loader
Picha

‘Wanafunzi wanapaswa kujengewa utamaduni wa kulinda mazingira’

TIMU ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inaamini kwamba wanafunzi shuleni wana nafasi kubwa katika kulinda mazingira na hivyo wanapaswa kuanza kujengewa fikra hizo kuanzia sasa. Ni kutokana hilo, LEAT inatoa mwito kwa wanafunzi wa shule za misingi na sekondari kote nchini kujengewa utamaduni wa kushiriki kikamilifu katika kutunza na kulinda mazingira katika maeneo yao ili kukabiliana ipasavyo na mabadiliko ya tabianchi. Akizungumza katika maadhimisho ya siku moja ya kulinda mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, mratibu wa mradi kutoka LEAT, Franklin Masika anasema vijana wana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa ajili ya kuboresha hali ya hewa, afya, uchumi na kusaidia kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.

Maadhimisho hayo yaliyofadhiliwa na shirika la 350. org, yalifanyika katika Shule ya Sekondari Charambe, Mbagala, Dar es Salaam ambapo LEAT kwa kushirikiana na shule ya sekondari Charambe walipanda miche 100 ya aina mbalimbali za miti. Lengo ni kuhamasisha wadau mbalimbali wa mazingira wakiwemo wanafunzi kuendelea na mapambano juu ya shughuli zote zinazoharibu na kuchafua mazingira, hususani matumizi ya nishati ambazo huchangia uzalishaji wa hewa ukaa. Mratibu huyo anasema kwa kiasi kikubwa shughuli za binadamu zimechangia matumizi ya nishati ambazo huchangia hewa ukaa na ukataji miti hovyo.

Sambamba na upandaji miti, LEAT iliwezesha kufanyika kwa mdahalo wa wazi kwa zaidi ya saa moja kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Charambe kuhusu matumizi ya nishati mbadala katika kuboresha uchumi na shughuli za kiuchumi nchini. Mdahalo huo uliongozwa na viongozi wa shule hiyo na kusimamiwa na walimu wao huku ukishuhudiwa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, wananchi wa kata ya Mianzini na wananchi wa Majimatitu.

Ni mdahalo uliowakutanisha wanafunzi kutoka katika vidato mbalimbali kupitia klabu zao za UN-Habitat na ya mazingira. Katika maadhimisho hayo, mratibu huyo alisema LEAT kwa kushirikiana na wadau kutoka kata ya Mianzini, wanafunzi, Manispaa ya Temeke na Taifa kwa ujumla wameamua kuadhimisha siku hiyo ili kujikinga na hali zote zinazoharibu mazingira nchini. “Sisi LEAT pamoja na uongozi wa Shule ya Sekondari Charambe na wa kata ya Mianzini tunaungana na wadau wengine nchini na ulimwenguni kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanatunzwa na kulindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Na kwa maana hiyo, matumizi ya nishati zinazochangia uharibifu lazima yapingwe. “LEAT inafanya tafiti za kisera na kisheria, ushawishi kwa masuala mbalimbali yenye maslahi ya umma kama haya maadhimisho yetu ya leo ambayo yanalenga kutukumbusha wajibu wetu wa kuyatunza mazingira yetu kwa maendeleo endelevu,” aliongeza. Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mianzini, Abdallah Kipende, anasema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuelewa dhana ya mabadiliko ya tabianchi, namna yanavyoathiri na namna bora ya kudhibiti hali hiyo ikiwemo upandaji wa miti. Anasema kuwa matarajio ni kuona hatua stahiki zinachukuliwa.

Akitolea mfano anasema kuwa wanafunzi na wakazi wa Kata ya Mianzini wanaweza kufanya ufuatiliaji na udhibiti juu ya shughuli zinazoharibu mazingira. Anasema LEAT imeanzisha mwendo na sasa kata nzima imepata ari mpya na nguvu mpya ya kuanza kupanda miti katika vyanzo vyote vya maji na maeneo yasiyokuwa na miti. Anawataka wanafunzi wote katika kata ya Mianzini na Manispaa ya Temeke kwa ujumla wawe mabalozi kokote waendako ili kutunza mazingira yaweze kuwasaidia kuleta maendeleo.

“Ndugu washiriki ni matumaini yangu kuwa sisi sote ni wadau wa rasilimali na wapenda maisha, hivyo siku ya leo iwe nafasi ya kujitafakari juu ya namna ya kuboresha maisha yetu ili kuthibiti mabadiliko tabianchi. Pia leo iwe fursa ya kujifunza ulinzi wa railimali za taifa,” anasema. Anawataka wananchi kutambua nafasi zao katika kushiriki na kulinda mazingira pamoja na kujua dhana ya mabadiliko ya tabianchi. Aidha, anawataka wanafunzi kutambua namna sekta ya elimu inavyoweza kutumika kuongeza mwamko kwa wanafunzi na vijana katika kulinda mazingira na misingi ya uwajibikaji katika kulinda taifa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Nawaomba mtambue kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu katika kuhakikisha rasilimali za maliasili zinatumika kutukinga dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” anasema. Akizungumzia mabadiliko ya tabianchi, Diwani Kipande anasema kuwa athari zake zinatisha wakazi wa Tanzania na kuwataka wananchi kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya mikutano ya kimataifa na mikataba kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Kwa mfano, jumuiya ya kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambapo nchi 195 zilikubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba wa kisheria wenye lengo la kupunguza gesi joto duniani. “Hivyo na sisi wakazi wa Mianzini lazima tusimame na dunia kuhakikisha tunafanya kazi kudhibiti mabadiliko ya tabianchi,” anasema.

Hadi leo wananchi wengi duniani wanaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi yanayojitokeza kwa njia kama ongezeko la joto duniani, eneo kupata mvua nyingi kupita kiasi au wakati mwingine kuwa na ukame. Kwa lugha nyingine tabia ya hali ya hewa ya mahala hubadilika kuliko ilivyozoealeka hata wakulima kushidwa kujua ni muda gani wa kuandaa mashamba. Sehemu mbalimbali kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya mimea na hata binadamu kutokana na ongezeko la joto. Jamii zinazotegemea ufugaji nazo zimeathirika na mabadiliko haya kwani chakula cha mifugo yao kimepotea pia. Wakulima nao hukutana na uzalishaji mdogo.

Kwa hali kama hii wadau wote lazima wahakikishe wanafanya kazi na jitihada kubwa katika kulinda mazingira yasizidi kuharibika. Akizungumzia nafasi ya vijana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, diwani huyo anasema vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa lakini kwa bahati mbaya vijana ndiyo kundi linaloongoza kujihusisha na shughuli zinazoharibu mazingira. Kwa mfano, vijana vijijini huongoza kwa kuanzisha mashamba makubwa, kukata miti, kufanya uwindaji haramu, na wakati mwingine kuharibu ikolojia. Vijana pia ndiyo hujihusisha na shughuli za kuuza mkaa unaovunwa holela (kwani kuna uvunaji endelevu wa mkaa), kuvuna magogo na mbao na kisha kusafirisha mazao hayo mijini.

“Kwa kuwa vijana ndiyo kundi linaloongoza kuharibu mazingira basi wanalazimika kulinda mazingira kwa hali na mali. Vijana lazima wawe sehemu ya uwekaji dira ya pamoja na kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Vijana washiriki kwa vitendo kuhakikisha nchi inaongeza jitihada na uwezo wa kuhimili mabadiliko haya,” anasema. Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Charambe, Paul Lorri anawapongeza LEAT kwa kuongeza mwamko wa utunzaji mazingira na kuwataka wanafunzi kujenga tabia ya kujiamini, kujituma na kupenda mazingira kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla. “Watoto hawa wakimaliza elimu yao ya sekondari hapa watakwenda mahali pengine kuendelea na masomo au kufanya kazi.

Tunawaomba wahakikishe wanapeleka elimu hii waliopata leo ili watu wengi zaidi waweze kunufaika,” anasema. Anasema kuwa Shule ya Sekondari ya Charambe itahakikisha inaendelea kupanda miti ili kuendeleza kazi iliyoanzishwa na LEAT. Ofisa Mazingira kutoka katika idara ya mazingira, Manispaa ya Temeke, Fidelis Njire anasema kuwa uchumi wa nchi yoyote hapa duniani unakua kutokana na mazingira yaliyotunzwa na kuhifadhiwa kwa usalama. “Tuwaunge mkono LEAT kwa sababu walichokifanya leo ni hatua ya kutuletea maendeleo maana bila mazingira bora hakuna maendeleo,” anasisitiza.

Katika mdahalo wao siku ya maadhimisho hayo, wanafunzi watatu waliibuka washindi na kukabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo zawadi ya fedha. LEAT ni asasi isiyokuwa ya kiserikali inayofanya shughuli za ulinzi na uhifadhi wa mazingira na rasilimali za maliasili. Ilinzishwa mwaka 1994 baada ya wanasheria waanzilishi kugundua kuwa sheria ni chombo muhimu cha kulinda mazingira na kusismamia vyema raliasili za taifa. Pamoja na mambo mengine, dhima ya LEAT ni kuchangia katika utawala bora wa matumizi na usimamizi endelevu wa mazingira na maliasili kwa maslahi ya Umma, kufanya ushawishi, kufanya tafiti za kimkakati na kuwajengea uwezo wananchi.

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi