loader
Picha

Watanzania tushikamane msiba wa MV Nyerere

Watanzania na jumuiya ya kimataifa, wanaendelea kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 163 waliozama maji katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza siku ya Alhamisi, baada ya Kivuko cha MV Nyerere kupinduka karibu na ufukwe wa gati la Ukara.

Kufuatia ajali hiyo, Rais John Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kuwatakia majeruhi wa ajali wapone kwa haraka, huku akiwatia moyo watu wote wanaoendelea na uokoaji na uopoaji miili ya watu waliofariki dunia.

Pia, Rais Magufuli alitangaza maombolezo ya kitaifa ya siku nne, ambapo bendera ya Taifa itapepea nusu mlingoti na kuwataka Watanzania wote wawe watulivu na waendelee kushikamana, kama ilivyo desturi yao.

Aidha, tumeguswa na salamu za Rais Magufuli kwa Taifa, ambapo alisema kwa masikitiko makubwa anawapa pole wananchi wa Ukerewe na Kisiwa cha Ukara na Watanzania wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo.

Huu ni msiba mkubwa kwa taifa letu. Tunaomba Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi marehemu. Rais anawaomba Watanzania wote kwa wakati huu ambapo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wananchi, wanaendelea na uokoaji, wawe watulivu na kuendelea kushirikiana.

Tukio hilo limetusononesha sana, kwani limepoteza nguvu kazi kubwa ya wapendwa wetu, ambao Taifa liliwategemea katika kuendeleza nchi kupitia shughuli mbalimbali walizokuwa wakifanya na hivyo kuacha pengo kwa serikali na familia zao, ndugu, jamaa na marafiki.

Tunakosa maneno ya kutosha, kuonesha masikitiko yetu kuhusu msiba huo, zaidi ya kusema tumehuzunishwa, tumesononeshwa na tumesikitishwa sana na tukio hilo baya. Tunaomba Watanzania wote, tuomboleze kwa pamoja bila tofauti za itikadi zao.

Tunaungana na Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuwataka wananchi washikamane zaidi wakati wakisubiri hatma ya kazi ya uokoaji wa watu walio hai na uopoaji wa maiti hadi mwisho, hasa ukizingatia bado wengine wako hai.

Kitendo cha kuokolewa jana kwa Fundi Mkuu wa Kivuko hicho, Mhandisi Alphonce Augustino Charahani, aliyeishi kwa siku tatu kwenye chumba maalum cha kivuko hicho kilichozama, ni ishara tosha kuwa bado upo uwezekano wa kuokoa maisha ya wahanga wengine wa tukio hilo.

Tunawapongeza wapiga mbizi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vikosi vya Wanamaji Zanzibar, wanaosaidiana na wakazi wa Ukara kwa kazi yao nzuri.

Ni matarajio yetu kuwa wananchi wataendelea kushikamana na kuungana na marafiki zetu wa jumuiya ya kimataifa, waliotutumia salamu za pole, kuomboleza kwa sala na michango. Tukio hilo litufundishe kuzingatia umuhimu wa usalama wa majini.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hayuko ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi