loader
Picha

'Kuna madereva hawajui kutafsiri alama barabarani'

JESHI la Polisi nchini limesisitiza umuhimu wa madereva nchini kupitia mafunzo ya udereva ili kuendesha vyombo vya usafiri kwa usalama kwa lengo la kuokoa maisha ili kupunguza vifo vinavyotokana na ajali.

Akizungumza Tanga, Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni alisema kazi ya ukaguzi wa leseni ni endelevu ila suala la uhakiki wa leseni za udereva halina mjadala kwa sasa kutokana na ongezeko la ajali.

"Unakuta dereva ana leseni halali lakini mpaka inakwisha muda wake hajawahi kuendesha gari, sasa huyu kwa nini tumpatie tena uhalali wa kumiliki hiyo leseni bila kumpatia mafunzo," alisema Kamanda Sokoni.

Aliongeza kuwa madereva wengi hawana ufahamu wa sheria na alama za barabarani hali inayosababisha kuendesha kwa uzembe na kusababisha ajali.

"Nina uhakika tukisimamisha baadhi ya madereva tukawauliza watutafsirie alama kumi za barabarani wanaweza kuzitambua kwa usahihi alama tatu au nne pekee," alisema.

Kutokana na ombi la madereva kuomba muda ili waweze kupitia mafunzo, Kamanda huyo aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limetoa muda wa miezi mitano kuanzia Agosti Mosi, mwaka huu kwa madereva kuhudhuria mafunzo hayo kabla ya uhakiki huo kuendelea.

Ukaguzi wa leseni ni lazima kwa kila dereva kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu Namba 77 ambapo dereva anapaswa kumuonesha askari polisi leseni yake pale anapohitaji kinyume na hapo dereva huyo atakabiliwa na kosa la uvunjaji wa sheria.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, madereva wa magari makubwa ya kubeba mizigo au mabasi ya abiria wanatakiwa kuhudhuria mafunzo kila baada ya miaka mitatu wakati wale wanaoendesha magari binafsi ni kila baada ya miaka mitatu kuanzia leseni daraja D kushuka chini.

Akifafanua, Kamanda Sokoni alisema ili dereva apande daraja la leseni ya juu, lazima awe amepitia mafunzo hayo ili aweze kujifunza kuhusu kujua matumizi sahihi ya barabara, kuzijua sheria mbalimbali za barabarani na kuendesha kwa kujihami.

Kamanda huyo aliomba vyombo vya habari kusaidia kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa usalama barabarani hasa kwa kipindi hiki ambapo ajali zimekuwa zikigharimu maisha ya watu, ongezeko la majeruhi na uharibifu wa mali.

Rais John Magufuli amemteua Dk. Michael Ng’umbi kuwa Mkurugenzi wa ...

foto
Mwandishi: Adam Lutta, Tanga

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi