loader
Picha

Zuio la kucha, kope bandia lawagawa wabunge

KUCHA na kope za bandia wanazobandika wanawake zimewagawa wabunge, hata hivyo wengi wao wamesema kubandika huko ni kumfundisha Mungu namna ya kuumba na kukosoa uumbaji wake. Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana, wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama vyao walisema, wanawake wanatakiwa kuheshimu uumbaji wa Mungu na kuacha kukosoa uumbaji wake.

Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vullu (CCM) alisema kuweka kope na kucha za bandia ni kumfundisha Mungu namna ya kuumba binadamu. “Kucha, kope pamoja na mavazi yanatakiwa kuwa yale yanayompa heshima Mbunge,” alisema. Alisema wanawake wanajichubua na kupaka mikorogo, kiimani wanajiharibia miili na afya yao, waliotengeneza wanataka kuleta athari kwa binadamu wenzao. Vullu alisema wabunge ni kioo cha jamii, chochote kinachofanywa nao kinaigwa na jamii, hivyo matendo na tabia zao zinatakiwa kuwa za mfano kwa jamii ili kuiga.

“Mbunge ni kioo anatakiwa kuwa katika hali nadhifu ili jamii ijifunze kutokana na mwonekano na uwepo wake, kwa kuweka kope za bandia na kucha ataelekezaje jamii?” alihoji. Mbunge Vullu alisema, kuhusu Spika Job Ndugai kutamka hivyo, ni haki yake na kwa mamlaka yake anaweza kukemea chochote na yeye anaunga mkono tamko hilo la kupiga marufuku kuweka kope na kucha za bandia. Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema kanuni za Bunge zinasema kuhusu mavazi, wala hazisemi lolote kuhusu kucha na kope za macho za kubandika.

Alisema kupaka kucha bandia na kope ni uhuru wa mtu na wala Bunge halitaweza kudhibiti watu wanaoingia wakiwa wameweka kope na kucha za bandia. Mbunge wa Mbinga Vijijini (CCM), Martin Msuha alisema Spika alikuwa na haki ya kupiga marufuku kucha na kope za kubandika, akasema walipokuwa Zanzibar kwenye mkutano wa maadili, aliombwa aangalie mavazi ya wabunge wakati wanapokuwa kwenye kamati mbalimbali za Bunge. “Spika aliwataka wenyeviti wa kamati kuangalia mavazi ya wabunge wanapokuwa kwenye kamati yanatakiwa kuwa ya heshima,” alisema.

Alisema Spika hajakosea ni haki yake kwani Mbunge ni mtu anayetakiwa kuonekana mfano bora kwa jamii, hivyo kuweka kucha za bandia na kope za bandia ni kutokuwa na maadili. Mbunge wa Viti Maalumu, Alfredina Kaigi (CUF) alisema Mungu aliwaumba viumbe wake wote wakawa wazuri, kitendo cha kuweka kucha na kope za bandia ni kukosoa uumbaji wa Mungu. Alisema mbunge ni kioo cha jamii, hivyo kitendo cha kujichubua ni aibu kwani unakuwa unaharibu ngozi ya asili ambayo inatambulisha Uafrika. Kaigi alisema kitendo cha Spika Ndugai kupiga marufuku hajakosea, kwani wabunge wanatakiwa kuonekana mfano wa kuigwa na jamii, badala ya kuharibu ngozi yao.

Mbunge wa Hanang, Dk Mary Nagu (CCM) alisema; “Kwa nini kubandika kucha na kupe wakati Mungu alikuumba vizuri. Kitendo cha kujichubua wakati ngozi ya asili ni njema inaonekana unataka kurekebisha uumbaji wa Mungu. “Wanawake wanatakiwa kutunza ngozi ya asili ambayo inatambulisha Uafrika wake, kwani ngozi ya asili ni nzuri na inatakiwa kutunzwa badala ya kuichubua,” alisema. Hata hivyo, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) alisema kope na kucha pamoja na kupaka wanja siku hizi vitu hivyo vinafanyika kitaaluma zaidi kwa kupaka unga katika kucha na zinakuwa ngumu, hivyo kitendo cha kuwakata kubandika ni udhalilishaji wanawake.

“Spika alitakiwa pia kuzungumza kuhusu wabunge wanaume ambao wamekuwa wakivuta sigara kupita kiasi pamoja na kulewa, kwani nao wanakuwa wamekosea,” alisema. Mbunge wa Kilwa Kusini, Vedasto Ngombale (CUF) alisema; “Kubandika kope na kucha kunakiuka utamaduni wetu, ni mapambo yaliyopitiliza kuliko mapambo ya kawaida ambayo mwanamke anaweza kujipamba.” Mbunge wa Viti Maalumu, Joyce Sokombi (Chadema), alisema wabunge wanatakiwa kujitambua kwani ni viongozi wa mfano, hivyo wanatakiwa kufuata maadili ya Bunge na kuachana na kitendo cha kumkosoa Mungu katika uumbaji wake.

WANAFUNZI wa kidato cha sita waliopo katika kambi maalum ya ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi