbili.

Alisema, "Tunataka kuimarisha biashara kwa nguvu na kwa kuanzia tumefufua treni ya mizigo kati ya Tanzania na Uganda ambapo kwa kuanzia imeweza kusafirisha tani 850 hadi 1,000 kwa safari moja ambapo kiwango hicho kingeweza kupata kusafirishwa kwa barabara kwa kutumia matrela 40 hadi 50.

"Kama wafanyabiashara watatumia treni hiyo vizuri watapunguza gharama kwa kuwa kwenye barabara gharama zake ni kubwa na hata huigharimu serikali fedha nyingi pale miundombinu inapoharibika," alisema Rais Magufuli.

Bomba la mafuta Kuhusu bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda, hadi Tanga, Rais Magufuli aliwataka mawaziri husika wa nchi zote mbili, kuharakisha mradi huo ili uanze kuwanufaika wananchi wote.

"Nataka mawaziri wahakikishe kuwa mradi huo unafanyika mapema kwa kuwa ni mradi wa kihistoria ambao utazidisha mahusiano kati ya nchi zetu," alisema Rais Magufuli.

Uagizaji wa sukari

Katika kuhakikisha kuwa bidhaa zinazalishwa ndani ya Afrika Mashariki, Rais Magufuli alishauri kuwa nchi wanachama wa jumuiya kuacha kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa kuwa zimekuwa zikiua viwanda vya sukari ndani ya nchi na kupoteza ajira nyingi kwa wananchi.

Rais Magufuli alisema, "Tunataka bidhaa za Uganda ziuzwe Tanzania, Kenya na Tanzania vivyo hivyo.

“Tatizo ni kuwa kulikuwa na bidhaa nyingi ambazo hazitengenezwi nchini Tanzania au Uganda ikiwemo sukari iliyokuwa ikiletwa nchini kwetu na kuchangia kuua viwanda na ajira kwa wananchi wetu.

"Mfano Zanzibar walisema wana sukari nyingi lakini mahitaji yao na uzalishaji hayakuwa na uwiano.

“Mahitaji yao ni tani 200,000, na wana uwezo wa kuzalisha kati ya tani 4,000 na 5,000 ambazo hazitoshelezi mahitaji yao, lakini walidai wanajitosheleza na wanaweza kuuza nyingine, kitu ambacho si sawa kwa sababu sukari hiyo ilikuwa ikitoka nje ya nchi," alieleza na kuongeza kuwa ana taarifa ya malori 20 yaliyobeba sukari ya magendo na kuyaingiza nchini kila siku.

Aliongeza; “Kama tunataka kujenga nchi zetu, suala la kukubali bidhaa zisizokuwa na ubora linatakiwa kuisha ili tuweze kupata maendeleo.”

Ununuzi wa meli mpya

Katika kuongeza uhusiano wa kibiashara, Rais Magufuli alisema kuwa tayari serikali ya Tanzania imetangaza zabuni ya ununuzi wa meli mpya, itakayoenda kuwa mbadala wa Meli ya Mv Victoria na kwamba itasaidia usafirishaji kati ya Tanzania na Uganda.

Kwa upande wake, Rais Museveni alisema kuwa Uganda ipo tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba biashara itaimarika kwa kuwa miundombinu ni rafiki.

Mkutano wa BRICS

Akizungumzia mazingira bora ya kibiashara yaliyopo kwenye nchi za EAC, Rais Museveni alisema yanaweza kuwafaidisha zaidi wawekezaji kuliko kwenda kuwekeza kwenye nchi za mabara ya Ulaya au Asia.

Rais Museveni alisema kuwa alipokuwa nchini Afrika Kusini, kuziwakilisha nchi za jumuiya hiyo kwenye mwaliko kwenye mkutano wa 10 wa viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi (BRICS Summit), alielezea mazingira mazuri ya kibiashara yaliyopo kwenye EAC.

BRICS Summit inawakutanisha viongozi wa juu wa nchi za Brazili, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Rais Museveni alisema kuwa alivyokuwa huko, alitoa hotuba kuelezea faida ya kuwekeza au kufanya biashara kwenye Jumuiya ya EAC.

"Nilieleza wataalamu kuwa wakija EAC watapata faida kwenye biashara zao na wataweza kupata faida kuliko ile ambayo watapata sehemu nyingine kama Ulaya na Asia.

"Sababu kuu nilizowaeleza ni kuwa Afrika Mashariki kuna miundombinu mizuri ikiwemo barabara, lakini pia niliwaeleza kuwa wanaweza kuwekeza kwenye viwanda na mahoteli ikiwa ni uwekezaji kwenye sekta ya utalii," alisema Rais Museveni.

Mbali na kuzungumzia faida za kufanya biashara na nchi za Afrika Mashariki, pia alimweleza mwenyeji wake Rais Magufuli kuhusu hatua ya amani kwenye nchi za Burundi na Sudan Kusini.

Rais Museveni alisema, "Kuhusu Burundi, wakimbizi waliokuwa kwenye kambi za wakimbizi Tanzania wameanza kurejea nchini kwao na hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa watarudi na kuendeleza nchi yao.

"Kwa upande wa Sudan Kusini, hao wamemaliza vita na wameridhia amani na sasa tunashirikiana na nchi hiyo Sudan na Umoja wa Mataifa kuhakikisha wakimbizi zaidi ya milioni 1.1 wanarejea nchini humo na kuendelea na shughuli zao ikiwemo kilimo. “Pia kuna wakimbizi 300,000 kutoka kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) waliopo Uganda ambao nao wanatakiwa kurudi kwao".

Rais Magufuli alisisitiza kuwa ni vyema kuimarisha biashara ndani ya Jumuiya ya Afika Mashariki na pia aliwapongeza raia wa Burundi walioanza kurejea nchi mwao.

Alisema, "wakimbizi kutoka Tanzania wameanza kurejea kwao nchi Burundi na hiyo ina maana kuwa kumetulia. Kiukweli mara kadhaa ambapo tumewasikia wakisema wanarudi nyumbani, sisi tumefurahi kwani ni jambo zuri kwao."

Rais John Magufuli amemteua Dk. Michael Ng’umbi kuwa Mkurugenzi wa ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi