loader
Picha

Masomo ya sayansi ni muhimu kwa wasichana

MWELEKEO mkubwa wa Rais John Magufuli, ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda. Kwa msingi huo, masomo ya sayansi ni muhimu kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali ama wawe wa kike, au wa kiume ili wote washiriki kutumia sayansi kutoa ufumbuzi wa kitaalamu wa changamoto na matatizo mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na uhandisi. Hata hivyo, teknolojia hiyo na sayansi kwa jumla inahitaji watu wabunifu, wenye uthubutu na uelewa mkubwa na hiyo, ndiyo inasababisha kuwapo hitaji kubwa na muhimu la jamii kuwekeza katika mambo hayo. Pamoja na ukweli huo, ushiriki wa wanafunzi wa kike katika masomo ya sayansi bado ni wa kiwango kisichoridhisha kutokana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo zikiwamo za baadhi ya watu kuwakatisha tamaa.

CHANGAMOTO ZENYEWE

Ushiriki hafifu wa wanawake kwenye shughuli yakiwamo masomo ya sayansi unasababishwa na mchango hasi wa mila baguzi na kandamizi katika jamii. Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa kwa kuwahoji walimu, wanafunzi na wadau wa mbalimbali wa masuala ya sayansi umebaini kuwapo kwa vikwazo vya kimila na kimazoea. Imebainika kuwa, changamoto kubwa ni wasichana wenyewe jamii kwa jumla, kuendekeza kasumba ya kuwakatisha tamaa wasichana dhidi ya ushiriki wao katika mambo na masomo ya sayansi. Kwa mujibu wa uchunguzi, baadhi ya wanajamii wanawakatisha tamaa wanafunzi wa kike kuwa masomo ya sayansi ni magumu na yanayohitaji muda na nguvu nyingi ambazo sio rahisi mwanafunzi wa kike kuzimudu.

Mmoja wa waliozungumza anayejitaja kwa jina la Warioba mkazi wa Kitunda wilayani Ilala anasema: “Haya mambo ya sayansi; uinjinia (akimaanisha ufundi), ni mambo ya wanaume; wanawake hawayawezi na watu wanamshangaa… Hivi nyie kwenu ni jambo zuri mtoto wa kike kupanda kwenye mti (nguzo) eti anatengeneza umeme au anajenga nyumba?” Hali hiyo, pia inachangia kuwasukuma wanafunzi wengi wa kike wasio na masimamo, kuyumba na kukimbilia katika masomo ya sanaa ambayo wengi wanadhani ni rahisi.

Mila nyingine zinazopaswa kutazamwa kwa ‘jicho kali’ ili zisizidi kudidimiza mwitikio wa wanafunzi wa kike kujihusisha na masomo ya sayansi katika zama hizo za sayansi na teknolojia, ni pamoja na kuzoeleka kuwa, wasichana wanapaswa kufanya zaidi shughuli za nyumbani kama vile kupika, kuosha vyombo na nyinginezo na hivyo, hukosa muda wa kujisomea na hatimaye, wengi kudhani ni vema wakimbilie katika masomo ya sanaa.

WADAU WA TEHAMA WANENA

Akizungumzia kiundani kuhusu suala hilo pamoja na suluhisho lake lake ili kuwachovchea wanafunzi wa kike kushiriki zaidi kwenye masomo ya sayansi, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika linalosaidia wanafunzi kujiimarisha kwenye masomo ya sayansi, la ‘Apps and Girls’, Carolyne Ekyarisiima, anasema jitihada za ziada zinahitajika kumaliza kasumba hiyo. Anataka mkakati uanzishwe na kupewa msukumo na nguvu zaidi ili kuwavutia zaidi wasichana na kuwafanya wayapende na kushiriki sawia katika masomo ya sayansi.

“Kwa kulitambua hilo,” anasema, Apps and Girls imeanzisha na kutekeleza mradi wa kuwapa mafunzo wanafunzi wa kike tangu wakiwa katika masomo ya sekondari ili kuwavutia katika masomo ya sayansi. Kupitia mradi huu walengwa wanawapatia mafunzo ya sayansi ya kivitendo hasa kwa kutumia tehama. Anasema, hupeleka kompyuta shuleni ambapo hutumia mifumo mbalimbali kuwafundishia wanafunzi mintarafu utengenezaji wa tovuti, kutengeneza roboti pamoja na programu mbalimbali za kiteknolojia. Anasema baada ya kutumia mbinu hiyo kwa muda mrefu na kuleta mafanikio makubwa baada ya kuwafikia wanafunzi zaidi ya 200. Kimsingi, Apps and Girls ikabaini kuwa kuwafundisha wanafunzi pekee haitoshi hivyo ikaamua kuwafikia na walimu.

Anabainisha, walimu kwa kushirikiana na kampuni ya Nlab wamewafikia walimu zaidi ya 150 ambapo 100 wametokea Dar es Salaam na 50 wanaobakia wanatokea Zanzibar huku mkakati wa kuwafikia wa mkoani Dodoma ukiwa unandelea. Walimu hao wanafundishwa kutengeneza programu mbalimbali za kompyuta pamoja na utengenezaji wa mifumo mbalimbali ya kiteknolojia inayowezesha kufanya kazi kwa kompyuta sambamba na kufungua tovuti. Anasema: ”Idadi ya walimu tuliopanga kuwafikia ni 300 ambapo kwa Dar es Salaam ni 200 kisha Dodoma na Zanzibar walimu 50, walimu hao kila mmoja atakuwa na wajibu wa kuwafundisha wanafunzi 20 sasa mwisho wa sikuni wanafunzi 6,000 watanufaika na mafunzo hayo.”

Anaongeza: “Lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwawezesha walimu ambao nao wataenda kupandikiza mbegu ya mapenzi ya masomo ya teknolojia kwa wanafunzi wao na mwisho wa siku tutakuwa na vijana wengi kwenye sekta hii.” Anasema wakishafundishwa, walimu hao wanapewa na ‘flashi’ zenye mafundisho mbalimbali kuhusu teknolojia. Imefahamika kuwa, watazitumia flashi hizo kuwafundishia wanafunzi huku akibainisha kuwapo kwa kompyuta kwenye shule hizo za kuwafundishia wanafunzi hao. Mkurugenzi Mkuu wa DITB, George Mulamula anasema, mafunzo hayo ni muhimu katika kuwaandaa wanafunzi pindi wanapojiunga na elimu ya juu kuwa tayari na uelewa wa matumizi mbalimbali ya kompyuta na hata kujikuta kuwa wataalamu wa masuala ya tehama.

Anasema, katika kuhakikisha wasichana hao wanapenda na kufanya kazi bora zaidi ya kisayansi hasa kwa kuanza kutumia mafunzo hayo kivitendo, DTIB inaendesha mafunzo na kisha kuwafuatilia wanafunzi kwenye shule. Mtaalamu huyo anaona njia bora zaidi ya kuwa na wanasayansi wanawake wazuri, ni kuanza kuwekeza katika elimu bora ya sayansi kivitendo kwa wasichana hao hasa kuwafundisha namna ya kutatua kero za jamii kwa kutumia teknolojia ili wawe msaada kwenye jamii watokazo. Katika kuhakikisha kuwa jinsia ya kike inakuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya sayansi, kampuni ya Vodacom kwa kushirikiana na DITB imeandaa wiki moja ya masomo ya tehama.

Wanafunzi wa Shule za Sekondari za Goba, Makongo Juu, Turiani, Mabibo na Chang’ombe jijini Dar es Salaam, wamenufaika na wiki hiyo ya masomo. Meneja Rasilimali Watu wa Vodacom, Immaculate Mwaluko anabainisha kuwa, wasichana wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazopelekea wasiwe karibu na teknolojia. Anasema: “Wamefundishwa namna ya utenegenezaji wa tovuti pamoja na uandaaji wa programu mbalimbali za kompyuta ikiwa ni mkakati wa kupandikiza mapenzi ya somo la sayansi kwa wasichana hawa.”

MAONI YA WALIMU

Mwalimu wa Sekondari ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, Celestina Liviga, anasema ili wanafunzi wavutiwe kwenye masomo ya sayansi walimu wanapaswa kupewa vifaa vya kufundishia kwa njia ya kidijiti. Anasema, kutokana na maendeleo ya teknolojia, walimu wanapaswa kuwezeshwa katika kuzifahamu mbinu mbalimbali za kiteknolojia ili wazitumie kuwafundishia wanafunzi wao. Anatoa mfano wa kufundisha kwa kutumia projekta na wanafunzi kuona wanachofundishwa moja kwa moja kwenye ubao au kuta za darasa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kijitonyama Kisiwani, Charles Nombo anabainisha uhitaji wa mazingira bora zaidi ya kiutendaji yatakayosaidia walimu kuwafundisha vema zaidi wanafunzi wao. Anatoa mfano uwepo wa mafunzo ya mara kwa mara kwa vitendo kwa wanafunzi katika nyanja za sayansi huku akiwataka wanafunzi wanaopata mafunzo kuwasaidia wenzao na pia, kuyatumia kuleta tija katika jamii na taifa kwa jumla katika zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia.

WANAFUNZI NAO WANENA

Katika mazungumzo na HabariLeo, baadhi ya wanafunzi wa kike wanajikita katika suala la kuwapo kwa vifaa vingi vya kujifunzia masomo hayo. Jania Haule wa Sekondari ya Chang’ombe anasema kwa muda ambao amekuwa akishiriki mafunzo kwenye semina za kuwajengea uwezo wasichana katika mambo ya sayansi, amekutana na mfumo mzuri zaidi wa ufundishaji unaoeleweka. Anasema, ni vema walimu wakatumia projekta kufundisha hasa katika masomo ya sayansi ili kuwavutia wanafunzi wote kuyapenda na kuyashughulikia ipasavyo.

Naye mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kibasila iliyopo wilayani Temeke, Joana Yateri, anawataka wazazi na walezi kuwasaidia wasichana kuyamudu masomo ya sayansi kwa kuwapatia muda zaidi wa kusoma. Kadhalika, anawataka wasichana wenzake kuepuka kukatishwa na kukatishana tamaa kuwa masomo hayo ni magumu kwani kila jambo linahitaji bidii, nidhamu na umakini.

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi