loader
Picha

Watoto ombaomba, wazazi kushitakiwa

Serikali imeagiza watoto wanaoomba mitaani na wazazi wao wakamatwe na washitakiwe mahakamani.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Joseph Kakunda amesema bungeni jijini Dodoma kuwa ombaomba wanasababisha watoto kukosa fursa ya kusoma shuleni au kuwa watoro.

"Omba wengi wamekuwa wanatumia watoto ambao wanatakiwa kuwa shuleni na wanazagaa ovyo mitaani ndiyo maana nikatoa wito kwamba sasa sheria ile ya elimu ya msingi na kanuni ya adhabu itumike kikamilifu katika kuhakikisha kwamba watoto kwanza wote warudishwe shuleni na vilevile wazazi ambao hawatekelezi wajibu wao nao vivlevile wachukuliwe hatua za kisheria" amesema.

"Naagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri chini ya usimamizi wa wakuu wa mikoa kupitia kamati za ulinzi na usalama kuwakamata watoto wote ambao badala ya kwenda shuleni huzagaa mitaani wakiombaomba...

"Wakamatwe wote pamoja na wazazi wao na washitakiwe mahakamani chini ya sheria ya elimu ya mwaka 1978 inayokataza utoro na sheria ya kanuni za adhabu kifungu cha 166, 167, na 169 (a) vinavyohusu wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto" amesema Kakunda.

Amesema hatua za kuwakamata na kuwarudisha makwao zinaonekana haisaidii sana hivyo mabaraza ya madiwani yanaweza kutunga sheria ndogo za kuzuia utoro na kudhibiti mienendo ya watu kuombaomba.

"Hali ya maisha ni ngumu ni kweli na ndiyo maana nimesema kwamba tutumie hizo fursa lakini kwa kusema uweli fursa ya elimu ya msingi bila malipo ni muhimu sana hiyo tuifuatilie vizuri ili watoto wetu wote ambao wanastahili kuwa shuleni wawe shuleni" amesema Kakunda.

Awali Kakunda alisema, kuna watu wazima wanatumia watoto kuomba na wamekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira jijini Dar es Salaam.

Kwa mujiu wa kiongozi huyo, kuna ombaomba wengi Dar es Salaam kwa sababu kuna vivutio wakiwemo watu wanawapa fedha ikiwa ni sehemu ya ibada.

Amesema, mara kadhaa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imetekeleza hatua za kuwaondoa ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwarudisha makwao lakini wamekuwa wakirudi.

"Mfano, mwezi Septemba 2013 ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa kwao ambapo watoto 33 walirudishwa shuleni. hii inathibitisha kuwa watu wazima wanawatumia watoto kuombaomba" amesema.

Ametoa mwito kwa Watanzania kuzitumia fursa za kupambana na umasikini zilizoandaliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na elimu ya msingi bila malipo, huduma za afya vijijini na uwepo wa sheria ya fedha ya 2018 inayotoa fursa kwa makundi ya uzalishaji mali kupata mikopo wakiwemo walemavu.

"Vilevile watumie uwepo wa ardhi ya kutosha yenye rutuba kama fursa ya kuweza kujitegemea na hivyo kujikomboa dhidi ya kuombaomba"amesema.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na ...

foto
Mwandishi: Basil Msongo, Dodoma

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi