loader
Picha

Mchango wa SADC, AU muhimu kujenga Zimbabwe mpya

HATIMAYE Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo baada ya kushinda uchaguzi mkuu. Rais Mnangagwa maarufu ED au Mamba nchini humo, aliapishwa na Jaji Mkuu wa Zimbabwe, Luke Malaba katika uwanja wa michezo wa Taifa katika sherehe iliyohudhuriwa na viongozi wa nchi kadhaa za Afrika, ikiwemo Tanzania. Rais John Magufuli aliwakilishwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete; Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula na Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha UDP, John Cheyo.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Paul Kagame wa Rwanda ambaye ni Mwenyekiti wa AU na mabalozi wa nchi za Ulaya na Afrika. Aliapishwa baada ya Mahakama ya Katiba (Concourt) Zimbabwe kutupa pingamizi la Nelson Chamisa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha MDC. Jaji Malaba akisaidiwa na wenzake wanane, kwa pamoja walitupa hoja za Chamisa kwa kukosa ushahidi wenye mashiko kuishawishi kufuta matokeo yaliyompa ushindi Mnangagwa.

“Wanasheria hawako hapa ili kushinda kesi. Hawa ni maofisa wa Mahakama wanaotakiwa kuisaidia Korti kuamua nani mwenye haki kati ya anayelalamika na anayelalamikiwa. Kwa ushahidi uliotolewa (na upande wa upinzani), hatuwezi kutengua matokeo ya sauti ya umma iliyoamua kumchagua Mnangagwa,” Jaji Malaba alisema wakati akisoma hukumu yake. Alikuwa akirejea jinsi mawakili wa Chamisa walivyoshindwa kuishawishi mahakama jinsi Mnangagwa na chama chake cha Zanu-PF alivuruga uchaguzi na kupindua matokeo.

Kwamba Mnangagwa ameshaapa kuwa Rais baada ya kesi hiyo kutupwa ikiiacha Zanu-PF ikimdai Chamisa dola milioni 33 za Zimbabwe kama gharama za uchaguzi siyo habari tena. Habari sasa inayogonga vichwa vya raia wa Zimbabwe, Afrika na dunia ni hatma ya nchi hiyo baada ya uchaguzi ukizingatia ushindi mwembamba ambao Rais Mnangagwa alipata. Wachambuzi wa masuala ya siasa, uchumi na diplomasia wanatafakari Zimbabwe mpya itakuwaje chini ya Rais Mnangagwa wakirejea upinzani kutoka kwa Rais wa zamani, Robert Mugabe anayeugulia maumivu ya kuondolewa.

Wanahoji hayo kutokana na ukweli kuwa, bado vumbi la uchaguzi huo halijatulia baada ya Chamisa kuamua kukata rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu Afrika (ACHPR) Arusha kupinga ushindi wa Mnangagwa. Na zaidi, wanahoji hayo kutokana na ukweli kuwa, Marekani, moja ya mataifa makubwa duniani yenye maslahi mapana na Zimbabwe imeonesha kutokubaliana na matokeo hayo na hivyo kujenga picha haitashirikiana na Rais Mnangagwa. Jopo la waangalizi wa uchaguzi wa Marekani lilitoa ripoti iliyokosoa uchaguzi ulivyofanyika hasa baada ya Jeshi kudaiwa kuua watu kadhaa, jambo ambalo ED amesema ataliundia tume.

Taasisi ya Demokrasia ya International Republican Institute and National Democratic Institute ya Marekani imekaririwa ikidai kuwa Zimbabwe inakosa utamaduni wa demokrasia ya “kuvumiliana ya vyama vya siasa kupewa haki sawa na raia kupiga kura kwa uhuru”. Kutokana na maoni ya taasisi hiyo iliyokuwa moja ya waangalizi wa uchaguzi, Marekani imesema vikwazo vya kiuchumi na fedha dhidi ya Rais Mnangagwa na maofisa wengine wa Zanu-PF na mashirika makubwa ya Serikali vitaendelea.

Hatua hiyo inamaanisha Mnangagwa atakuwa na wakati mgumu wa kupata misaada ya Shirika la Kimataifa la F edha (IMF ) ambalo Marekani ina ushawishi mkubwa ingawa Umoja wa Ulaya (EU) umeiondolea nchi hiyo vikwazo. Hata hivyo, tayari Rais Mnangagwa ameonesha nia ya kukwepa kitanzi hicho kwa kutangaza na kusisitiza utayari wake wa kujenga Zimbabwe mpya yenye umoja na mshikamano na ujenzi wa uchumi mpya kwa kushirikisha makundi yote.

Rais Mnangagwa ameripotiwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya Zimbabwe akitumia mtandao wake wa Tweeter na hotuba yake ya kumwomba mpinzani wake, Chamisa ampe ushirikiano waweze kujenga Zimbabwe mpya. “Sisi wote ni Wazimbabwe. Kinachotuunganisha ni kikubwa zaidi kuliko kile kinachoweza kutugawa,” alisema katika hotuba yake wakati akiapishwa ambapo aliwataka Wazimbabwe kuungana bila kujali itikadi za siasa, ukabila wala tofauti za rangi. “Visheni ya Zimbabwe mpya, yenye maendeleo ambayo wote tunataka kuijenga ni ya ushirika, inayovuka mipaka ya tofauti za kisiasa. Kama Rais naahidi kutenda haki, bila woga, wala upendeleo, kama Rais wa Wazimbabwe wote,” alisema Mnangagwa.

Maneno hayo yalikoleza ujumbe wa Tweeter kwa Chamisa aliomtaka mpinzani wake huyo kupokea ‘mikono ya ushirikiano’ anaoutaka kwake katika kuijenga Zimbabwe mpya ijayo. Hata hivyo, Chamisa amedai haoni kama Rais Mnangagwa ana dhamira ya kweli ya hayo anayosema kwani aliwahi kumwandikia barua kumtaka wakutane kuzungumza ana kwa ana kuhusu hatma ya Zimbabwe, hakumjibu na hata viongozi wa SADC hawajamjibu kuhusu hilo. Ni madai hayo yanafanya wachambuzi wa siasa, uchumi, diplomasia waone haja ya jumuiya za kimataifa kama SADC, Umoja wa Afrika, EU, Umoja wa Mataifa (UN) kuchukua hatua haraka kuwasaidia wananchi kujenga Zimbabwe mpya.

Wafanye hivyo wakijua baada ya Rais Mugabe kuondolewa na Rais Mnangagwa kuapishwa, ni muhimu Zimbabwe ikasonga mbele kiuchumi baada ya miaka mingi ya vikwazo vya uchumi na tofauti za kisiasa na mataifa ya magharibi. Jambo la muhimu ni kwamba, Rais Mnangagwa ameonesha nia njema ya kufufua uchumi wao na kupambana na rushwa, ubadhirifu, urasimu na kuzingatia haki za binadamu na hivyo kuna haja ya jumuiya ya kimataifa kumuunga mkono. Ni muhimu jumuiya ya kimataifa kama SADC, AU, EU, UN kumuunga mkono sasa akiwa na uhalali wa kisheria kufuatia kushinda kwake uchaguzi huru na haki kama Mahakama ya Katiba (Concourt) iliyourasimisha kwa sababu, awali alipotwaa madaraka, alipungukiwa hilo.

Kuchelewa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua, kunamaanisha kuruhusu ombwe lichukue nafasi ya kuipeleka Zimbabwe kwenye vurugu za kisiasa za maandamano ya kupinga matokeo. Nionavyo, baada ya Rais Mnangagwa kuapishwa, huu ni wakati mwafaka kwake kufungua ukurasa mpya wa kutekeleza ahadi zake za kushirikiana na wanasiasa wengine na hasa Chamisa aliyeungwa mkono na Mugabe ili apate fursa nzuri ya kujenga uchumi wao. Zimbabwe inadaiwa dola bilioni 2 za Marekani kama mikopo kutoka Benki ya Dunia na taasisi zake. Kazi ya Mnangagwa ni kurekebisha uchumi kwa kuomba misaada na mikopo nafuu kwa mashirika ya kimataifa iliyokwama muda mrefu.

Kwangu mimi, hatua ya Chamisa kukata rufaa Korti ya Haki za Binadamu Afrika (ACHPR) ni kuchelewesha ujenzi wa Zimbabwe mpya kwani kwa kurejea uamuzi wa Councourt, uwezekano wa kutengua matokeo hayo ni mdogo kutokana na uwezo wa ACHR kusikiliza kesi kama hiyo. Nilitazama mwanzo hadi mwisho hukumu ya Jaji Malaba iliporushwa mubashara na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) na kubaini, pamoja na Jaji Malaba kukubaliana naye kuwa Tume ya Uchaguzi Zimbabwe ilikiri kukosea hesabu za baadhi ya kura, ukosefu wa ushahidi dhahiri na upungufu wa hoja zenye mashiko za kisheria ikiwemo kuchelewa kufungua madai, zilitosha kuwanyima ushindi wanaoulilia mno.

Ni kwa msingi huo nadhani badala ya jumuiya ya kimataifa, SADC, AU kusubiri wafuasi wa Chamisa waandamane kudai haki kwa njia mbadala, inapaswa kuwakutanisha Chamisa na Rais Mnangagwa kwa njia za kidiplomasia ili kufikia mwafaka kushirikiana kuendesha nchi. Uzuri Rais Mnangagwa ameonesha yuko tayari kwa hilo na Chamisa anachohoji ni kitu kidogo tu, dhamira ya kweli ya Rais huyo kuhusu hilo hivyo jumuiya ya kimataifa ikimsihi, atakubali. Tayari ameonesha dhamira safi ya kufanya hivyo kwa kuteua tume ya kuchunguza mauaji ya wananchi wakati wa kampeni ambapo Mkuu wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali mstaafu Davis Mwamunyange ni mjumbe wa tume hiyo.

Kwa kurejea matokeo ya uchaguzi nyuma, ukweli unabaki kuwa hata wakati wa Mugabe na aliyekuwa Kiongozi wa MDC, Morgan Tsvangirai, kushindwa kwa kishindo ni ndoto. Ni wazi, hata Chamisa akienda ACHPR, bado uchaguzi unaweza kuleta matokeo kama hayo na hivyo atahitaji ushirikiano wa wanasiasa wengine kuijenga Zimbabwe mpya waitakayo. Ni vyema akasikiliza sauti za upatanishi wa wanadiplomasia kama mabalozi wa nchi za nje ikiwemo EU wanaotaka serikali ya umoja wa kitaifa kwani hata viongozi wenzake wa MDC wanaripotiwa kuhofia nguvu ya jeshi wakiamua kuandamana kama suluhisho la mgogoro wao.

Nionavyo, hatua ya Mugabe kumtumia Rais Mnangagwa salamu za pongezi, kuwakilishwa na binti yake katika sherehe zake ni ishara ya kupungua kwa joto la tofauti zao na hivyo ni rahisi jumuiya ya kimataifa kuwapatanisha tena. Ni matarajio yangu SADC ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Rais John Magufuli itachukua hatua. Pengine kutumwa kwa Rais Kikwete ambaye Mugabe anamkubali ni mwanzo tu. Rais Kikwete akiwa Mwenyekiti wa AU ndiye aliyezima kelele za Magharibi kutaka Mugabe aondolewe alipoenda Zimbabwe na kusema Afrika iachwe iamue mambo yake yenyewe.

ROSEMARY Dickson ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi