loader
Picha

Taasisi ya Korea - Afrika ilivyogeuka daraja la ushirikiano kiuchumi, kijamii

UMUHIMU wa Bara la Afrika kwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa kimaendeleo duniani, unaongezeka siku hadi siku na kufanya mataifa hayo yabuni mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhusiano wao na nchi za bara hilo katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kijamii na kiuchumi.

Jamhuri ya Korea ni miongoni mwa mataifa ambayo yameanzisha mikakati ya makusudi ya kushirikiana na nchi za Afrika kwa lengo la kupata faida za pamoja na kuanzisha taasisi maalumu ya kushughulikia masuala ya Afrika ijulikanayo kama Korea- Africa Foundation. Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Oscar Mbuza yaliyofanyika mjini Seoul, Rais wa taasisi ya Korea- Afrika, Balozi Choi Yeon-ho anaeleza mikakati ya nchi yao kukuza ushirikiano na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano: SWALI: Korea- Africa Foundation ni taasisi ya aina gani, ilianzishwa lini na yapi ni majukumu yake ya msingi? JIBU: Kama inavyofahamika nchi mbalimbali za Afrika zipo katika harakati za kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ili kujipatia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa watu wake. Jamhuri ya Korea kama mbia muhimu wa maendeleo katika dunia ya sasa iliona kuna umuhimu wa kuwa na taasisi kama hii ili iwe kiunganishi muhimu kati yake na mataifa ya Afrika kuchochea maendeleo ya pande zote. Bunge la Jamhuri ya Korea ndilo lililoazimia kuanzishwa kwa taasisi hii chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea (MOFA), uamuzi uliopitishwa mwaka jana na mimi nilichaguliwa kuwa Rais wa taasisi Februari, mwaka huu na iliofika Juni 10, tukapata usajili rasmi na Juni 21, mwaka huu taasisi hii ilizinduliwa rasmi.

Msingi mkubwa au majukumu ya taasisi hii ni kuwa kiungo kati ya serikali ya Jamhuri ya Korea na serikali za nchi za Afrika, sekta binafsi, asasi za kiraia na ili kuwa kiungo muhimu, taasisi hii itakuwa na wajibu wa kufanya utafiti wa mambo mbalimbali ya mataifa ya Kiafrika kwa kupeleka wataalamu mbalimbali ambao watatupa majibu ya nini kifanyike katika kuiunganisha Jamhuri ya Korea na mataifa ya Afrika kwa faida za pande zote.

Afrika kama mbia muhimu wa maendeleo kwa Jamhuri ya Korea, mwezi uliopita ilisherehekea Siku ya Afrika ambapo shughuli mbalimbali ikiwemo semina za kibiashara zilifanyika na mataifa ya Afrika yaliwakilishwa ipasavyo na ilikuwa fursa muhimu kwa pande zote kuweza kubadilishana uzoefu wa kibiashara baina yao. SWALI: Ni kwa nini taasisi hii imeanzishwa sasa na sio wakati mwingine wowote kabla? JIBU: Hivi sasa Afrika ni tegemeo kubwa katika uchumi wa Jamhuri ya Korea.

Mimi binafsi na Taifa la Korea tunafahamu umuhimu wa Bara la Afrika katika kuibua fursa za kiuchumi. Kwa bahati nzuri katika utumishi wangu serikalini nimewahi kuwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Afrika Kusini nikizisimamia pia nchi za jirani kama Botswana, Lesotho na Madagascar na nyinginezo ambapo nilijifunza mengi kuhusu Afrika na watu wa Afrika. Afrika inajitahidi kukuza uchumi kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na zipo nchi ambazo zimeanza kupata mafanikio chanya. Afrika inakuja juu, inapata maendeleo katika utawala bora, ukuaji wa uchumi, maendeleo ya kilimo, afya, elimu na maendeleo ya watu wake.

Ni kwa kutambua hilo, ndio maana kama Taifa tumeona wakati ni sasa, na tumechukua hatua kwa kuanzishwa kwa taasisi hii muhimu. SWALI: Ni upi mwelekeo wa taasisi katika kipindi hiki kifupi tangu kuanzishwa kwake? JIBU: Mwelekeo ni mzuri sana. Jamhuri ya Korea na hata mataifa ya Afrika wamekuwa na matumaini makubwa na taasisi kuliko hata tulivyotazamia na hili linaweza kuwa limegeuka kuwa changamoto kubwa kwa taasisi na sisi tuliokabidhiwa kazi kusimamia taasisi yenyewe.

Yapo matukio ambayo tayari yamefanyika na tumetumia fursa hizo kukutana na wawakilishi kutoka mataifa ya Afrika, ipo mikutano iliyoandaliwa na taasisi za kifedha, lakini pia ipo mikutano ya kiserikali imefanyika ukiwemo ule nilioutaja mwanzo wa Siku ya Afrika ambayo tuliisherehekea Julai 11, mwaka huu chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea. Kupitia fursa hii tumeweza kueleza nia na madhumuni ya taasisi yetu na kupitia fursa hizo tumeweza kuwa na semina za kibiashara na kiuchumi ambapo wawakilishi wa pande husika wamepata nafasi ya kujadiliana pamoja hatua za kuchukuliwa kuelekea mafanikio ya pamoja.

Mfano mzuri ni nchi unayotoka, Tanzania ambapo mwakilishi wake, Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mwanamani Kidaya alielezea Serikali ya Tanzania inavyochukua hatua madhubuti katika kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika kufikia lengo la Serikali ya Tanzania kuwa na Uchumi wa Viwanda na alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Korea kufika Tanzania kwa uwekezaji. Katibu Mkuu pia alielezea mikakati mingine ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kama chachu ya kuboresha miundombinu ya reli ambayo ni muhimu katika kufanikisha uchumi wa viwanda na kwa namna hiyo amefungua njia kwa wawekezaji wa Korea kufika Tanzania.

Na huko nyuma tumewahi kuwa na kongamano baina ya vijana wa Afrika na wa Jamhuri ya Korea. Na kupitia fursa hiyo, vijana wasomi kutoka vyuo vikuu walikutana pamoja na eneo ambalo tulilipa msukumo mkubwa lilikuwa la matumizi ya sayansi katika kukuza uchumi. Moja ya mikakati ya taasisi hii itakuwa ni kuhamasisha vijana wa Afrika waliopo Jamhuri ya Korea kushiriki programu za sayansi zinazofundishwa na vyuo vikuu vya Korea ili kukuza uwezo wao wa kisayansi.

Kazi nyingine itakuwa ni kuwapeleka wataalamu wa Korea katika mataifa ya Afrika kukuza ujuzi na hasa katika utaalamu wa kada ya kati ambao ni muhimu zaidi katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa mataifa machanga ya bara la Afrika. SWALI: Ni yapi maoni yako binafsi na taasisi yako kuhusu uhusiano wa Jamhuri ya Korea na Tanzania? JIBU: Uhusiano wa pande hizo mbili ni mzuri sana kwa sababu unajengwa na misingi ya kihistoria. Zipo hatua mbalimbali ambazo tayari zimeshaanza kuchukuliwa baina ya mataifa hayo mawili kuimarisha zaidi uhusiano wao katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Jamhuri ya Korea inatekeleza malengo yake ya kukuza ushirikiano na Tanzania kupitia mashirika yake ya kimataifa ya maendeleo ya KOICA na EDCF ambayo sisi tunayachukulia kama kiungo muhimu kufanikisha malengo ya kukuza zaidi ushirikiano wetu na Tanzania. Naiona Tanzania yenye nafasi kubwa zaidi kwa mataifa ya Afrika katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii na Jamhuri ya Korea. Kama nilivyosema awali, uhusiano wetu haujaanza leo, unabebwa na misingi ya kihistoria.

Kama unavyofahamu, baada ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili mwaka 1992, Jamhuri ya Korea ilifungua Ubalozi Tanzania mwaka huo huo. Mwaka 1998, Rais wa Tanzania wakati huo (Benjamin Mkapa) alitembelea Korea na mwaka 2013 Spika wa Korea (bila kumtaja) alitembelea Tanzania. Katika mwendelezo huo, mwaka jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania (Balozi Augustine Mahiga) naye alifika hapa (Korea). Januari mwaka huu, Tanzania ilifungua rasmi ubalozi wake hapa Jamhuri ya Korea na zaidi ya hapo hivi karibuni Waziri Mkuu wetu, (Lee Nak-yon) alikuwa Tanzania kama njia ya kukuza ushirikiano wa kindugu na kiuchumi na mawaziri wetu wengi tu wamefika Tanzania.

Hizi ni hatua madhubuti na za kimkakati katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili. Kupitia uhusiano wa kimataifa mataifa haya mawili yapo vizuri sana lakini pia kiuchumi tuna ushirikiano mzuri sana. Takwimu zinaonesha hadi mwaka huu karibu Dola za Marekani milioni 200 zimewekezwa na Jamhuri ya Korea katika biashara nchini Tanzania. Lakini kwa upande wa kusaidia maendeleo ya jamii, Jamhuri ya Korea haipo nyuma kwani zaidi ya Dola za Marekani milioni 414 zimetumika katika kusaidia kuboresha afya, elimu na miundombinu mbalimbali. Tanzania pia inatumia soko la Korea kukuza biashara, kwa mfano kahawa maarufu hapa Korea inatoka Tanzania.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha ripoti ...

foto
Mwandishi: Oscar Mbuza

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi