loader
Picha

Kofi Annan kuzikwa kesho Accra

KESHO dunia na Afrika itashuhudia maziko ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan (80) aliyefariki dunia hivi karibuni. Kofi Annan anatarajiwa kuzikwa katika kaburi jipya maalumu la kijeshi katika mji mkuu wa Ghana, Accra, nchi aliyozaliwa. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga alisema jana kuwa kiongozi huyo atakumbukwa daima. Akizungumza na HabariLeo kuhusu kiongozi huyo shujaa na mwenye kuheshimika duniani kwa uongozi wake, Waziri Mahiga alisema Kofi atakumbukwa kwa utendaji kazi mzuri.

“Kiongozi huyu anapumzishwa keshokutwa (kesho). Daima atakumbukwa kwa uwezo wa kiutendaji. Alikuwa mchapakazi aliyeboresha amani katika Umoja wa Mataifa (UN),” alisema. Alisema Annan atakumbukwa kwa mengi na zaidi mawazo yake ya kimageuzi ndani ya UN, kukifanya chombo hicho kiwe na wajibu zaidi ya kulinda amani kwa kuhakikisha inaondoa au kuzuia vitu vinavyozorotesha amani duniani kote ambavyo ni pamoja na umasikini na njaa. Waziri Mahiga alisema mbali na mtazamo wake huo wa kimageuzi uliokubalika UN, Kofi pia alileta dhana nyingine vita ya Iraki ambapo majeshi ya Marekani yalishiriki bila ruhusa ya UN.

“Annan baada ya ile vita ya Iraki alionya taifa kubwa kuamua jambo bila kushirikisha mataifa mengine ndani ya UN ni vibaya,” alisema. Mbali na mawazo hayo ya kimageuzi, Balozi Mahiga alisema anamkumbuka Kofi kama mtu aliyemwita alipokuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kumwomba aishawishi Tanzania kushiriki kulinda amani. “Nikiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Kofi aliniita wakati huo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ulinzi wa Amani UN kabla hajawa Katibu Mkuu na akaniomba niishawishi nchi yangu, Tanzania kushiriki kwenye majeshi ya ulinzi wa amani kwa alichodai tuna sifa nzuri,” alisema Mahiga.

Alisema, kuanzia wakati huo, Tanzania ilianza kupeleka askari wake kulinda amani kwenye majeshi ya UN na walianza kwa kupeleka askari Lebanon na kisha nchi nyingine ambapo hadi leo ushiriki wa nchi umekuwa na sifa nzuri. Mapema jana, mwili wa Kofi Annan uliwasili Ghana, nchi aliyozaliwa tayari kwa maziko yatakayofanyika kesho mjini Accra. Kofi alifariki dunia Agosti 18, mwaka huu baada ya kuugua kwa muda mfupi na kifo chake kimeacha simanzi duniani, hasa kwa kuwa alikuwa miongoni mwa viongozi wachache duniani walioheshimika kwa uongozi wao.

Mwili wake ulisafirishwa kutoka Geneva, Uswisi kurejea Ghana, jeneza lake likifunikwa bendera ya umoja huo na ulisindikizwa na mkewe, Nane-Maria Annan, watoto wake na maofisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa. Kofi Annan, mwanadiplomasia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alikuwa kiongozi wa kwanza wa UN kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika aliyetumikia UN miaka 10. Baada ya mwili wake kuwasili Ghana, Rais wa nchi hiyo, Nana Akufo-Addo alikuwa miongoni mwa viongozi waliompokea, na viongozi wa jadi, viongozi wa kidini, viongozi wakuu wa kijeshi na wanasiasa mbalimbali nchini humo.

Baada ya ndege kutua na viongozi kumpokea, askari sita wa jeshi la nchi hiyo walikwenda kubeba jeneza lake na bendera kubadilishwa kutoka ya UN na kuwekwa bendera ya taifa. Jana wananchi wa nchi hiyo walianza kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo na kesho viongozi mbalimbali kutoka kila pembe za dunia watawasili nchini hapo kutoa salamu na heshima zao na kuhudhuria maziko hayo. Tangu alipostaafu, Kofi alikuwa anaishi Uswisi na atazikwa katika kaburi jipya la kijeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Accra.

Baada ya tangazo la kifo cha Annan, serikali ya Ghana ilitangaza wiki moja ya maombolezo ya kitaifa, bendera zikipeperushwa nusu mlingoti. Viongozi mbalimbali wa Afrika akiwemo Rais Uhuru Kenyatta wametuma uwakilishi kwenye maziko hayo yatakayohudhuriwa na kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga.

Akimzungumzia Kofi, Rais Uhuru alisema ni kiongozi shujaa na msuluhishi wa mgogoro ulioibuka nchini humo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 na kusababisha mauaji. Wengine waliothibitisha kushiriki maziko hayo ni Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Ivory Coast, George Weah, Rais wa Namibia, Hage Geingob na Rais wa Niger, Mahamadou Issoufou. Viongozi wa mataifa ya nje ya Afrika ambao hadi sasa wamethibitisha kushiriki ni marais wastaafu wa Uswisi, Ujerumani na Finland.

WANAFUNZI wa kidato cha sita waliopo katika kambi maalum ya ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi