loader
Picha

Mambo yote Ligi Kuu Bara

BAADA ya kusimama kwa siku kadhaa kupisha mechi za kimataifa, Ligi Kuu Tanzania Bara inarejea tena mwishoni mwa wiki hii huku kila timu ikiwa na moto wa kutaka kushinda. Ligi ilisimama kuipisha timu ya taifa, Taifa Stars iliyocheza na Uganda mechi ya kuwania kufuzu fainali za kombe la Mataifa Afrika, Afcon 2019, mechi iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Kampala na kumalizika kwa suluhu.

Timu zote 20 zipo kwenye maandalizi kabambe kuhakikisha zinafanya vizuri kwenye mechi hizo ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi. Washindi wa pili msimu uliopita, Azam wataendelea na kampeni zao Ijumaa wakiwa ugenini kucheza na Mwadui FC ya Shinyanga saa nane mchana huku kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, African Lyon ikiwaalika Wagosi wa Kaya, Coastal Union kutoka Tanga.

Azam inaingia uwanjani na nguvu mpya baada ya kurejea kwa mshambuliaji wake mpya Donald Ngoma iliyomsajili msimu huu kutokea Yanga. Ngoma hajaonekana uwanjani muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, lakini sasa anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi takriban wiki mbili zilizopita. Jumamosi, mabingwa watetezi Simba watakuwa ugenini uwanja wa Nagwanda Sijaona Mtwara kumenyana na Ndanda iliyoahidi kupindua meza na kufuta uteja wa kufungwa na Simba mara nyingi. Siku hiyohiyo, Prisons itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.

Mechi nyingine siku hiyo ni kati ya Mbao watakaokuwa nyumbani kwenye uwanja wa CCM Kirumba kuikaribisha JKT Tanzania huku KMC ikiwaalika Singida United kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Lipuli FC itakuwa nyumbani uwanja wa Samora Iringa kuwakabili Mtibwa Sugar na mechi ya mwisho siku hiyo itakuwa Mara ambako wenyeji Biashara watakwaana na Kagera Sugar.

Jumapili ya Septemba 16 kutakuwa na mechi mbili, mabingwa wa zamani Yanga wakiwa nyumbani Uwanja wa Taifa kuwaalika Stand United ya Shinyanga na kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya wenyeji Mbeya City watacheza mechi yao ya kwanza nyumbani msimu huu dhidi ya Alliance ya Mwanza. Mpaka sasa Mbao FC, ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa wamejikusanyia pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na sare moja huku Azam FC wakiwa nafasi ya pili na pointi zao sita sawa na mabingwa watetezi Simba waliopo nafasi ya tatu.

Yanga wapo nafasi ya 10, baada ya kucheza mechi moja na kuchukua pointi zote tatu dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa ufunguzi. Na timu za Mwadui FC na Mbeya City zinaburuza mkia zikiwa hazina pointi, City wakipoteza michezo yote mitatu wakati Mwadui michezo miwili. Kiujumla timu tatu zinazoshika nafasi za juu zimeonekana kufanya vizuri kwenye mechi za awali hasa Azam FC ambao mpaka sasa katika mechi mbili wamefunga mabao matano huku wakiwa hawajaruhusu nyavu zao kutikishwa.

Wanafuatiwa na Simba ambao wamefunga mabao matatu yote yakifungwa na mshambuliaji wake nyota Meddie Kagere na wao hawajaruhusu nyavu zao kutikiswa wakati vinara Mbao FC wao wameruhusu bao moja na kufunga mabao matatu kwenye mechi zao tatu walizocheza. Simba, Yanga na Lyon zilitumia mapumziko kujiweka sawa kwa kucheza mechi za kirafiki ambapo Simba ilicheza dhidi ya AFC Leopard ya Kenya na kushinda mabao 4-2 huku Yanga ikijipima na Lyon na kushinda bao 1-0.

WAKATI Klabu ya Simba wakidhamiria kumpeleka mwanachama wa timu hiyo ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi