loader
Picha

Umuhimu wa migodi kunufaisha wananchi kwa miradi mikubwa

JUZI nilisoma habari moja kuhusu Kampuni ya Mantra kukamilisha ujenzi wa maktaba tano kwa ajili ya shule za sekondari wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii kutoka faida yake.

Kwa mujibu wa habari hiyo, moja ya maktaba hizo ilikabidhiwa na Mkurugenzi wa Mantra, Frederick Kibodya kwa Shule ya Sekondari Nanungu iliyoko Kata ya Hanga, Namtumbo. Kibodya anasema, mbali ya maktaba hizo tano, wamewezesha pia mradi wa umeme jua kwa mabweni matatu unaotarajiwa kuanza mwezi huu baada ya mkataba kusainiwa na wahusika. Anasema Mantra inaweka kipaumbele katika elimu, afya, usafi, ushirikiano wa biashara, mazingira na vita dhidi ya ujangili.

Katika kuchangia kuhakikisha wananchi wana afya njema, wanatoa pia msaada wa Sh milioni 100 za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo na Kituo cha Afya Mchomolo, miradi ya malihai club n.k. Kwa mujibu wa Kibodya, maktaba zile tano ni utekelezaji wa ubia na Shirika la Read International ulioanza mwaka 2013.

Hadi sasa mradi huo umeshagharimu Sh milioni 77 na kunufaisha wanafunzi 2,500 wa Namtumbo. Sambamba na misaada hiyo, Mantra ambayo ni kampuni tanzu ya Uranium One inayotafiti madini ya urani wilayani Namtumbo, iliko mbuga kubwa ya Selous, pia imetoa msaada wa kisima chenye thamani ya Sh milioni 12 kwa Shule ya Sekondari Selous, Kata ya Likulya.

Kibodya alikaririwa akisema mradi huo wa maji utawaondolea wananchi usumbufu wa kufuata huduma ya maji mtoni. Kimantiki, maji hayo siyo salama kwa kuwa kuna wanyama wakali wa Selous wanatumia maji hayo. Kama ilivyopokewa misaada ya maktaba na mingine iliyotolewa na kampuni hiyo, ndivyo pia hata kisima hicho kilivyopokewa na wananchi na viongozi wao; kwa furaha kubwa, vifijo na vigelegele kwani adha yao imeondoka. Naungana na wananchi hao na viongozi hao kuwashukuru na kuwapongeza Mantra na kampuni mama, Uranium One kwa misaada yao iliyolenga kunufaisha jamii inayozunguka mradi wa mgodi wa urani ambao wanatafiti hadi leo.

Hata hivyo, ningefurahi zaidi kama Mantra na wawekezaji wengine nchini hasa katika migodi ya dhahabu, almasi, tanzanite, ruby na madini mengine yaliyopo Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara, Arusha, Morogoro, Tanga watatafakari tena na tena aina ya misaada wanayoitoa kwa jamii. Nasema haya nikirejea mzozo wa Desemba, 2012 Johannesburg, Afrika Kusini katika mkutano wa wahariri 25 waandamizi kutoka nchi za Afrika Ubalozi Mdogo wa Marekani.

Katika mkutano huo, wahariri hao, nikiwemo mimi, walieleza kutofurahishwa kwao na jinsi vyombo vya habari vya nchi za Magharibi visivyoitendea haki Afrika kwa kuripoti habari zinazoakisi bara hilo kama lenye shida pekee, jambo ambalo si kweli kwani zipo neena na fursa yingi, shida na si neema. Wahariri wengi walielekeza zaidi lawama zao kwa luninga ya Marekani CNN huku wahariri kutoka Kenya wakieleza kusikitishwa na jinsi ilivyoripoti habari ya ghorofa kuanguka Nairobi na kuua watu wakihusianisha na tukio la ugaidi wakati mwandishi aliyetuma habari hizo kwao hakusema lilikuwa tukio linalohusiana ugaidi.

Mwakilishi wa CNN Afrika Kusini alikiri upungufu huo, lakini hakuondoa machungu ya mwandishi wa makala hii kuhusu CNN kupitia kipindi cha Inside Africa 2012 kudai wananchi wa Geita na Usukumani, Mwanza, Shinyanga hupenda kuua watu wenye ualbino ili watajirike. Nikiwa nimetoka kutazama kipindi hicho CNN siku chache kabla ya kwenda Afrika Kusini kwa semina ya uandishi wa habari za uchunguzi Afrika ulioenda na ufunguzi wa Taasisi ya Habari ya Marekani Afrika (Africa Media Hub), sikufurahishwa na maudhui ya kipindi hicho.

Kutokana na kutofurahishwa nacho, nilitumia fursa ile kueleza masikitiko yangu kama mtu ninayetokea Misungwi, Mwanza. Huko pia, kuna maeneo yenye dhahabu na watu wenye ualbino na baadhi wamekuwa wakiuawa au kunusurika na kubaki na ulemavu wa kudumu. Nilieleza kutofurahishwa kwa sababu, kipindi kile kililenga kuiaminisha dunia kuwa, watu wa Geita na maeneo mengine yenye madini hasa dhahabu wanatumia albino kwa imani za kishirikina kwa imani kuwa viungo vyao ndio vitawapa utajiri.

Kwamba wapo watu wenye imani hizo si suala la mjadala kwani mwanahabari nguli, Vicky Ntentema alifanya uchunguzi na kubaini mengi na Serikali ilichukua hatua kudhibiti mauaji yao. Lakini wakati hilo likidhibitiwa na Serikali, changamoto za sababu za CNN kudai watu wanaua albino kutaka utajiri hazijamalizwa na kufanya watu wa Geita na maeneo ya madini waonekane wabaya wakati kumbe ni maskini kwa sababu rasilimali yao inachukuliwa buree. Ni hali hiyo ya dunia kuaminishwa kuwa Wasukuma wanaua albino ili watajirike iliyonifanya niseme katika mkutano ule nilivyokerwa na maudhui ya kipindi cha CNN kujenga picha potofu kuhusu Afrika; Tanzania, wananchi wake na imani zao.

Nilisikitika zaidi baada ya mmoja wa wahariri kutoka Zimbabwe kusimama na kusema kuwa alishirikiana na mtangazaji wa CNN kuandaa kipindi kile kilichowadhalilisha Watanzania. Nilieleza katika hadhira ile jinsi kampuni za nje yanavyovuna rasilimali za Afrika na kwenda nje kwa kigezo cha uwekezaji na kuaacha watu wakiwa maskini wakati zilitakiwa ziwanufaishe. Kwamba Tanzania ilikuwa mwathirika wa uchotaji rasilimali hizo. Uchotaji huo umethibitishwa na hatua za Rais John Magufuli kuziba mianya yote ya uvunaji madini nchini kwa kuzuia mchanga wa dhahabu kwenda nje na kutunga sheria mpya ya madini.

Pamoja na kumpongeza Rais JPM kwa jitihada hizo kubwa kudhibiti rasilimali, nionavyo bado safari ya haki katika biashara ya madini nchini ni ndefu. Iko haja wawekezaji kunufaisha zaidi jamii za jirani na migodi kwa miradi mikubwa. Ni kwa kurejea makala ile ya CNN nimeamua kuwaomba kwa heshima kubwa wawekezaji wote nchini, kuzipa jamii, miradi ya maana ya kudumu na yenye maslahi mapana kwa jamii na inayolingana au kukaribia thamani ya madini. Mwaka 2011 nilibahatika kutembelea mgodi wa Uranium One na kampuni yake tanzu ya Mantra nikiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa chini ya James Lembeli aliyekuwa mbunge wa Kahama.

Niliyoyaona huko yalinifanya niulize watu wa Namtumbo wangependa wafanyiwe kitu gani ili thamani ya madini hayo iendelee kujiakisi hata siku yakimalizika kuchimbwa. Hata hivyo, nilifikia hatua ya kujijibu na jibu lilikuwa angalau wajengewe chuo kikuu ili watoto wao na wengine nchini, wasome huko. Kwa kujenga chuo kikuu na si miradi midogo midogo, wahitimu wake wanaweza kuendelea kuwa chanzo cha mapato miaka nenda rudi na kukaribiana na thamani ya madini yao kwani maprofesa watakaopatikana huko, wanaweza kwenda hata nje kufanya kazi na kuingiza fedha za kigeni zitakazoakisi madini yanayovunwa.

Hali inapaswa kuwa hivyo pia kwa madini ya almasi huko Shinyanga, dhahabu Geita, Mara, Mwanza, Handeni (Tanga), Tanzanite (Arusha) na Manyara ambako bado wananchi wake ni maskini licha ya kulala juu ya utajiri wa madini. Ni matumaini yangu, Mantra wataichukua hoja yangu kama changamoto ya kufikiria kujenga chuo kikuu Namtumbo si kupeleka umemejua, maktaba, kisima cha Sh milioni 12 na hospitali. Na hata wawekezaji wa almasi Mwadui nao waone haja ya kujenga Chuo Kikuu kikubwa kama Udom huko Shinyanga au Mwanza kwa ajili ya kanda ya Ziwa kupunguza ulazima wanafunzi wa huko kuja kusoma Dar es Salaam.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha ripoti ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi