loader
Picha

Waitara, Kalanga wafichua siri ya ushindi

WASHINDI katika uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, Mwita Waitara na Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Julius Kalanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameeleza siri ya ushindi wao kuwa ni kukubalika kwa sera za chama hicho kwa asilimia kubwa.

Aidha, wamesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo, unaofanywa kwa kasi na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli umekiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupendwa na wananchi wengi hivi sasa. Waitara ameshinda kwa kura 77,795 sawa na asilimia 89.1, akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Asia Msangi aliyepata kura 8,676 sawa na asilimia 9.95 ya asilimia 29.4 ya wapiga kura waliojitokeza. Naye Kalanga ameibuka mshindi kwa kupata kura 65,714 sawa na asilimia 95, huku mgombea wa Chadema, Yonas Laizer akiambulia kura 3,187 sawa na asilimia 5.

Jana Waitara aliwataka wananchi wake kujiandaa kwa maendeleo makubwa yatakayobadilisha maisha yao. Vyama 14 vilishiriki uchaguzi huo, ambapo mgombea wa kupitia chama cha NRA, Murshid Kabiriga alishika mkia kwa kupata kura sita. Akizungumzia ushindi wake, Waitara alisema ni kutokana na kukubalika kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Magufuli na chama hicho cha CCM, hasa kwa wananchi wanyonge.

Pia alibainisha kuwa ushindi huo, unatokana na imani waliyonayo wananchi wake hao jimboni humo na ndiyo walioamua kumrejesha bungeni kwa ushindi mzuri. Alisema kwa muda aliokuwa mbunge wa jimbo hilo, amekuwa karibu zaidi na changamoto nyingi, zinazowakabili wananchi na kuwa atahakikisha anazitatua zote akiwa ndani ya CCM. Alisema:“Najua kwa sasa nipo kwenye chama kinachomiliki dola hivyo ni ukweli kuwa changamoto zitatatulika kwa haraka na kwa ufanisi zaidi hivyo wananchi wajiandae kupokea maendeleo.

“Nitaanza na miundombinu ya barabara, elimu, ajira na masuala mengine muhimu katika kukuza maisha ya wananchi wangu hawa.” Aliwataka wananchi hao kukumbuka sababu kubwa, iliyomhamisha Chadema kuingia CCM kuwa ni imani aliyonayo kwenye chama hicho katika kutekeleza sera za maendeleo ya wananchi. Aliwataka kushirikiana naye katika kufanikisha adhima hiyo ya kuwaletea maendeleo. Uchaguzi ulikuwa wa haki Mapema jana; Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Jumanne Shauri alisema kuwa uchaguzi ulifanyika kwa haki na kuzingatia kanuni zote, kama zinavyoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Alisema, mazingira ya uchaguzi yalikuwa ya kuridhisha huku akiwashukuru wagombea pamoja na wananchi wa kufanya uchaguzi kwa amani. Aliongeza, idadi ya wapiga kura iliyoandikishwa ni 300,605 huku idadi halisi ya waliojitokeza kupiga kura ni 88,270 na idadi ya kura halali ni 87,224, ambapo zilizokataliwa zilikuwa kura 839. Alisema;”uchaguzi umefanyika vema, mshindi kapatikana wananchi walijitaidi kuwa wastaarabu na kumaliza uchaguzi huo vema Waitara ameshinda kwa kura 77,795”.

Mkazi wa jimbo la Ukonga, Bhoke Juma aliliambia gazeti hili kuwa ana imani Waitara atawaletea maendeleo kwa haraka zaidi, ikilinganishwa na ilivyokuwa awali wakati akiwa mbunge kupitia Chadema. Julai 28, mwaka huu Waitara alihamia CCM akitokea Chadema, kwa kile alichodai kukimbilia maendeleo ya kweli na sera zinazotekelezeka katika kuwaletea wananchi maendeleo. Kalanga kuanza na maji,afya na ardhi Kalanga alipokabidhiwa hati ya ushindi juzi usiku, aliwashukuru wananchi wa Jimbo la Monduli kwa kumpigia kura nyingi, zilizomwezesha kuibuka mshindi wa kiti hicho cha ubunge.

Alisema CCM ilifanya kampeni za kistaarabu na anashukuru Mungu kwa ushindi huo na viongozi wote wa chama, waliomsaidia kupata kura hizo. Lakini, alisisitiza kutatua kero tatu kubwa zinazosumbua jimbo hilo, ambazo ni kero ya maji, migogoro ya ardhi na ukosefu wa vituo vya afya na zahanati. Alisema jimbo hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji na migogoro ya ardhi, hivyo atashirikiana na serikali kutatua kero hizo, ikiwemo kujenga zahanati kwa kila kijiji na vituo vya afya, kupunguza tatizo la kinamama kujifungulia majumbani.

“Namshukuru Rais John Magufuli, nawashukuru wabunge wenzangu, viongozi wa chama na watu mbalimbali walionisaidia kuwa Mbunge hapa na naahidi kuwatumikia wananchi wangu kwa kutatua kero mbalimbali nilizokutana nazo hapa wakati wa kampeni za uchaguzi, niliomba kura kwa ajili ya kuwatumikia na sasa nipo tayari kuwatumikia.” Akitangaza matokeo ya ushindi wa CCM juzi usiku, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Monduli, Stephen Ulaya alisema Kalanga aliibuka mshindi kwa kupata kura 65,714 sawa na asilimia 95 huku mgombea wa Chadema Laizer akiambulia kura 3,187 sawa na asilimia 5.

Aliwataja wagombea wengine, Simon Ngilisho kutoka Demokrasia Makini aliyepata kura 35 sawa na asilimia 0, Francis Ringo (ADA-TADEA) kura 21 sawa na asilimia 0, Omary Kawaga (DP) kura 34 sawa na asilimia 0, Wilfred Mlay (ACT Wazalendo) kura 144 sawa na asilimia 0 , Feruziy Feruziyson (NRA) kura 45 sawa na asilimia 0 na Elizabeth Salewa (AAFB) aliyepata kura 16 sawa na asilimia 0. Baadhi ya wabunge, wapenzi wa CCM na wananchi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, walianza kuimba na kucheza kushangilia ushindi huo.

TIMU ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, imerejea katika fainali ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi