loader
Picha

Miaka 19 ya kifo cha Mwalimu J.K. Nyerere

OKTOBA 14 mwaka huu, Watanzania tutaadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere. Ni miaka 19 sasa imepita tangu Mwalimu atutoke. Hakika siku hii sasa imekuwa muhimu sana kwetu Watanzania.

Maana, Watanzania wanazidi kutambua kuwa Mwalimu Nyerere, pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu katika uhai wake, siku zote alisimama upande wa wanyonge walio wengi.

Mwalimu aliitazama zaidi Tanzania kuliko chama alichokiongoza. Mwalimu alidhamiria kuwakomboa Watanzania kifikra ili waondokane na unyonge na umasikini wao. Hakika Nyerere alikuwa kiongozi wa kanuni, kilichokufa ni kiwiliwili, fikra zake ziko hai na atabaki milele katika mioyo ya Watanzania wengi. Mwalimu aliwataka Watanzania waamke.

Na hapa nitasimulia visa viwili vinavyotukumbusha wajibu wetu wa kuamka sasa kutoka usingizi wa pono. Hapo zamani palipata kutokea bwana aliyefanya biashara ya kuuza kofia. Alizipanga kofia zake kichwani.

Alivaa moja na nyingine zikapangana juu yake. Zikawa kama kichuguu. Siku moja wakati akivuka pori akitembeza kofia zake, akajiwa na uchovu. Akaamua kukaa chini ya mti kivulini. Usingizi ukamjia.

Alipoamka akashangaa kuona tumbili wametapakaa juu mitini wakiwa wamevaa kofia. Walimwachia kofia moja tu kichwani mwake. Bwana yule akajaribu kutoa ishara zote kuwataka tumbili wale wamrudishie kofia zake.

Tumbili waliigiza ishara zile, lakini hawakwenda kumrudishia kofia zake. Mwishowe bwana yule akajiwa na busara. Akavua kofia yake na kuibwaga chini ardhini. Tumbili nao, wakiwa juu ya miti, wakafanya hivyo hivyo. Wakazibwaga kofia zile chini. Hivyo basi, bwana yule alifanikiwa kuziokota kofia zake zote. Miaka ikapita, bwana yule hakuweza tena kuendelea na biashara ile.

Aliaga dunia, lakini kabla hajafa alimrithisha mwanawe ambaye pia alimhadithia kisa kile cha tumbili na kofia. Ikatokea siku moja mwanawe katika biashara yake ya kuuza kofia, ikamkuta hali kama iliyomtokea marehemu baba yake. Akafanya kama alivyofanya marehemu baba yake. Ilipofika hatua ya yeye kubwaga kofia yake chini ardhini, tumbili wale walizikamata kofia zao kichwani kwa mikono yao.

Tumbili wale walihakikisha hazianguki ardhini. Naam, wakati ulikuwa umebadilika, tumbili walibadilika pia, lakini mtoto wa mwanadamu hakubadilika. Maana, hata tumbili wale nao walihadithiwa na babu zao kisa cha kuhadaiwa na kufanywa wajinga na binadamu. Walijiandaa kutofanya makosa yale yale waliyofanya babu zao. Na hiki hapa ni kisa kingine; palitokea watu watatu.

Watu hao walikuwa na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Akatokea bwana mmoja akawakabidhi mikungu mitatu ya ndizi. Akawapa pia bahasha yenye barua ndani yake. Akawaagiza; “pelekeni mikungu hiyo ya ndizi nyumbani kwa rafiki yangu”. Njiani watu wale wakajisikia njaa kali. Wakautafuna mkungu mzima wa ndizi. Walipofika mwisho wa safari, wakaikabidhi mikungu ya ndizi na barua ile kwa mwenyeji wao.

Mwenyeji aliisoma kwanza barua ile, akawashukuru. Kisha akasema; “Naiona mikungu miwili. Je, uko wapi mkungu wa tatu wa ndizi? Watu wale walitahayari. Walishangaa sana, kuwa bwana yule amebaini kuwa njiani wamekula mkungu mzima wa ndizi! Walirudi nyumbani wakiamini, kuwa bahasha ile waliyopewa ilikuwa na macho. Iliwaona mara ile waliposimama njiani na kula ndizi zile.

Ikatokea tena, wanaume wale wakatumwa na bwana yuleyule, waende mji uleule na kwa rafiki yake yuleyule. Wapeleke tena mikungu mitatu ya ndizi. Njiani wakajisikia tena njaa kali. Wakaambizana; tusimame na tuule mkungu mzima wa ndizi. Lakini, tuhakikishe, kuwa mmoja wetu ameichukua bahasha tuliyobeba. Aiweke ardhini, kisha aifukie kidogo na mchanga.

Halafu aikalie kwa matako, bahasha isiweze kabisa kuona wakati tunatafuna mkungu wa ndizi! Wakamaliza kuutafuna mkungu wa ndizi. Wakahakikisha wametupa maganda porini. Wakafika kwa mwenyeji wao. Wakakabidhi mikungu miwili ya ndizi na bahasha. Wakashangaa sana, kuwa hata safari hii, mwenyeji wao amewauliza tena ulipo mkungu wa tatu wa ndizi.

Wakabaini, kuwa humu duniani kuna maarifa ya kusoma na kuandika. Miaka kumi na tisa baada ya kifo cha Mwalimu, jamii yetu iliyokuwa imezamishwa kwenye bahari ya ufisadi, imeanza sasa, kwenye uongozi huu wa awamu ya tano kuona mwanga wa matumaini.

Hata hivyo, jamii inahitaji elimu zaidi kuweza kuwabaini wezi wao. Ni kwa vile wanajua kuwa bado kuna masalia ya viongozi wezi. Kwamba kuna ‘mikungu yao ya ndizi’ inaliwa njiani na watu waliotakiwa kuifikisha kwa wananchi. Hizi zote ni dalili za Watanzania kuanza kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo. Watanzania wameanza kukemea kwa sauti na bila woga, yale ambayo Baba wa Taifa alikemea wakati wa uhai wake.

Na sasa wanaye Rais John Magufuli mwenye kuwaongoza kwa vitendo. Watanzania wameanza kuwaandama wale wenye kutafuna mikungu yao ya ndizi mchana wa jua kali huku wakidhani, kuwa Watanzania ni wajinga ni vipofu wasioona.

Mapambano haya ni ya lazima, maana tumeshuhudia huko nyuma wachache wenye kuhujumu rasilimali za taifa kwa ufisadi wao walivyoonesha pia dharau kwa umma. Wakiamini kuwa fedha zao zingenunua haki mahakamani. Bob Marley ni mmoja wa wasanii mahiri wa muziki wa reggae waliopata kutokea humu duniani. Msanii huyu alipata kuimba; Unaweza kuwapumbaza watu wachache kwa kipindi fulani, lakini huwezi kuwapumbaza watu wote kwa wakati wote.

WAKATI ninajiandaa kuandika makala haya niliwauliza Oscar Mbuza na Godfrey ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi