loader
Picha

Kampuni yapongezwa kuchangia uchumi

SERIKALI imepongeza kampuni ya Universal Leaf Corporation yenye makao makuu yake Marekani kupitia kampuni zake tanzu mbili kwa mchango wake kiuchumi, ikiwamo kuchangia hazina pamoja na kuajiri Watanzania wengi.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe alieleza kufurahishwa na kampuni hiyo yenye makao yake makuu Marekani kupitia kampuni zake tanzu za hapa nchini ambazo ni Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) na Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL).

Amesema hayo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 100 ya kampuni hiyo mama; miaka 50 ya TLTC na 21 ya TTPL tangu kuanzishwa.

Dk Kebwe alisema serikali inafurahisha kusikia kampuni hiyo ina wafanyakazi zaidi ya 587 walioajiriwa katika mikataba ya kudumu, na zaidi ya 2,000 wakiwa katika mikataba ya muda maalumu.

Aidha, aliipongeza TLTC kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa na kufufua kiwanda ambacho kilikuwa kinaelekea kufa baada ya ubinafsishaji.

“Sisi serikali tunaipongeza menejimenti ya TLTC na TTPL kwa kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kampuni zenu zinachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, hivi vikiwa ni miongoni mwa viwanda 16 vilivyojengwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hapa mkoani Morogoro, kwa nia ya kuifanya Morogoro kuwa kitovu cha viwanda na vilibinafsishwa wakati wa ubinafsishaji.

“Na ni miongoni mwa viwanda vichache vinavyofanya vizuri na kuchangia kiasi kikubwa katika uchumi na maendeleo ya kijamii ya nchi yetu,” amesema Dk Kebwe.

Dk Kebwe pia ameiomba Menejimenti ya TLTC na TTPL kuona namna nzuri ya kutumia reli kwa ajili ya usafirishaji wa mazao kutoka mikoani hadi Morogoro na kisha katika bandari ya Dar es Salaam, akisema reli hiyo ina gharama nafuu kuliko kutumia barabara.

Amesema kwa kufanya hivyo wataunga mkono serikali katika azma yake ya kufufua reli ikiwamo kujenga reli mpya. Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo pia alizipongeza kampuni hizo kwa kutoa fursa ya ajira kwa watu wa wilaya yake na kuahidi kuwaunga mkono.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hizo mbili, Rory Micklem alisema wanayo furaha kuendelea kufanya kazi na serikali kuleta maendeleo ya nchi.

Aliunga mkono ushirikiano kutoka serikalini, akisema wameisaidia kufikia mafanikio katika kufanya biashara nchini Tanzania kwa miaka 50.

Wakati wa sherehe hizo, kampuni na wafanyakazi wake walitembelea maeneo mbalimbali Morogoro Mjini ikiwamo soko, hospitali na shule mbali mbali na kufanya shughuli za usafi.

Wafanyakazi na wageni walipanda miti ya matunda kwa nia ya kuwa na hifadhi ya misitu kwa kizazi kijacho.

Pia kampuni iliwazawadia wafanyakazi wake 21 wa muda mrefu walioitumikia kuanzia miaka 10, 15 na 20. Aidha, kulikuwa na ngoma za kiutamaduni na michezo mbalimbali.

Rais John Magufuli amewakaribisha wananchi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi