loader
Picha

Kwa nini muhimu Serikali ikafikiria kuijenga Dodoma kimkakati ipendeze

HAYAWI hayawi sasa yamekuwa. Ile ndoto ya miaka zaidi ya 45 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kutaka Dodoma iwe makao makuu ya nchi hatimaye sasa inaendelea kutimia.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni limepitisha muswada wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu rasmi ya nchi. Sheria hiyo sasa inasubiri kutiwa saini na Rais John Magufuli ili ianze kutumika rasmi. Naipongeza Serikali kwa kuhamia Dodoma na pongezi za pekee zimwendee Rais Magufuli kwa kusimama kidete kutimiza ndoto ya Nyerere. Ni matumaini yangu kuwa hatachukua muda kuisaini sheria hiyo ili ianze kutumika rasmi. Rais Magufuli alitangaza nia ya Serikali kuhamia Dodoma alipowahutubia wabunge na ameisisitiza hadi nia hiyo imekamilika.

Kwa mtazamo huo, ni matarajio ya watu wengi kwamba atasaini sheria hiyo haraka kuchagiza mchakato wa serikali na watumishi kuhamia Dodoma. Kwamba mchakato huo unaenda vizuri ni jambo la kufurahisha kwani matamanio ya wengi ni kuifanya makao makuu kuchagiza maendeleo. Enzi zake, Mwalimu Nyerere alilenga kuchagiza maendeleo ya nchi kwa kusogeza huduma za Serikali kwa mikoa ya pembezoni kutokana na Dodoma kuwa katikati ya nchi na hivyo kufikika kirahisi.

Ili kuharakisha kuhamia Dodoma, Rais Magufuli alianza na watendaji wa serikali, mawaziri, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na yeye mwaka huu. Alihamasisha mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini kuhamia huko kwa kuwapa ardhi kubwa ya bure wajenge ofisi zao na tayari ubalozi wa Ujerumani umekuwa wa kwanza kufungua ofisi.

Kutokana na watumishi wengi wa idara na wizara mbalimbali za serikali na viongozi waandamizi kuhamia Dodoma, mji huo umezidiwa na watu na hivyo miundombinu iliyopo kutowatosha ipasavyo. Ili kukidhi mabadiliko yaliyotokana na hatua hiyo, serikali imeongeza miundombinu kusaidia Dodoma kupokea watu wengi zaidi kuliko awali na kuifanya Jiji baada ya kuivunja iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).

Baada ya watumishi wengi kuhamia Dodoma, kumekuwa na uhaba wa nyumba za makazi na za wageni, barabara za kukidhi wingi wa magari yanayopita jijini humo, majengo ya ofisi na ya kibiashara. Hatua hizo ni kujenga barabara mpya za lami, kupanua na kurefusha kiwanja cha ndege cha Dodoma, kupanua hospitali ya mkoa na stendi ya kisasa ya mabasi ya mikoani na daladala.

Nyingine ni Halmashauri ya Jiji Dodoma kupima ardhi kwa ajili ya viwanja vya makazi, ofisi na biashara kwa ajili ya watu binafsi, mashirika, kampuni za biashara na wawekezaji, serikali na taasisi za nje kama ofisi za kibalozi na za dini. Hatua za serikali ya awamu ya tano zinakoleza kazi ya Serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere, ya pili chini ya Ali Hassan Mwinyi, ya tatu chini ya Benjamin Mkapa na ya nne chini ya Jakaya Kikwete zilizoweka miundombinu kadhaa pia.

Miundombinu hiyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Hospitali ya Benjamin Mkapa, makao makuu ya chama tawala, CCM na ukumbi wake mpya wa mikutano, ofisi za wizara, idara za Serikali kama Benki Kuu, Takwimu, Mifuko ya Pensheni kama jengo la LAPF na mingine mingi. Kutokana na Bunge kupitisha sheria, sasa kutakuwa na ongezeko kubwa zaidi la watu na hasa baada ya Rais Magufuli kuhamia rasmi Dodoma.

Hii inatokana na ukweli kuwa, baadhi ya watu walikuwa hawaamini kama kweli itakuwa hivyo kufuatia kuhamia Dodoma kusuasua miaka 45. Kuhamia kwa Rais Magufuli Dodoma kutahitimisha mjadala wa kuhama kwa Serikali kutoka Jijini Dar es Salaam na kufungua ukurasa mpya wa uendeshaji wa Serikali na zaidi fursa mpya pia.

Kutamaanisha mambo yote ya kiserikali sasa yataendeshwa kutoka Dodoma na hivyo wenye shida lazima waende huko na kuzidisha mahitaji ya miundombinu ya makazi, malazi na ofisi. Ndio maana inaongeza miundombinu ya stendi, barabara, huduma za afya, vyanzo vya maji, kiwanja cha ndege cha kimataifa Msalato, cha mchangamano cha michezo na kujenga Ikulu. Miundombinu hiyo ikikamilika, itabadilisha sura na mandhari ya mji wa Dodoma na kuufanya wa kisasa zaidi kulingana na hadhi ya Jiji.

Katika kuhakikisha wananchi, taasisi binafsi na za umma wanashiriki ujenzi wa makazi, ofisi na maeneo ya biashara, Jiji la Dodoma lilipima na kuwauzia viwanja katika maeneo mbalimbali. Watu hao walitakiwa kulipia viwanja hivyo na kujenga na walioshindwa, jana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi aliwatangazia watanyang’anywa na kupewa wengine ili waviendeleze inavyotakiwa.

Hatua ya Mkurugenzi huyo ni nzuri kwa sababu imelenga kuchagiza watu kulipia viwanja. Hata hivyo, kuna jambo ambalo viongozi wa Dodoma wanapaswa kujifunza CDA na Dar es Salaam na kubuni mbinu za kujenga mji bora wa Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi anajua Dar es Salaam ilivyomsumbua katika utatuzi wa migogoro ya ardhi kutokana na ujenzi usio na mpangilio.

Lakini pia, Dar es Salaam iko hivi ilivyo siyo tu kutokana na ujenzi holela, bali ujenzi ambao unafanywa na watu kulingana na vipato vyao na kuchangia utitiri wa majengo ya kila aina. Ni matamanio yangu kuiona Dodoma mpya ambayo si kama Dar es Salaam ambayo utakuta nyumba mbovu zinabomolewa kila leo kupisha majengo ya kisasa baada ya eneo kupanda thamani baada ya kufikiwa na miundombinu.

Natamani kuiona Dodoma inayojengwa kwa mpangilio, nyumba bora na za kisasa katika eneo maalum na kujaa kabla ya kugawa viwanja eneo lingine kuweka uwiano na kupendezesha. Hilo litawezekana Serikali ikianzisha taasisi maalumu ya kujenga nyumba za bei rahisi na kuwauzia wananchi katika eneo moja kwa kuondoa kodi kwenye vifaa vya ujenzi kama mradi maalum wa angalau miaka mitano au 10.

Ni vyema Jiji Dodoma likajua watu kutolipia viwanja haimaanishi hawataki kujenga bali uwezo mdogo wa kifedha unawakwamisha na ndio sababu ya ujenzi holela ulioikumba Dar es Salaam kwa kila mtu kujenga kwa kudunduliza. Itapendeza Dodoma ikifanywa mradi maalumu wa ujenzi utakaohusisha makandarasi wazawa kupewa kazi za kujenga, kutumia Suma JKT na Magereza kwa kuondoa kodi kwenye vifaa na watu kuuziwa nyumba zilizo tayari kwa mikopo ya mabenki na wao kulipa kidogo kidogo zaidi. Kama Ulaya, Marekani watu wanapata makazi kwa kununua nyumba zilizo tayari na kuondoa utitiri wa vijumba vinavyojengwa kwa kila mtu kudunduliza, vipi kwa Dodoma ya karne ya 21?

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi