loader
Picha

TSN kuibua fursa Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amesema mkoa huo uko tayari kushirikiana na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ili kuhakikisha kuwa jukwaa la fursa za kibiashara linafanyika mkoani humo haraka iwezekanavyo.

Mwanri aliyasema hayo jana kwenye kikao kilichohudhuriwa na watalaamu wa ofisi yake, wawakilishi kutoka Chama cha Biashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) mkoa na Meneja wa Wakala wa Misitu Kanda ya Magharibi Valentine Msusa mara baada ya kupokea ujumbe kutoka TSN uliongozwa na Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, Tuma Abdallah.

Amesema serikali ya mkoa wa Tabora imekuwa ikifuatilia kwa karibu majukwaa ya fursa za kibiashara yaliyokuwa yakiendeshwa na TSN na kubaini kuwa mkoa wa Tabora unaweza kunufaika kiuchumi kupitia jukwaa hilo.

“Tunahitaji wawekezaji wengi waje mkoani kwetu, reli ya kisasa inapita mkoani kwetu na tayari tutapata huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria kwa sababu hakuna mwekezaji atakayekuja kuwekeza kama hana uhakika wa umeme, maji na usalama wake", amesema.

Aliongeza kuwa mkoa wake uko tayari kupokea fursa hiyo ya jukwaa la biashara ambalo litaleta mageuzi ya kiuchumi mkoani kwake.

Alimuelekeza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Msalika Makungu kuhakikisha timu ya mkoa iliyoundwa kwa ajili ya maandalizi ya jukwaa hilo iwe inawasiliana na timu ya TSN ili kuhakikisha kuwa mambo yote muhimu yanafanyika kwa wakati uliopangwa.

Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN Tuma Abdallah amesema, licha ya kushukuru kwa mapokezi mazuri, alisema TSN imekwishafanya majukwaa saba kwa mikoa ya Arusha, Tanga, Simiyu, Mwanza, Geita na Zanzibar.

Alieleza kuwa lengo la kufanya majukwaa hayo ni kusaidia maendeleo ya mkoa husika kwa kuibua vivutio vingi vilivyopo kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kwenda kuwekeza.

"Tunavitumia vyombo vyetu vya habari vya magazeti na vile vya mitandaoni kuanika fursa hizo kwa dunia nzima ambapo zitatoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje kwenda kuwekeza kwenye mikoa hiyo", amesema.

Alisema kwa jukwaa la kibiashara lililofanyika mkoani Geita tayari limeshazaa matunda ambapo mkoa umepokea maombi ya wawekezaji wawili mmoja akitokea nchini Uganda kwa ajili ya kuwekeza mkoani humo.

"Kupitia jukwaa litakalofanyika hapa, tutaibua fursa za mkoa wa Tabora na katika kufanya majukwaa haya hatuko peke yetu, tunatembea na taasisi za fedha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambazo hushirikiana nazo katika kutatua changamoto zinazojitokeza kutoka kwa wadau siku ya jukwaa kwenye mkoa husika,"amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Misitu Kanda ya Magharibi, Valentine Msusa alisema ujio wa jukwaa la biashara la TSN kwa mkoa wa Tabora litatoa fursa kutangazwa kwa rasilimali adimu za miti ya asili na asali zilizoko mkoani Tabora.

Mtendaji Mkuu wa TCCIA, David Mtinya amesema ujio wa TSN kwa mkoa wa Tabora utawezesha fursa na vivutio vingi vya utalii vilivyoko kufahamika vyema na kukuza uchumi wa mkoa huo.

Rais John Magufuli amewakaribisha wananchi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya ...

foto
Mwandishi: Nashon Kennedy, Tabora

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi