loader
Picha

Mambo 10 kwa Magufuli Tanzania iwe kitovu vita ya uchumi Afrika- 4

Katika toleo lililopita, makala haya yaliishia katika aya inayosema: “Ufike wakati viongozi wa Afrika waone kuwa Afrika inaweza bila misaada au ikibidi kwa misaada kidogo na isiyo na masharti magumu kwani tayari msomi, Dambisa Moyo katika kitabu “Dead Aid,” cha mwaka 2009 aliwaanulia siri ya misaada ya nje isivyozisaidia nchi za Afrika kwani fedha nyingi, asilimia karibu 70 hurudi zilikotoka kupitia wataalamu na ununuaji wa vifaa vya miradi wanayokuja kuitekeleza huku.” Endelea...

Akihojiwa katika kipindi cha ‘This Week in Perspective’, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Maendeleo ya China (CCS), Profesa Humphrey Moshi anasema Afrika ina nafasi nzuri zaidi ya kujifunza kwa China ambayo miaka 50 tu iliyopita ilikuwa sawa kimaendeleo na baadhi ya nchi za Afrika, lakini sasa imepiga hatua kubwa.

Anasema, ni rahisi kujifunza kwa mtu ambaye mnakaribiana kuliko kwa nchi zilizoendelea zaidi ya miaka 200 iliyopita huko Ulaya kwani China ina nafasi nzuri zaidi ya kueleza jinsi ilivyozitumia baadhi ya tabia za kibepari na zikaifaa katika mazingira ya kijamaa na kuendelea hadi ilipo sasa. Anasema, wakati mitaji ya nchi za Ulaya ni dola bilioni 38 Afrika, mitaji inayowekezwa na China ni zaidi ya dola bilioni 200 inayoonesha China ilivyodhamiria kusaidia Afrika kuendelea katika mawasiliano, mitaji, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, bandari na rasilimali watu huku ikijiepusha kuingilia masuala ya ndani ya nchi kama walivyokubaliana katika mkutano wa Bandung Conference wa mwaka 1955 ulioweka msingi wa usawa kati ya nchi bila kujali udogo.

IFANYIKE TATHMINI YA VITA KUJUA ATHARI/FAIDA Kwa kuwa katika vita yoyote kuna kushinda na kushindwa, iko haja nchi za Afrika kutafakari na kutathmini utayari wake, uwezo wake, uthabiti wake wa kupigana vita hii, athari zitakazozipata na jinsi zitazikabili kama zitashindwa na kama zitashinda, zitatumiaje fursa hiyo mpya kujiendeleza zaidi bila kutegemea misaada hiyo. Wakati wa vita vya ukombozi wa Afrika, lengo lilikuwa ni nchi zote za Afrika ziwe huru ndio Tanzania nayo ijione imekuwa huru.

Vita ya uhuru wa kisiasa iliisha kwa ushindi, lakini iliacha makovu ya athari za uchumi ambazo hadi leo zinaendelea kufanya wengine watamani kuona nchi kama Afrika Kusini zenye uchumi mzuri, zikitoa mchango zaidi kwetu. Ni wazi, vita hii tukishinda itatuacha huru zaidi kisiasa na kiuchumi na tukishindwa, itatuacha hoi. Waswahili walisema kupanga ni kuchagua. Ukweli ni kuwa, tukitaka, tusitake, lazima vita hii ipiganwe kama nchi moja moja kivyake au na nchi za Afrika kwa umoja wake kama bara jambo ambalo ni bora zaidi.

Lazima vita ipiganwe kwa sababu, nchi zote zina kiu ya maendeleo na kinachochelewesha maendeleo yake, ni uchumi duni unaotokana na kutegemea zaidi misaada badala ya kujitegemea zenyewe au kutumia misaada isiyo na masharti. Tathmini hiyo ioneshe muda ambao vita hiyo itapiganwa, ni miaka mingapi, 10, 30 au 50 kabla ya kupima mafanikio yake, ianishe vikwazo na changamoto ambazo huenda nchi hizo zikakumbana navyo na njia za kuzitatua.

Ifanye hivyo ikiwa na mifano hai ya nchi au viongozi ambao wamekuwa waathirika wa vita ya uchumi katika nchi zao Afrika au nje ya Afrika kama Muammar Gaddafi wa Libya aliyeuawa kwa sababu ya kutaka Afrika isimame kidete akiwa na rekodi ya kuipa uchumi mzuri nchi yake kwa sababu ya hazina ya mafuta safi akitoa msaada kwa nchi nyingine Afrika akililia Afrika moja.

Mwingine ni Patrice Lumumba wa iliyokuwa Zaire (Congo DRC) aliyeuawa na Wabelgiji akiiacha maskini lakini yenye utajiri wa madini, Saddam Hussein wa Irak aliyeuawa akiiacha nchi za magharibi zikinufaika na mafuta baada ya vita vya Ghuba na Nyerere aliyelazimika kupigana vita na Amin na kulazimika kutumia hazina yake kubwa ya fedha za kigeni vitani na kuishia kwenye matatizo ya uchumi miezi 18.

Kama China iliyokuwa masikini miaka 50 iliyopita iliweza kiasi leo ina jeuri kuikopesha hata Marekani, vipi nchi za Afrika zishindwe? Afrika itumie vema fursa za uwekezaji kutoka China, India, Japan na nchi rafiki za Ulaya kujitoa kwenye makucha ya misaada yenye masharti yanayofungamanishwa na demokrasia. HITIMISHO Ni kweli vita ambayo Afrika inataka kuianza ni ngumu na inahitaji msaada kukabiliana na hali ngumu watoa msaada watakapokatisha ghafla misaada yao au kuweka vikwazo kama fimbo ya kuzilazimisha ziendelee na utegemezi.

Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa diplomasia ya vikwazo haina nguvu tena siku hizi kama inavyojidhihirisha katika sakata Marekani kuibana Iran kuhusu usitishaji utengenezaji wa nyuklia ambapo nchi za Ulaya, Urusi na nyingine zimekataa kutii agizo la Marekani kuendeleza vikwazo kwa Iran na hivyo kuamua kuendelea kufanya nayo biashara. Kutakuwa na vikwazo hivyo, lakini kwa kuwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kimeahidi kuisaidia Afrika katika vita hii, ni matarajio ya wengi nchi za Afrika zitakuwa na uwezo wa kuhimili mapito hayo zikiwa hata na nguvu zaidi ya ulinzi.

China ni nchi inayojiimarisha zaidi kijeshi katika nchi washirika. China inatekeleza Ujamaa wa Kichina wa Karne ya 21 katika muktadha huu unaolenga kuifanya ipige hatua kubwa kiuchumi na maendeleo. Inataka kuona Afrika hasa nchi zenye mwelekeo wa Ujamaa, zikinufaika na misaada yake isiyo na masharti magumu kama ile ya magharibi. Kutokana na matatizo ya nchi za Afrika kufanana, ndio maana CPC, CCM na vyama rafiki vya ukombozi vya Afrika viliona iko haja ya kulifanya suala hilo ajenda ya Afrika kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi kwa nchi zote ukombozi huakisi maendeleo ya wote si baadhi.

Ni vema Tanzania ikabeba jukumu hilo ikijua vita hii ina changamoto, lakini isikate tamaa kwani ina baraka za wanyonge wa Afrika na China na ijue majirani zake wasipokuwa na uchumi mzuri, itabeba mzigo wa wakimbizi na shida nyingine na kutumia rasilimali zake kuwasaidia na kuondoa maana ya maendeleo inayotaka kuyajenga katika awamu hii ni zijazo. Kwa kuwa Rais Kikwete aliwahi kusema akili za kuambiwa, weka na za kwako, basi iko haja wakati Tanzania ikiongoza vita ya uchumi, ikiona kuna nchi hazielewi somo hilo, iachane nazo na tusonge mbele na hao wachache hadi hapo watakapoelewa somo na kuungana nasi. Shime tumuunge mkono JPM katika vita hiyo.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha ripoti ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi