loader
Picha

Watendaji wajibikeni msisubiri maagizo

KUNA tabia inaota mizizi na kushamiri nchini ambayo kama isipopigwa vita, shida kubwa inaweza kulikumba taifa hili, shida ya ugoigoi wa utatuaji wa matatizo ya wananchi.

Wakati taifa hili linapiga mbio kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda, kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kufanywa na watendaji ngazi za chini ili wananchi waweze kuwa sawa.

Aidha michango ya watendaji katika kukabiliana na viunzi mbalimbali vya maisha kwa wananchi walio wengi wanyonge ni muhimu kama taifa hili litaendelea kutaka kusonga mbele kushawishi maisha ya wananchi wake kupitia kauli mbiu ya hapa kazi tu.

Ukiangalia vyombo vya habari na ukasikiliza taarifa mbalimbali utabaini kwamba imekuwa ni kawaida kwa watendaji kuketi katika ofisi zao, kuendelea na maisha kama kawaida wakati kuna shida zinawakabili wananchi na zinatakiwa kutatuliwa.

Kutokana na tabia hiyo kushamiri imekuwa ni kawaida kwa sasa ziara za viongozi wakuu wa serikali kama Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu kupokewa na mabango yanayoeleza dhiki mbalimbali ikiwamo ukosefu wa haki.

Mengi ya mambo wanayoyaandika wananchi ni mambo ambayo yanaweza kutatuliwa na viongozi wa ngazi za chini katika mfumo wa serikali.

Viongozi hawa wa umma wanapaswa kuhakikisha kwamba mambo madogo yanayowakera wananchi yanapatiwa tiba ili mfumo uende na si kulazimisha kila mara viongozi wakuu kutoa amri.

Hii inatokana na ukweli kwamba mambo hayo mengi yao hayawahusu kiutendaji kwa kuwa malalamiko hayo yangeliweza kumalizwa na watu wa chini kabisa katika mfumo wa utawala na kitendo cha wakubwa kutwisha mzigo wa mabango unaonesha kukosekana kwa uwajibikaji.

Ukiangalia mfumo wa utawala utaona kwamba mengi ya malalamiko hayo yanakwenda sanjari na ukiukaji wa utaratibu wa utawala, ambapo msingi mmoja wa uwajibikaji unasuasua na kubakisha demokrasia ambapo wananchi wanatumia kushitaki kwa viongozi wakuu kupitia mabango.

Aidha kutokana na kutowajibika huko viongozi hao wa kitaifa wamekuwa wakijikuta wakitoa maagizo kila siku wakati watendaji wapo na wanatakiwa kuelewa wajibu wao, hivyo kupunguza maana halisi ya matamko ya viongozi wakuu wa kitaifa.

Mathalani tatizo la wafanyabiashara ndogo limepigiwa kelele mno na viongozi wa kitaifa na sasa inapofika Waziri Mkuu kumwelekeza tena Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha anatafuta eneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo inakatisha tamaa.

Tunasema inakatisha tamaa kwa kuwa hawa watendaji wamepewa maelekezo ya kufanya shughuli hiyo tangu awamu ya tano iingie madarakani na sasa ni miaka mitatu bado wimbo ni ule ule, wekeni maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo.

Hivi tunauliza watendaji hawaelewi na hata kama hawaelewi hawawezi kujiongeza kidogo kutambua kwanini watu hao wanatakiwa kutengewa maeneo?

Haiwezekani kila mara malalamiko na kuondolewa eneo bila kupewa eneo mbadala wala hakuna halmashauri inayokuja na mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ndogo wanaweka eneo muafaka na kudumu.

Tunasema ifike wakati wakurugenzi wajipime wenyewe kama wanafaa kuendelea kubaki katika nafasi zao wakati wao ndio wanaopanga bajeti zinazostahili kwa ajili ya kuwaondolewa wananchi kero zao.

Ni vyema watendaji wakaelekeza nguvu zao katika kukabili shida za wananchi na kuzitatua, hivyo kuwaacha watendaji wakuu wa serikali wakifanya shughuli ya kusimamia sera ili kuipaisha nchi zaidi katika nyanja mbalimbali.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hayuko ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi